2017-04-26 12:42:00

Upendo ambao ni kielelezo cha ushindi wa Kristo umeenea duniani kote


Na tazama mimi niko pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari ni ahadi ambayo ilitolewa na Kristo Yesu na hivyo kuwa ni chemchemi ya matumaini ya Kikristo na utabiri wa kinabii unaoonesha uwepo endelevu wa Mungu kati pamoja na watu wake hadi atakaporudi tena kuwahukumu wazima na wafu! Huyu ndiye Immanueli yaani Mungu pamoja nasi! Hili ndilo hitimisho la Injili linalojikita katika Fumbo la Mungu pamoja nasi; Mungu ambaye anatembea na kumwambata mwanadamu; Mungu anayempenda kwa dhati binadamu kiasi hata cha kushindwa kutengana naye!

Kwa bahati mbaya, mwanadamu ana uwezo wa kuchagua nani wa kujenga naye mahusiano na nani wa kuvunjilia mbali daraja linalowakutanisha na kuwauganisha pamoja! Mwenyezi Mungu ana moyo unaowaka mapendo daima hata pale mapendo haya yanapokumbana na moyo wa mwanadamu uliosinyaa kama “plastiki iliyoungua kwa moto”! Mwenyezi Mungu anaendelea daima kumsindikiza binadamu katika safari yake ya maisha, hata pale anapomsahau na hatimaye kumweka pembezoni mwa maisha na mipango yake; pale anapokengeuka  na kupigwa na ubaridi wa imani, lakini daima Mwenyezi Mungu anaendelea kumpenda mwanadamu na kamwe hawezi kumwacha peke yake!

Hii ni sehemu ya katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 26 Aprili 2017 wakati huu anapoendelea kuzama zaidi na zaidi kuhusu matumaini ya ya Kikristo. Katika hija ya maisha ya hapa duniani, daima mwanadamu anasindikizwa na Mwenyezi Mungu, kwani tangu awali Yesu amewahakikishia wafuasi wake kwamba, atakuwa pamoja nao hadi utimilifu wa dahari, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Yote yatakuja na kupita, lakini Neno la Mungu litadumu milele yote, kwani binadamu ni sehemu ya moyo wa Mwenyezi Mungu! Anajali na kumwahangaikia binadamu katika mahitaji yake; anapokuwa katika majaribu na hata pale anapotembea katika giza na uvuli wa mauti!

Hiki ni kielelezo cha uwepo, ukaribu na maongozi ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Matumaini ya Kikristo ni sawa na nanga inayojikita katika uhakika na usalama ambao Mwenyezi Mungu ameahidi na kutekeleza kwa njia ya Kristo Yesu na mwanzo wa mwaliko wa kumfuasa pasi  na kigugumizi. Kwa uhakika huu,  anasema Baba Mtakatifu Francisko, Mkristo anaweza “kuchanja mbuga” katika maisha yake, kwani ajapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, hataogopa mabaya kwa maana Mwenyezi  Mungu yupo pamoja naye daima, huku akimwangazia mapito yake.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuning’iniza matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu, lengo na hatima ya maisha yao. Ikiwa kama waamini watategemea na kuamini nguvu zao wenyewe, watashangaa na kupigwa bumbuwazi, kwani watapotea na kufutika kama ndoto ya mchana, kwani ulimwengu umegubikwa sana na ubinafsi. Waamini watambue kwamba, Yesu yuko pamoja nao, kumbe wanapaswa kuwa na matumaini thabiti katika maisha yao kwa kumwaminia na kumtegemea Mungu ambaye daima atatekeleza kazi yake hata pale ambapo kwa macho ya kibinadamu inaonekana kuwa haiwezekani kabisa! Familia ya Mungu inakumbushwa kwamba daima iko katika safari ya matumaini, inatambua kwamba, upendo wa Mungu unawaambata kwani ushindi wa Kristo Mfufuka umeenea duniani kote! Ushindi huu ni upendo wa Kristo kwa watu wote!

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee amewakumbuka mahujaji na waamini kutoka Poland ambao, katika maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu, wamefanya kumbu kumbu ya miaka 600 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Gniezno, siku maalum pia kwa ajili ya kumkumbuka Mtakatifu Adalbert, Askofu na shahidi ambaye pia ni Msimamizi wa Poland. Huyu ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Poland. Baba Mtakatifu ameiweka familia yote ya Mungu nchini Poland chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Adalbert pamoja na kuwataka kutunza kwa uaminifu Mapokeo yao ya maisha ya kiroho na kitamaduni, ili kuwarithisha pia vijana wa kizazi kipya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.