2017-04-25 14:58:00

Heri wale waliolala katika usingizi wa milele katika Kristo Yesu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe  24 Aprili 2017 majira ya alasiri, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameongoza Ibada ya Mazishi ya Kardinali Attilio Nicora aliyefariki dunia, Jumamosi tarehe 22 Aprili 2017 akiwa na umri wa miaka 80. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali. Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao!

Kardinali Sodano katika mahubiri yake anasema, haya ni maneno ya faraja yanayomsindikiza Marehemu Kardinali Nicora katika safari yake ya mwisho hapa duniani, baada ya kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 80 tangu kuzaliwa hivi karibuni! Hiki ni kitabu cha maisha kilichoandikwa kwa ushuhuda wa huduma makini kwa Kanisa la Kristo! Ushuhuda huu umejionesha kwa namna ya pekee tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo kuu la Milano, kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Verona na hatimaye, Kardinali akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Kanisa la Kiulimwengu na kwamba, jina lake litaendelea kukumbukwa kati ya wateule wa Mungu.

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea na kumsindikiza Marehemu Kardinali Nicora yamefanyika wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Kipindi cha Pasaka, kwa kumshangilia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa kusema Aleluiya! Ufufuko wa Kristo ni msingi na kiini cha imani ya Kikristo. Kanisa linaimba Aleluiya hata katika Ibada ya mazishi kwani lina matumaini katika ufufuko wa wafu kama alivyowahi kuandika Mtakatifu Jerome. Waamini wanakumbushwa kwamba, Yesu ni njia ya kwenda nyumbani kwa Baba wa milele kama anavyokaza kusema Mwinjili Yohane kwamba wasifadhike mioyoni mwao, bali wamwamini Mwenyezi Mungu na Kristo wake kwani amekwenda mbinguni ili kuwaandalia makao, ili aweze kuwachukua na kuwaweka mahali alipo yeye!

Kardinali Angelo Sodano anasema, ujumbe wa matumaini unapaswa kuwa ni dira na mwongozo wa waamini kwa nyakati zote: wakati wa furaha, wakati wa majaribu na taabu. Huu ni mwelekeo ambao unawaletea waamini faraja na wokovu kwani Paulo mtume anaandika akisema, “Spe salvi facti sumus” yaani “tumeokolewa kwa imani”. Huu ndio ujumbe wa matumaini ambao Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ameliachia Kanisa katika Waraka wake wa kitume “Spe salvi” yaani “Matumaini yanayokoa”. Ni matumaini haya ambayo yamewakusanyisha waamini kuzunguka Altare ya Bwana kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Kardinali Attilio Nicora aliyefariki dunia akiwa na matumaini ya ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo.

Ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wa yale yote aliyotenda katika maisha ya Mtumishi wake Kardinali Nicora. Wakati Baba Mtakatifu Francisko anabariki sanduku la maiti ya Kardinali Nicora, kwaya ilisikika ikiimba “Malaika wakusindikize Paradisi, Malaika wakupokee katika mji Mtakatifu wa Yerusalem ya mbinguni, ili uweze kupata pumziko la milele. Hii ndiyo iliyokuwa pia sala ya familia ya Mungu iliyokutanika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kumwombea na kumsindikiza Marehemu Kardinali Attilio Nicora kwenye usingizi wa amani anasema Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.