2017-04-27 16:31:00

Papa Francisko: Ombeeni maskini, toba, utakatifu na umissionari


Kila mwaka wakati wa kipindi cha Pasaka, wajumbe wa Mfuko wa Papa wanafanya hija ya maisha ya kiroho mjini Vatican pamoja na kuwasilisha mchango wao unaopania kusaidia juhudi zinazofanywa na Baba Mtakatifu kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Hiki ni kipindi ambacho Mama Kanisa anasherehekea ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti sanjari na maisha mapya kutoka kwa Roho Mtakatifu. Hija ya wajumbe wa Mfuko wa Papa inapania pamoja na mambo mengine pia kuwaimarisha katika imani, matumaini sanjari na kuendelea kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Mchango wao wa hali na mali umekuwa ni msaada mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maisha ya kiroho na huduma ya upendo, ambayo inapewa kipaumbele cha pekee na Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 27 Aprili 2017 amepata bahati ya kukutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Papa. Anasema, ulimwengu mamboleo umesheheni makovu ya vita, chuki na uhasama; na utandawazi usioguswa na mahangaiko na shida za watu wengine! Katika mazingira na changamoto za namna hii kuna haja ya kuonesha ushuhuda wenye mvuto na mashiko ili kutangaza Injili ya matumaini inayofumbatwa katika nguvu ya wokovu, upatanisho na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu; mambo msingi yanayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo!

Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wajumbe wa Mfuko wa Papa kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kulisaidia Kanisa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini hadi miisho ya dunia, daima likijizatiti kutekeleza miradi ya maendeleo ya maisha ya kiroho na kimwili kwa watu sehemu mbali mbali za dunia, hasa zaidi wale wanaoishi katika nchi zinazoendelea duniani. Kila mwamini anaitwa na kuhamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni mjumbe wa umoja na mjenzi wa amani kwa familia yote ya Mungu, mintarafu utashi wa Mungu katika Kristo Yesu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewataka wajumbe wa Mfuko wa Papa kujisadaka zaidi katika sala ili kuombea mahitaji ya maskini duniani, toba na wongofu wa ndani, uenezaji wa Injili pamoja na kukua kwa Kanisa katika utakatifu na ari ya kimissionari. Amewaomba pia kumkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa sala na sadaka yao na hatimaye, akawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.