2017-04-25 15:47:00

Papa: Tangazeni na kushuhudia Injili kwa unyenyekevu na moyo mkuu!


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Aprili, anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Marko, Mwinjili. Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 25 Aprili 2017 ametolea nia ya Misa kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea waamini wa Kanisa Kikoptik na kwa namna ya pekee, Papa Tawadros II. Itakumbukwa kwamba, Kanisa la Alexandria lilianzishwa na Mwinjili Marko. Baba Mtakatifu anawaombea waamini wote wa Alexandria baraka na neema, ili kweli Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki na kuwatunza watu wake!

Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa pia na  Baraza la Makardinali washauri linaloendelea na kikao chake hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kwa Wakristo kutoka kifua mbele ilikutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, badala ya kubweteka na kutafuta usalama wa maisha katika mambo mpito! Wakristo wameitwa na kutumwa na Kristo Yesu kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, ili wale wasiomfahamu Yesu wapate nafasi ya kutangaziwa Injili ya wokovu.

Hija hii inapaswa kumwambata mtu mzima katika maisha yake: kiroho na kimwili kama wanavyotangaza na kushuhudia Injili ya Kristo wagonjwa wanaotolea shida na mahangaiko yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ni tukio la furaha, imani na matumaini, linalotangazwa kwa njia ya unyenyekevu wa maisha na kuondokana na tabia ambazo zinaweza kuwa ni kikwazo katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Habari Njema ya Wokovu inafumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu na utukufu wa Kristo Mfufuka. Huu ni mwaliko kwa waamini kushinda kishawishi cha kutaka kumezwa na malimwengu: kwa kuwa na uchu wa mali na madaraka, bali watambue kwamba, wanatangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Waamini watambue kwamba, daima watakutana na vishawishi katika safari ya maisha yao ya kiroho, kumbe, wanapaswa kuwa makini kwa kusimama imara!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu baraka ya kutoka katika ubinafsi wao, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, hata kama watakabiliwa na nyanyaso na madhulumu, bali wawe imara na thabiti katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kristo Mfufuka daima atakuwa pamoja na waja wake wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu. Ikumbukwe kwamba, kila Mkristo anaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya wokovu kwa watu wa Mataifa. Fumbo la Umwilisho ni kashfa kwa baadhi ya watu, lakini kwa Wakristo ni kielelezo cha huruma, upendo na uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.