2017-04-24 10:59:00

Papa Francisko: Endeleeni kukumbatia na kuambata huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 23 Aprili 2017 amefafanua kwa kina na mapana maana ya Jumapili ya Pili ya Pasaka kadiri ya Mapokeo ya Kanisa na mwendelezo wake kama Jumapili ya huruma ya Mungu, ambamo Kanisa linatumwa na Kristo Yesu kuwa ni chombo cha huruma na upatanisho kwa kuwaondolea watu dhambi zao! Jumapili ya Pili ya Pasaka inajulikana kama “In Albis” yaani “Jumapili nyeupe”, siku ambayo Wakristo waliobatizwa kwenye mkesha wa Pasaka walikuwa wanavua mavazi yao meupe, yaliyokuwa yana maanisha utu mpya wa watoto wa Mungu waliozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Mavazi haya meupe anasema Baba Mtakatifu wakati huo yalivaliwa kwa muda wa juma zima, kumbe, Jumapili Nyeupe ilikuwa ni mwanzo wa maisha mapya ndani ya Kristo Mfufuka na Kanisa lake!

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo aliamua kuipatia Jumapili hii umuhimu wa pekee na kuwa ni Jumapili ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ni muda mfupi tu, Kanisa limefunga maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kujichotea nguvu na neema zinazobubujika kutoka katika huruma ya Mungu. Injili ya Siku inaonesha jinsi ambavyo Yesu alivyowapatia mitume wake dhamana ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa kuwapatia Roho Mtakatifu.

Pasaka ya Bwana inakuwa ni fursa nyingine kwa waamini kuweza kuonja huruma ya Mungu kwa njia ya msamaha wa dhambi. Yesu Mfufuka analipatia Kanisa dhamana ya kuwatangazia watu huruma na msamaha wa Mungu, unaowakirimia waamini amani, utulivu wa ndani na furaha inayobubujika kwa kukutana na Kristo Mfufuka. Huruma ya Mungu katika mwanga wa Pasaka ni kielelezo cha ufahamu ambao unaweza kuchukua mtindo mbali mbali katika maisha ya mwanadamu yaani: kwa kutumia milango ya fahamu, kwa kufundishwa, lakini kubwa zaidi ni kwa njia ya mang’amuzi ya huruma ya Mungu inayofungua akili na nyoyo za watu ili kuweza kufahamu kwa kina na mapana zaidi Fumbo la maisha ya Mungu na maisha ya mtu binafsi.

Huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba: vita, chuki, uhasama na ubaya wa moyo ni mambo ambayo hayana msingi kabisa na kwamba, waathirika wakubwa ni wale watu wanaofungwa katika hali kama hizi, kwani ni mambo yanayowapokonya utu wao. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Huruma ya Mungu anaendelea kusema Baba Mtakatifu Francisko inawasha moto wa upendo mioyoni mwa watu, kwa kuguswa na mahitaji yao pamoja na kuwashirikisha. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuishi kwa furaha yote haya.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, ameyaelekeza mawazo yake huko Oviedo, nchini Hispania, ambako, Kardinali Angelo Amato, Jumamosi tarehe 22 Aprili 2017 kwa niaba ya Baba Mtakatifu amemtangaza Padre Luis Antonio Rosa Ormières kuwa Mwenyeheri ambaye aliishi kunako karne ya kumi na tisa. Mwenyeheri Padre Luis alijisadaka bila ya kujibakiza, akatumia karama na mapaji yake ya maisha ya kiroho na kiutu kwa ajili ya kuwekeza zaidi katika elimu kwa maskini. Akabahatika kuanzisha Shirika la Watawa wa Malaika Mlinzi. Sala na ulinzi wake viwasaidie anasema Baba Mtakatifu Francisko wadau mbali mbali wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza katika sekta ya elimu. Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni, amewashukuru wale wote waliomtumia salam na matashi mema ya Siku kuu ya Pasaka. Anapenda kuwarudishia tena kwa moyo huo wa ukarimu, huku akiwaombea heri na baraka kutoka kwa Kristo Yesu Mfufuka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.