2017-04-26 13:26:00

Misri tayari kumekucha! Tayari kumpokea baba Mtakatifu Francisko


Baba Mtakatifu Francisko anasema, hija yake ya kitume nchini Misri kuanzia tarehe 28 – 29 Aprili 2017 inapania kuwafariji Wakristo wote huko Mashariki ya Kati pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Askofu mkuu Bruno Musaro’, Balozi wa Vatican nchini Misri anasema, kimsingi maandalizi yote yamekamilika na familia ya Mungu nchini Misri inamsubiri kwa hamu Baba Mtakatifu Francisko mjumbe wa amani aweze kuwatembelea na kuwaimarisha katika umoja, udugu, upendo na mshikamano wa kitaifa tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya amani ndani na nje ya Misri.

Askofu mkuu Musaro katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, ushuhuda wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko umekuwa na mvuto mkubwa kwa watu wengi nchini Misri kiasi kwamba, wanataka kushuhudia hayo wanayoona kwenye vyombo vya habari! Huu ndio ule muda uliokubaliwa wa kuonana mubashara na Baba Mtakatifu Francisko. Ni Baba wa maskini, mtetezi wa wanyonge, anayependa kusimamia ukweli, haki, ustawi na mafao ya wengi.

Ni kiongozi anayejisadaka kwa ajili ya maskini si tu kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake. Ibada ya Alhamisi kuu jioni inayomwezesha Baba Mtakatifu kukutana na watu waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, imekuwa ikiwagusa watu wengi nchini Misri. Watu wanausifu moyo wa ukarimu na ujasiri; upendo na mshikamano wa uekumene wa damu ambao unashuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko, licha ya mashambulizi ya kigaidi yaliyojitokeza nchini Misri na kusababisha  watu kadhaa kupoteza maisha pamoja na miundo mbinu kuharibiwa vibaya sana, lakini Baba Mtakatifu hajakata wala kukatishwa tamaa, yuko tayari kwenda kuwafariji ndugu zake katika Kristo; mashuhuda wa imani wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake!

Serikali ya Misri imeshukuru sana Baba Mtakatifu kwa kuamua kutekeleza azma yake ya kutembelea Misri licha ya changamoto za ulinzi na usalama zilizojitokeza hivi karibuni. Uwepo wa Baba Mtakatifu nchini Misri utasaidia pia kuwa ni kichocheo ya utalii, ikizingatiwa kwamba, mashambulizi ya kigaidi nchini Misri yamepelekea kuchechemea kwa sekta ya utalii ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika bajeti ya serikali. Askofu mkuu Bruno Musaro’, Balozi wa Vatican nchini Misri anasema uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika mkutano wa kimataifa wa majadiliano ya kidini ni muhimu sana katika medani za kimataifa kama sehemu ya mchakato unaopania kudumisha amani, haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi. Kumbe, mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Al- Azhar, Cairo, Misri ni muhimu sana.

Kwa upande wake, Askofu Makarios Tewfik wa Jimbo la Ismayliah, anasema, hii ni mara ya pili kwa Papa kutembelea nchini Misri. Hija ya kwanza ilitekelezwa na Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa maadhimisho wa Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Kimsingi Familia ya Mungu nchini Misri imepokea kwa ari na moyo mkuu ziara ya Papa Francisko nchini mwao. Hii ni faraja kubwa kwa Wakristo na pia ni mchango muhimu sana katika kukuza na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene kwa kuaminiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi za kidini na kiimani.

Papa Tawadros II wa Kanisa la Kikoptik nchini Misri alipokutana na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 alimwalika kutembelea Misri na kumwahidi kwamba, angeweza kutembelea Misri siku moja! Ni kiongozi ambaye ameguswa kwa namna ya pekee na ushuhuda wa Wakristo wanaoteseka kwa kumwaga damu isiyokuwa na hatia; mbegu ya uekumene wa damu! Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa Papa Tawadros II wakati wa Pasaka alikazia umuhimu wa kushikamana kwa dhati katika uekumene wa sala na maisha ya kiroho; uekumene wa damu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili. Mashambulizi ya kigaidi Jumapili ya matawi yaliwasikitisha wapenda haki na amani nchini Misri.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza amealikwa kushiriki pia katika mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa ambao umeandaliwa na Chuo Kikuu cha Al Azhar, Cairo. Hawa ni mashuhuda na vyombo vya amani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Mfufuka. Umefika kwa viongozi wa kidini kukemea kwa nguvu zao zote misimamo mikali ya kidini na  kiimani. Waamini  wa dini mbali mbali wajenge utamaduni wa kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi changamoto wanazokabiliana nazo, ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kwa pamoja kwani hakuna mtu anayeweza kuishi peke yake kama kisiwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.