2017-04-24 06:30:00

Ibada kwa Bikira Maria na Huruma ya Mungu ni nyenzo msingi kiroho


Katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima, yaani Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos, Baba Mtakatifu Francisko kwa heshima ya Bikira Maria, ameamua kuwatangaza Wenyeheri Francis na Yacinta Marto kuwa watakatifu wakati wa hija yake ya kitume nchini Ureno kuanzia tarehe 12- 13 Mei 2017. Itakumbukwa kwamba, hili ni tukio la tatu kuadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko nje ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, baada ya kumtangaza Mtakatifu Joseph Vaz tarehe 14 Januari 2015 nchini Colombo na Mtakatifu Junìpero Serra, tarehe 23 Septemba 2015, nchini Marekani.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ureno inaongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mjini Fatima 2017 pamoja na Bikira Maria kama mahujaji wa matumaini na amani”. Padre Wojciech Adam Koscielniak, Msimamizi mkuu wa Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakaribisha mahujaji kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Musoma waliofika kituoni hapo Jumamosi, tarehe 22 Aprili 2017 ili kuadhimisha Jumapili ya huruma ya Mungu, amewatafakarisha kuhusu maneno ya Yesu Msalabani, “Tazama, Mama yako! Tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua Bikira Maria nyumbani mwake”.

Kumbe, Ibada kwa Bikira Maria na Ibada ya huruma ya Mungu ni nyenzo muhimu sana katika hija ya kuutafuta na kuukumbatia utakatifu wa maisha pamoja na kuendelea kuwa wafuasi aminifu wa Kristo sanjari na mashuhuda wa huruma ya Mungu hapa duniani. Anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kutambua na kuthamini dhamana na nafasi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa katika ufuasi wao. Bikira Maria ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu, Mtumishi mwaminifu na mwalimu mkuu katika shule ya huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake. Ni nyota angavu inayowasindikiza waamini katika hija ya kumwendea Baba wa milele!

Padre Wojciech Adam Koscielniak katika mahubiri yake anasema, Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa katika mapambano ya maisha ya kiroho, kwani ni kielelezo cha Eva mpya, Sanduku la Agano, Mlango wa huruma ya Mungu na mbingu, Nyota angavu ya asubuhi na Mama wa mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Bikira Maria alikingiwa dhambi ya asili, kielelezo makini cha upendeleo wa Mungu katika maisha yake, akamkinga na dhambi pamoja na mauti, ili aweze kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa, tayari kuwasaidia waamini kumfuasa Kristo kwa ujasiri na moyo mkuu. Huu ni mwaliko wa kuingia katika shule ya upendo inayoongozwa na kusimamiwa na Bikira Maria.

Hapa waamini wanapaswa kukubali kuona kwa jicho la imani mateso na mahangaiko ya Bikira Maria tangu siku ile alipopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu hadi aliposimama chini ya Msalaba na kushuhudia Mwanaye mpendwa akiinamisha kichwa na kukata roho! Waamini wajitahidi kumchukua Bikira Maria katika maisha yao kwa kujiweka wakfu kwa Bikira Maria; kwa kusali na kutafakari Rozari ambayo kimsingi ni muhtasari wa Injili, yaani: maisha, utume na historia ya kazi nzima ya ukombozi na kwamba  hii ni Biblia ya waamini wa kawaida! Waamini wajenge na kudumisha Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria pamoja na kufanya mapilizi kwa ajili ya dhambi za walimwengu. Ili kukuza na kudumisha moyo na ari ya Ibada kwa Bikira Maria kuna haja ya kujikita katika fadhila ya: imani, utii, unyenyekevu, huruma, uwajibikaji pamoja na kujiaminisha kwa Kristo Yesu!

Padre Wojciech Adam Koscielniak katika mahubiri yake kwenye mkesha wa Jumapili ya huruma ya Mungu amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumjifunza Kristo Yesu kutoka katika Fumbo la Msalaba, ufunuo wa utimilifu wa huruma ya Mungu, tayari kuwa ni mitume na mashuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu kwa waja wake, katika ukweli na haki; katika utakatifu na unyofu wa moyo, tayari kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji, dira na mwelekeo kwa Baba wa milele! Mtakatifu Faustina Kowalska na Yohane Paulo II ni mitume na mashuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu ambayo kwa sasa inavaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko.

Fumbo la Msalaba linalofumbata mateso na kifo cha Kristo ni kilele cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Yesu Kristo Mfufuka ni yule yule: Jana na leo; nyakati zote ni zake. Waamini wawe na ujasiri wa kupokea mateso na mahangaiko katika maisha yao kwa imani na matumaini kama kielelezo cha mateso yanayookoa badala ya kukimbilia kuambata imani za kishirikina! Waamini wajitahidi kuifanya midomo yao kuwa ni lango la huruma ya Mungu, kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu; kwa kuupenda na kuuthamini Msalaba, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Kristo Yesu. Kwa ajili ya mateso makali ya Yesu Msalabani, waamini wapate huruma pamoja na walimwengu wote! Padre Wojciech Adam Koscielniak anahitimisha mahubiri yake katika mkesha wa Jumapili ya huruma ya Mungu kwa kuwawekea waamini mbele yao mitume wa huruma ya Mungu ambao kwa sasa ni Sr. Faustina Kowalska, Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na Padre Mikaeli Sepocko kutoka Poland ambaye alikuwa ni baba wa maisha ya kiroho wa Sr. Faustina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.