2017-04-26 07:37:00

Huruma ya Mungu isaidie kuboresha utu na heshima ya binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, dhana inayopaswa kuvaliwa njuga ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Huruma ya Mungu ni sehemu muhimu sana ya mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu anasema Askofu Gianni Ambrosio wa Jimbo la Piacenza-Bobbio katika hotuba yake elekezi kwenye kongamano lililoandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya hivi karibuni huko nchini Sarayevo.

Kongamano hili pamoja na mambo mengine lilipembua kwa kina na mapana changamoto zinazolikabili Bara la Ulaya kwa nyakati hizi na umuhimu wa Kanisa kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Huruma ya Mungu iwaguse pia wanasiasa ili waweze kufikiri na kutenda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Ulaya sanjari na kuonesha mshikamano na wakimbizi na wahamiaji ambao wanaendelea kuteseka na kunyanyasika kana kwamba, si mali kitu!

Ulimwengu mamboleo unakabiliwa kwa kiasi kikubwa na wasi wasi wa usalama wa watu na mali zao kutokana na vita, mashambulizi ya kigaidi, kinzani na mipasuko ya kijamii. Hali ngumu ya uchumi na athari zake wananchi wengi wa Ulaya hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ambao wanakosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha kutokana na ukosefu wa fursa za ajira, matokeo yake ni kundi ambalo limekuwa likitumiwa na baadhi ya wanasiasa kwa ajili ya mafao yao binafsi na kwa kutaka kujijenga kisiasa na matokeo yake ni maandamano yenye vurugu na mapambano na vyombo vya dola.

Athari za mabadiliko ya tabianchi na  majanga na maafa asilia ni kati ya mambo yanayoendelea kukwamisha juhudi za wananchi wengi wa Ulaya kutaka kujikwamua na hali ngumu ya maisha. Kumekuwepo na dhana potofu ya uhuru usiokuwa na mipaka, hali ambayo inapelekea kumong’onyoka kwa kwa maadili na utu wema; kuvunjika kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia! Zote hizi ni changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga kwa mwanga wa Injili ya huruma ya Mungu kwa kumwilisha huruma hii hata katika masuala ya kisiasa, ili watunga sera waweze kuguswa na mahitaji msingi ya binadamu, ili hatimaye, kuyapatia ufumbuzi wa kudumu!

Mshikamano wa kimataifa unaosimikwa katika kanuni auni ukisindikizwa na Injili ya huruma ya Mungu unaweza kuwa ni msaada mkubwa katika kukabiliana na changamoto mamboleo anasema Askofu Gianni Ambrosio wa Jimbo la Piacenza-Bobbio katika hotuba yake, kwani huruma hii ikimwilishwa kikamilifu inaweza kugusa akili na nyoyo za watu kiasi cha kuweza kubadilika. Karama ya ugunduzi inapaswa kwanza kabisa kutekelezwa na wale ambao wamekabidhiwa dhamana na madaraka ya kuwaongoza watu. Jambo la msingi ni kukuza na kudumisha Injili ya haki na amani; upatanisho na maridhiano kati ya watu. Kwa njia hii, kuna haja ya kuwa na miwani ya huruma ya Mungu ili kuangalia madhara ya umaskini, magonjwa na ujinga mambo yanayoendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu!

Viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii waangalia sababu zinazopelekea watu kugeuka kuwa wakimbizi na wahamiaji, ili kwa mwanga wa huruma ya Mungu wasaidie kuwakirimia katika mahangaiko yao. Huruma ya Mungu ni chachu ya kutafuta majibu ili kukabiliana na changamoto, shida na magumu yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo pasi na kukata wala kujikatia tamaa. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu kuondokana na ubinafsi na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao na badala yake kujikita katika utamaduni wa upendo na mshikamano, unaojali kwanza kabisa: utu na heshima pamoja na haki msingi za binadamu.

Huruma ya Mungu isaidie kuondoa matabaka ya kijamii kwa watu wachache wanaofaidika na rasilimali za nchi wakati kuna kundi kubwa la watu wanaoteseka kutokana na umaskini wa hali na kipato! Sera za kisiasa na kijamii zikifumbatwa katika huruma ya Mungu, binadamu atapewa kipaumbele cha kwanza, uchumi utajielekeza katika kujibu mahitaji msingi ya binadamu na wala si kwa ajili ya kutafuta faida kubwa kwa kuweka rehani utu, heshima na tunu msingi za maisha ya binadamu! Huruma inatabia ya kusikiliza kwa makini na kujibu kwa wakati, daima utu wa binadamu ukipewa msukumo wa pekee.

Huruma ni chachu ya uwajibikaji makini, upendo na mshikamano kati ya watu, ili kujenga dunia inayosimikwa katika umoja, udugu na mshikamano wa kweli! Ni changamoto inayowataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa upatanisho badala ya “kutunishana misuri” kwa malumbano ya mashambulizi ya kivita kama inavyojionesha kwa sasa ili kweli haki, amani na maridhiano yaweze kufikiwa na kuwaambata watu. Daima ikumbukwe kwamba, vita haina pazia! Huruma iwe ni chachu ya majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa kuwashirikisha wadau wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko, kamwe asiwepo mtu anayetengwa, bali majadiliano yajenge madaraja ya watu kukutana na kujadiliana mustakabali na hatima ya maisha yao!

Mama Thereza wa Calcutta ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha ya watu kwa kuwajali na kuwasaidia maskini. Uchumi wa dunia uwe ni kwa ajili ya: maendeleo endelevu na huduma kwa binadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani. Vinginevyo anasema Baba Mtakatifu Francisko pasi na huruma, mikutano na makongamano ya kimataifa, kikanda na kitaifa yatabakia kuwa ni “maneno matupu ambayo kamwe hayawezi kuvunja mfupa”! Utamaduni wa watu kukutana utasaidia kudumisha utu na heshima ya binadamu katika ujumla wake; utawawezesha watu kufahamiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi na hatima yake ni kuaminiana. Dhana ya huruma iwajengee watu uwezo wa kuganga na kuponya madonda ya vita, kinzani na utengano. Kimsingi, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, dhana ya huruma itaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kutoka katika hali ya unyonge na udhaifu wa kushindwa kutekeleza maamuzi yake msingi kutokana na wasi wasi, woga na hofu zisizokuwa na mvuto wala mashiko. Injili ya huruma ya Mungu, iwasaidie wanasiasa kutoa kipaumbele cha pekee kwa mafao ya wengi badala ya kujikita katika ubinafsi na hali ya kujitafuta wenyewe. Huruma iwajengee watu uwezo wa kujadiliana na kushirikishana katika ukweli na uwazi, daima utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza anasema Askofu Gianni Ambrosio wa Jimbo la Piacenza-Bobbio, katika hotuba yake elekezi kwenye kongamano la Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.