2017-04-24 08:49:00

Askofu Amani: kumong'onyoka kwa kanuni maadili na utu wema ni hatari!


Hivi karibuni nchini Tanzania kumekuwepo na matukio mbali mbali yanayoashiria kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya kimaadili na utu wema; mambo yanayohatarisha misingi ya haki na amani; umoja wa kitaifa na mafungamano ya kijamii. Kumekuwepo na matukio ya baadhi ya watu kupotea katika mazingira tatanishi; askari Polisi kuuwawa kikatili na baadhi ya watanzania kufurahia tukio hili ambalo kimsingi linasikitisha sana kwani kuna maisha ya watu waliokuwa wanatekeleza dhamana na wajibu wao wa ulinzi kwa raia na mali zao, waliouwawa kikatili wakiwa kazini! Kumekuwepo na dalili za maovu na vitisho kuongezeka nchini Tanzania!

Ufufuko wa Kristo uwe ni ushindi dhidi ya vitendo vyote hivi vinavyohatarisha amani, usalama, ustawi na mafao ya wengi! Huu ni mwaliko wa nguvu ambao umetolewa na Askofu Isaac Amani Massawe wa Jimbo Katoliki Moshi wakati wa mahubiri yake kwenye Siku kuu ya Pasaka. Matukio yote haya ni viashiria kwamba, misingi ya haki, amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, yanaendelea kumeng’enyuliwa na baadhi ya watu kwa mafao yao binafsi. Kuna haja anasema Askofu Amani kwa watanzania kuondokana na maovu yanayojikita katika mawazo, akili na hatimaye kutekelezwa kwa vitendo.

Umefika wakati wa kukazia na kudumisha tunu msingi za kimaadili na utu wema kwa kuondokana hata na imani za kishirikina zinazopelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia sanjari na nyanyaso za kijinsia. Askofu Amani anasikitika kusema kwamba, vitendo hivi vyote vinalipaka matope taifa la Tanzania na kuanza kulitumbukiza katika ombwe na giza la hofu na wasi wasi kwa kukosa mwanga wa matumaini katika maisha. Haya ndiyo matunda ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia yasiyozingatia kanuni maadili na utu wema. Ni matokeo ya ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; ulevi wa kupindukia, matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na imani za kishirikina, hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi!

Itakumbukwa kwamba, Askofu Augustine Shao wa Jimbo la Zanzibar, katika ujumbe wake wa Pasaka kwa Mwaka 2017 alikazia kuhusu umuhimu wa Pasaka kuwa ni ushindi wa dhambi na mauti na mwanzo wa mchakato wa amani na furaha ya binadamu wote. Ufufuko wa Kristo Yesu uwe ni nguvu ya wanyonge na maskini, ili kushughulikia maovu yanayoiandama Tanzania katika mwanga wa Injili ya haki, amani na umoja wa kitaifa.

Ufufuko wa Kristo uwe ni ujumbe wa matumaini na furaha kwa watanzania wote kwa kupambana kufa na kupona na vitendo vya rushwa na ufisadi; matumizi mabaya ya madaraka pamoja na rasilimali ya taifa. Ufufuko wa Kristo uwe ni ujumbe kwa viongozi kuwajibika barabara ili kuwaondolea watanzania kero mbali mbali za maisha, ili kuwajengea matumaini ya maisha bora zaidi kwa kuwekeza katika elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi. Ikumbukwe kwamba, Tanzania itajengwa na watanzania wenyewe na wala hakuna njia ya mkato! Watanzania wafanye kazi na kuwajibika barabara kwa kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.