2017-04-25 15:25:00

Kard. Parolin simameni kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira!


Kifo ni ukweli unaofahamika na wote na wala hakuna upinzani, lakini ufufuko kwa wafu ni kiini cha imani ya Wakristo na matumaini ya maisha na furaha ya uzima wa milele kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu ameshinda: dhambi na mauti, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, imani kwa Kristo Mfufuka inakuwa ni dira na mwongozo katika maisha yao, tayari kupambana na changamoto za maisha kwa imani na matumaini zaidi. Imani inapaswa kukua na kuongezeka ili kumpatia mwamini mwelekeo mpana zaidi wa maisha.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumapili tarehe 23 Aprili 2017 katika Ibada ya Maadhimisho ya Misa Takatifu kwenye “Villaggio della Terra” yaani “Kijiji cha Dunia”, ili kuonesha umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote, kielelezo makini cha kazi ya uumbaji. Wasi wasi na mashaka kuhusu Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu  ni jambo la kawaida kabisa kama ilivyotokea kwa Mitume na wafuasi wa Kristo, hata kwa waamini wa nyakati hizi wasishangae hata kidogo kwani ni sehemu ya mchakato wa maisha ya kila siku katika imani.

Hata siku ile Yesu alipopaa kwenda mbinguni bado Mitume na wafuasi wake waliendelea kushangaa kwani kushangaa ni sehemu ya maisha ya binadamu kama alivyoshuhudia Mtakatifu Toma, kinara wa imani haba kama kiatu cha raba! Lakini akabahatika kuimarishiwa imani yake na Kristo Mfufuka. Kardinali Parolin, anawaalika waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Kristo Mfufuka kama ambavyo hatimaye Mtume Toma alivyoweza kukiri: Bwana wangu na Mungu wangu! Kanisa la Mwanzo lilishikamana katika umoja, upendo na udugu; waamini wakawa tayari kushirikishana rasilimali zao kwa ajili kukidhi mahitaji ya jirani zao; wakatambulikana kwa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; wakadumu katika sala na ibada!

Huu ni ushuhuda wa Kristo Mfufuka unaopaswa kuwa ni utambulisho wa Jumuiya za Wakristo hata kwa nyakati hizi, ushuhuda ambao unamwilishwa kwa namna ya pekee na Chama cha Kitume cha Wafokolari ambacho kimekuwa mstari wa mbele katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Itakumbukwa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa tarehe 23 Aprili 2017 imeadhimisha Siku ya Utunzaji wa Mazingira Kimataifa. Chama hiki pia anasema Kardinali Parolin, kimekuwa mstari wa mbele katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kukuza na kudumisha amani duniani. Anawataka waendelee kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, changamoto pevu inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Siwe iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”!

Makubaliano ya utekelezaji wa Itifaki ya Paris ya Mwaka 2015 juu ya udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi unahitaji mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa ili kufanikisha utekelezaji wake, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi hazichagui wala kubagua nchi maskini wala tajiri, wote wanaathirika ingawa kwa viwango tofauti. Hii ni changamoto ya kuwekeza katika teknolojia rafiki na mazingira. Utekelezaji huu ni hatua kubwa katika mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza mamilioni ya watu katika umaskini wa hali na kipato.

Wanasayansi na watetezi wa mazingira wanasema, utekelezaji wa itifaki hii unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu. Jambo la msingi ni kupunguza hewa ya ukaa sanjari na kudhibiti uchafuzi wa mazingira. Kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa anapaswa kuhakikisha kwamba anachangia kwa hali na mali katika mchakato huu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa, bila kusita na kutumbukia tena kwenye uchafuzi wa mazingira. Hii ni changamoto kwa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba wanatekeleza kwa dhati Ajenda ya Maendeleo Endelevu Ifikapo mwaka 2030.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.