2017-04-25 16:15:00

Padre Paul Lontsie-Keune ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Yokadouma


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Eugeniusz Juretzko wa Jimbo Katoliki Yokadouma nchini Cameroon la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa sana Padre Paul Lontsie –Keune kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Yokadouma. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule alikuwa ni Gombera wa Seminari kuu ya Maroua-Mokolo na ni mzaliwa wa Jimbo Katoliki la Bafoussam.

Askofu mteule Paul Lontsie –Keune alizaliwa kunako tarehe 25 Agosti 1963 Jimboni Bafoussam, nchini Cameroon. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi kunako tarehe 17 Machi 1991 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na kuingizwa Jimbo Katoliki la Bafoussam. Kati ya mwaka 1991 hadi mwaka 1994 alipelekwa na Jimbo kwenda kuchukua masomo ya juu. Kati ya mwaka 1995 - 1998 alikuwa ni Paroko usu na Mkurugenzi wa Chuo cha “Saint Jean Baptiste”. Kati ya mwaka 1998- 2008 alipewa dhamana ya kuwa Katibu mkuu wa Idara ya Elimu Jimbo, Jaalim na Mlezi pamoja na kuwa ni Paroko usu. Kuanzia mwaka 2008 hadi kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Aprili 2017 kuwa Askofu alikuwa ni Gombera wa Seminari kuu ya St. Augustin huko Maroua-Mokolo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.