2017-04-24 14:50:00

Iweni mashuhuda amini wa Fumbo la Ufufuko!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu tarehe 24 Aprili 2017 amewataka waamini kuwa imara katika imani yao kwa Kristo Mfufuka na kamwe wasikubali kuyumbishwa hata kidogo. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa pia na Baraza la Makardinali washauri ambalo linakutana mjini Vatican chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 24 hadi 26 Aprili 2017 ili kuendeleza mchakato wa mageuzi kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa na Makardinali wakati wa mikutano yao elekezi!

Waamini wanakumbushwa kwamba, kwa njia ya Roho Mtakatifu wamewekwa huru na hivyo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ari na moyo mkuu, pasi na makunyanzi. Kuhusu kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, Yesu alitumia nafasi hii kwa upole na uvumilivu kumfafanulia Nikodemo maana na umuhimu wa kuzaliwa kutoka juu, yaani kuzaliwa katika Roho Mtakatifu; kutoka katika malimwengu na kuanza kuambata mambo ya mbinguni, kama ilivyojitokeza kwenye Somo la kwanza kwa Mitume Petro na Yohane kuelezea kwa kina na mapana bila kupapasa papasa macho kwamba yule kiwete ameponywa kwa nguvu ya Kristo Mfufuka.

Katika vitisho, bado Mitume waliweza kusimama kidete katika imani kwa kusema kwamba, wao kamwe hawawezi kuacha kuyanena mambo waliyoyaona na kuyasikia. Baba Mtakatifu anakaza kusema, imani ya Kikristo inafumbatwa katika uhalisia wa maisha kwani Neno wa Mungu amefanyika mwili na huu ndio ukweli wa imani inayongamwa na Wakristo katika Kanuni ya Imani na wala hakuna kitu cha kuweza kuwababaisha kwani wanao ujasiri, ari na moyo mkuu kutoka kwa Roho Mtakatifu anayewawezesha kusimamia ukweli huu na kuutolea ushuhuda kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kwa Baraza kuu la Wayahudi, hakuna Fumbo la Umwilisho, bali kwao Yesu amefanyika kuwa ni sheria inayopaswa kutekelezwa hadi nukta ya mwisho. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, hata katika historia ya Kanisa kumekuwepo na nyakati ambapo Kanisa limeyumba katika Mafundisho yake kwa kukazia zaidi sheria na kusahau kwamba, Kanisa limewekwa huru kwa njia ya Roho Mtakatifu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwamba, Kristo Yesu ni Bwana! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu awakirimie mwanga utakaowaimarisha katika imani ili kweli waweze kuwa na ujasiri wa kuishuhudia, kwani wao wamezaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu, kumbe wanapaswa kuishi na kutenda kadiri ya imani yao bila kuwa na shingo ngumu, bali kwa njia ya ushuhuda wa uhuru wa wana wa Mungu unaowawajibisha kumtangaza Kristo Yesu, aliyejifanya mwanadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.