2017-04-27 10:06:00

Yaliyojiri mkutano wa Baraza la Makardinali washauri!


Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Baraza la Makardinali Washauri kwa muda wa siku tatu, yaani kuanzia tarehe 24- 26 Aprili 2017 wamefanya mkutano wao wa XIX uliokuwa unajadili Mabaraza ya Kipapa ya Uinjilishaji wa watu; Baraza la Kipapa kwa ajili ya kuhamasisha Uinjilishaji mpya; Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja na Baraza la Kipapa la Nyaraka za Sheria pamoja na mahakama zake kuu tatu: Mahakama ya Toba ya Kitume, Mahakama kuu ya Kanisa pamoja na Mahakama kuu ya Rufaa ya Kipapa.

Makardinali wamejadili pamoja na mambo mengine uteuzi na majiundo makini ya wafanyakazi katika Sekretarieti kuu ya Vatican, walei na wakleri! Makardinali wamejadili kuhusu mahusiano kati ya Mabaraza la Maaskofu Katoliki pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, ili kuangalia umuhimu wa kuweza kurudisha baadhi ya madaraka kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, kuliko hali ilivyo kwa wakati huu ambapo maamuzi mengi yanafanywa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican.

Mkutano umewashirikisha pia baadhi ya viongozi wakuu kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican ili kutoa ufafanuzi makini pale ulipokuwa unahitajika! Baraza la Makardinali litafanya tena mkutano wake kuanzia tarehe 12 hadi 14 Juni 2017. Haya yamefafanuliwa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumatano, tarehe 26 Aprili 2017.

Muswada wa Katiba mpya ya Kitume unaendelea kufanyiwa kazi, lakini hadi wakati huu, bado haujakamilika na kwamba, hii ni kazi ambayo bado inahitaji muda ili kutoa nafasi kwa Baraza la Makardinali kutafakari kwa kina na hatimaye, kuwasilisha ushauri wao kwa Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuutolea maamuzi. Kardinali George Pell,amewataarifu Makardinali juu ya hali ya uchumi na udhibiti wa bajeti ya Vatican kwa mwaka 2016. Kardinali Sean O’Malley ametaarifu kuhusu kazi ya Tume ya Kipapa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo, kwa kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa programi za malezi na majiundo makini kama sehemu ya mchakato wa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.