2017-04-28 10:23:00

Dini ina dhamana ya kuenzi utu, heshima na haki msingi za binadamu!


Viongozi wa kidini wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanasaidia kujenga na kudumisha utamaduni wa amani duniani unaojikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kudumisha usalama wa watu na mali zao. Viongozi wa kidini wawe mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ili kuondokana na utamaduni wa kifo unaosimikwa hasa zaidi katika misimamo mikali ya kidini na kiimani, ambayo imepekea watu wengi kupoteza maisha  na mali zao kutokana na mashambulizi ya kigaidi!

Haya ni kati ya mawazo makuu yaliyojitokeza kwenye mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa ulioanza kutimu avumbi tarehe 27 Aprili 2017 kwenye Chuo Kikuu cha Al Azhar, kilichoko mjini Cairo, Misri. Kilele cha mkutano huu ni uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni, tarehe 28 Aprili 2017. Viongozi wa kidini wanapaswa kuwasaidia watu kuwa na mwelekeo sahihi kuhusu utakatifu wa maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Raia wote wanapaswa kuheshimiana na kushirikishwa katika mchakato mzima wa maendeleo endelevu pasi na ubaguzi. Vitabu vitakatifu ni muhimu sana katika kukuza imani ya watu, lakini vitabu hivi vinapaswa kuwa tafsiri sahihi ili kufahamu yale mambo makuu yanafumbatwa katika vitabu hivi, vinginevyo ni uwepo wa misimamo mikali ya kidini na kiimani ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha mashambulizi ya kigaidi, changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinolopol anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha uhuru na utu wa binadamu kama nguzo muhimu sana ya ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na mashambulizi ya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia ambayo yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Vitendo vya kigaidi vinaendelea kujenga hofu na wasi wasi kati ya watu kiasi cha baadhi ya watu kudhani kwamba, dini zinachochea mashambulizi ya kigaidi na machafuko. Kimsingi dini zinapaswa kujizatiti kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Mashambulizi ya kigaidi ni kielelezo cha dini kushindwa kusimamia haki, amani na maridhiano kati ya watu. Majadiliano ya kidini yanapaswa kujenga na kudumisha uhusiano mwema kati ya raia wenye imani tofauti kwa kutambua kwamba, dini haipaswi kuwa ni sababu ya choko choko na migawanyiko, bali amana inayopaswa kudumishwa na wote!

Kwa upande wake Patriaki Louis Raphael Sako wa kwanza anasema, kuna haja ya kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ili kujenga misingi ya haki, amani na upatanisho; kwa kukazia haki msingi za raia na wajibu wa serikali kwa raia wake na kwamba, kuna haja ya kutenganisha kati ya dini na serikali, ili kuimarisha haki msingi za binadamu; uhuru wa kuabudu na usawa kati ya wananchi wote. Misimamo mikali ya kidini na kiimani ni kati ya changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi yanaweza kusaidia kukoleza mchakato wa watu kufahamiana, kuthaminiana na kuheshimiana hata katika tofauti zao msingi, dini kisiwe ni kigezo msingi cha utambulisho wa mtu na haki zake msingi, bali usawa. Toba na wongofu wa ndani sanjari na upatanisho wa kweli ni nyenzo muhimu sana katika kujenga na kukuza amani duniani.

Muhammad Al Tayyib, Imam mkuu  wa Msikiti wa Al-Azhar, Cairo mwenyeji wa mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa anasema: usawa miongoni mwa raia, amani na utulivu ni kati changamoto kubwa sana zinazomwandama mwahadamu katika ulimwengu mamboleo. Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaloyaunganisha Makanisa 300 anasema kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa kupambana na misimamo mikali ya kidini na kiimani inayotishia usalama, amani na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Raia watambue kwamba, wana haki zao msingi na wajibu wanaopaswa kuutekeleza mbele ya Serikali na jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.