2017-04-28 08:31:00

Hija ya kitume ya Papa Francisko nchini Misri ni mwanzo mwema!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya mitandao ya kijamii anasema, anakwenda nchini Misri kama hujaji wa amani katika Misri ya amani! Anataka kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli haki, amani na maridhiano kati ya watu yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani upendo kwa Mungu na jirani! Patriaki Ibrahim Isaac Sedrack wa Kanisa la Wakoptik wa Alexandria nchini Misri anapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri kuanzia tarehe 28 – 29 Aprili 2017, kielelezo cha Mchungaji mwema anayeguswa na shida, mahangaiko na matumaini ya watu wake. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri utasaidia kuwaimarisha ndugu zake katika imani na matumaini pamoja na kuihamasisha familia ya Mungu nchini Misri kujikita zaidi katika mchakato wa haki, amani na maridhiano kati yao!

Ni ukweli usiopingika kwamba, kumekuwepo na mashambulizi ya kigaidi mara kwa mara zinapokariba siku kuu za Kikristo, yaani Noeli na Pasaka, hali inayotishia uhuru wa kuabudu, nguzo ya haki msingi za binadamu. Patriaki Ibrahim Isaac Sedrack anasema, familia ya Mungu imejiandaa kwa sala na kufunga ili kufanikisha hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri inayoongozwa na kauli mbiu “Papa wa amani nchini Misri”. Ni matumaini ya Wakristo nchini Misri kwamba, hija hii ya kitume itasaidia kuimarisha uhusiano kati ya Vatican na Serikali ya Misri, ili kusaidia mchakato wa kulinda, kudumisha na kuendeleza misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Wakristo ni sehemu muhimu sana ya familia ya Mungu nchini Misri kumbe, wanapaswa pia kushirikishwa katika ustawi na maendeleo ya nchi yao na wala si kutengwa na kubaguliwa kana kwamba, wao ni wananchi wa daraja la tatu!

Kanisa nchini Misri limeendelea kuwa mstari wa mbele kwa utoaji wa huduma makini anasema Patriaki Ibrahim Isaac Sedrack katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi. Kanisa linamiliki na kuendesha shule 170. Lina hospitali, zahanati na vituo kadhaa vya afya vinavyotoa huduma kwa wananchi wote wa Misri pasi na ubaguzi, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Uwepo wa Baba Mtakatufu Francisko, Papa Tawadros II, Patriaki Bartlomeo wa kwanza na pamoja na Muhammad Al Tayyib, Imam mkuu  wa Msikiti wa Al-Azhar, Cairo ni muhimu sana wakati huu mgumu wa historia ya wananchi wa Misri wanaopaswa kujiimarisha katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli Misri iweze kuwa ni nchi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Patriaki Ibrahim Isaac Sedrack wa Kanisa la Wakoptik wa Alexandria nchini Misri anapenda kuwatia shime wananchi wote wa Misri kujikita katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano; ustawi na maendeleo ya wengi. Anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko aliyekubali kupokea mwaliko wa Sinodi ya Maaskofu wa Kikoptik ili kutembelea Misri, mwaliko uliotolewa Februari 2016 wakati wa hija yao ya kitume mjini Vatican. Baba Mtakatifu ni kielelezo cha mchungaji mwema, asiyekatishwa tamaa na changamoto za maisha, daima yuko mstari wa mbele katika mchakato wa haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri ni heshima kubwa kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.