2017-04-24 15:32:00

Maandalizi ya Jubilei ya miaka 50 ya Uhamsho wa Kikatoliki yaanza!


Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia tangu tarehe 22 - 25 Aprili 2017 kinaadhimisha mkutano wake wa 40 unaosindikizwa na kauli mbiu “Furahini: Bwana ametenda hayo: Shangilieni: Bwana ameufunua utukufu wake”. Hili ni tukio la sala na uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha unaofumbatwa katika uhalisia wa aisha ya waamini. Hiki ni kipindi cha sala na tafakari ya kina; muda wa maombi hasa kwa ajili ya wagonjwa na wale wanaoteseka kiroho na kimwili. Ni wakati uliokubalika wa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kishindo kama mwanzo na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho haya yanafanyika mara tu baada ya kufunga rasmi Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kwa namna ya pekee maadhimisho ya Mwaka huu yanawalenga hasa vijana, familia na wakleri!

Hii ni sehemu ya utangulizi wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Duniani. Kilele cha maadhimisho haya kitafanyika mjini Roma kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Siku kuu ya Pentekoste kwa mwaka 2017. Kwa kutambua uzito wa tukio hili katika maisha na utume wa Kanisa, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu amemtumia ujumbe Dr. Salvatore Martinez, Rais wa  Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia, akiwatakia heri na baraka katika maadhimisho haya.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, anawataka Wanachama wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia kubaki wakiwa wameshikamana kwa dhati katika upendo na kwamba, umoja huu unapaswa kuonekana. Kanisa linawataka kushuhudia mwanga wa ushuhuda huu unaopaswa kuwaangazia wote ili kamwe asiwepo mtu ambaye ananyimwa mwanga wa nguvu ya Injili. Baba Mtakatifu anawatakia mafanikio makubwa katika maadhimisho haya pamoja na kuendelea kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Anawaalika hata wao, kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umesomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Angelo Giovanni Becciu, Katibu mkuu Msaidizi wa Vatican aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu katika ufunguzi wa maadhimisho ya 40 ya Chama cha Uhamsho wa Kikristo nchini Italia. Katika mahubiri yake, amekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa Injili katika maisha ya waamini, kama dira na mwongozo wao. Waamini wajibidishe kumsifu, kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Kikanisa.

Karama yao inayofumbatwa katika Roho Mtakatifu iwe ni chachu ya kumtambua Kristo Yesu katika maisha, daima wakijitahidi kushinda giza la utepetevu wa imani na kushuhudia kwa walimwengu, mwanga wa upendo angavu! Waamini wanaendelea kuhamasishwa kujikita katika mchakato wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili, sanjari na kuambata Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa waja wake! Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Duniani kuanzia tarehe 31 Mei hadi tarehe 4 Juni 2017 kitakuwa kinaadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Viongozi wakuu wa Chama hiki tayari wako mjini Roma, hawa ni akina Michelle Moran, Rais Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Kimataifa pamoja na Gilberto Gomes Barbarosa, Rais wa Udugu wa Kikatoliki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.