2017-04-24 15:06:00

Papa Francisko: Padre Milani alitoa upendeleo wa elimu kwa maskini!


Padre Lorenzo Milani, Mkuu wa nyumba ya kitawa ya Barbiana katika maisha yake alijiwekea utamaduni wa kukimbilia mara kwa mara katika kiti cha huruma ya Mungu ili kuomba toba na msamaha wa dhambi zake kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya huruma ya Mungu na Mama mpendelevu kwa watoto wanaokimbilia huruma na tunza yake ya kimama! Hivi ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa onesho la vitabu lililoandaliwa Jimbo kuu la Milano kuanzia tarehe 19 - 23 Aprili 2017. Huyu ni Padre ambaye alisadaka maisha yake kwa ajili ya kuandika vitabu, akaitupa dunia akiwa na umri wa miaka 44.

Ni kiongozi ambaye alibahatika kuwa ni mwalimu na mlezi wa vijana; tunu msingi alizorithishwa kutoka katika familia yake ambayo haikuwa na imani na wakati mwingine, ilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa Mapadre. Ni tabia ambayo aliibeba katika maisha yake, kiasi kwamba, hata wakati mwingine alikuwa ni mgumu na wengi walishindwa kumwelewa hata baada ya toba na wongofu wake wa ndani kunako mwaka 1943, wakati anatekeleza dhamana na wajibu wake wa kichungaji kama Padre. Haya ni mambo yanayoweza kujionesha katika maandiko yake mintarafu mfumo wa elimu, upendeleo kwa maskini pamoja na kusimama kidete kulinda na kudumisha uhuru wa dhamiri.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kulipenda na kulithamini Kanisa hata kama limejeruhiwa vibaya. Lakini elimu inayotolewa na Kanisa inawasaidia watu kuwa na upeo mpana kuhusu uhalisia wa maisha kwa kufungua akili na nyoyo zao, kiasi kwamba, wanaweza kuwa ni jasiri kukabiliana na ukweli wa maisha. Shuleni watu wanajifunza kwanza kabisa mambo msingi na baadaye wanajielekeza kwa mambo msingi kwani shule ni mahali ambapo mtu anajifunza kujifunza na baada ya kujifunza kujifunza anaendelea kujifunza zaidi kwani elimu haina mwisho.

Huu ni ushuhuda wa wema na upendo kwa wanafunzi wake aliotamani kuwapatia utu na chachu ya upendo kwa Kristo na Injili yake; kwa Kanisa na Jamii, huku akitamani na kuota kwamba, shule iwe ni hospitali wazi katika uwanja wa vita ili kuwaokoa na kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Lengo ni kuwapatia ujuzi, kufahamu na kuzungumza kwa weledi, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao msingi. Haya ni mambo ambayo Padre Lorenzo alipenda kuyatumia hata wakati wa mahubiri yake na maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa.

Yesu Kristo alikuwa ni mwanga, dira na mwongozo wa maisha ya Padre Lorenzo, ingawa kivuli cha Msalaba kimeyaambata sana maisha yake, lakini ndani mwake, alihisi kwamba, alikuwa anashiriki kikamilifu katika Fumbo la Pasaka, Yesu akawa ni Baba wa maisha yake ya kiroho na akatamani kuitupa dunia akiwa ni Padre Mkristo. Mateso, mahangaiko na Msalaba wa maisha, kamwe hayakuzima mwanga wa Pasaka ya Kristo Mfufuka ndani mwake, kwani ndani mwake, alitaka kuonesha upendo wa dhati kwa wanafunzi wake wadogo kama anavyofundisha Kristo Yesu. Padre Milani akawa ni mfano bora wa kuigwa kwa wanafunzi wake, kiasi cha kutamani kwamba, Wakleri wote wangekuwa kama yeye! Kwa kujisadaka kwa ajili ya maskini anaweza kuimba utenzi wa sifa kwa kusema, heri maskini maana ufalme wa mbinguni ni wao!

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika washiriki katika onesho hili la vitabu kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa Padre Lorenzi Milani, shuhuda wa Kristo na Injili yake aliyejitahidi kumtangaza, kumshuhudia kwa kumsamehe dhambi zake kwa njia ya mwanga wa wema, neema na faraja; tunu msingi ambazo waamini wanaweza kuzipata kwa kukutana na Kristo Yesu ndani ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.