2017-04-22 14:35:00

Mshikamano wa kimataifa kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu


Kardinali Giovanni Battista Re katika tafakari yake kuhusu kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Populorum Progressio” yaani “Maendeleo ya watu” alipenda kukazia kwa namna ya pekee kabisa: utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili. Aliitaka Jumuiyaya Kimataifa kujenga na kudumisha mshikamano wa dhati unaojikita katika kanuni auni, ili kuweza kutumia rasilimali na utajiri wa dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi kwa kutambua kwamba, maendeleo ni jina jipya la amani duniani! Kiini cha Waraka huu ni maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili!

Huu ni ushuhuda wa kinabii ambao kamwe hauwezi kupitwa na wakati na kwamba, ni changamoto inayohimiza mshikamano unaofumbata kanuni ya auni ili kuweza kukabiliana na matatizo na changamoto mbali mbali katika maisha ya binadamu kwa kutumia rasilimali na utajiri ambao Mwenyezi Mungu amewakirimia binadamu wote pasi na ridhaa yao; utajiri ambao unapaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kardinali Giovanni Battista Re anasikitika kusema kwamba, Waraka huu unaonekana kusahauliwa na wengi, lakini unagusa mambo msingi ya kijamii na kiuchumi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia!

Mwenyeheri Paulo VI anakaza kusema, maendeleo endelevu yanayosimikwa katika ukweli yanamhusisha mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, yanasimikwa katika mshikamano unaoongozwa na kanuni auni ili kuifanya dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa kuyapatia ufumbuzi wa kudumu matatizo, mahangaiko na changamoto zinazomwandama binadamu hasa katika masula ya elimu, afya na ustawi. Mwenyeheri Paulo VI alitamani kuona dunia ambamo watu wanaweza kuishi maisha marefu wakiwa na afya bora, wenye elimu ya kutosha kupambana na mazingira na kutiisha ulimwengu; dunia ambamo misingi ya haki, amani na ustawi wa wengi vinapewa kipaumbele cha kwanza. Kwa maneno machache huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa na kudumishwa na wote!

Maendeleo ya binadamu yanapaswa kusimikwa katika mshikamano wa dhati ili kupambana na umaskini, ujinga, njaa na magonjwa yanayomwandama mwanadamu. Waraka huu ni changamoto kwa familia ya Mungu katika ujumla wake anasema Kardinali Giovanni Battista Re katika tafakari yake Mama Kanisa anapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipotia mkwaju kwenye Waraka wake wa Kitume “Populorum progressio” yaani “Maendeleo ya watu” hapo tarehe 26 Machi 1967.

Ni maendeleo ya wote wale walioko kwenye Nchi tajiri zaidi duniani na wale ambao bado wanajikongoja kutafuta maendeleo ya kweli. Maendeleo ya kweli ni jina jingine la amani duniani, kiu ya watu wengi kwa sasa ni kuona kweli kwamba, haki, amani na maridhiano kati ya watu yanaendelezwa na kudumishwa ili watu waweze kujikwamua kutoka katika shida na changamoto mbali mbali zinazowasibu! Amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha binadamu; amani ni utamaduni unaopaswa kuvaliwa njuga na wote kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii vinakwamisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, ndiyo maana Mama Kanisa anakazia umuhimu wa kujikita katika kulinda, kutunza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Maendeleo endelevu ya binadamu ni kiini cha Mfundisho Jamii ya Kanisa. Sera na mikakati ya kiuchumi ilenge kwa namna ya pekee kukidhi mahitaji msingi ya binadamu, kwa kusimamia utu, heshima na ustawi wake, vinginevyo, ikiwa kama uchumi utajikita katika kutafuta faida kubwa, matokeo yake ni ndiyo hayo ya athari za mkitikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa: leo hii fursa za ajira zinapatikana kwa manati!

Vijana wengi wa kizazi kipya hawana matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kiasi hata cha kushindwa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao! Huu ni uchumi wa fedha na vitu na wala si uchumi unaomwambata binadamu na mahitaji yake msingi! Maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi, wapewe kipaumbele katika sera na mikakati ya maendeleo kitaifa na kimataifa, bila kuzingatia mahitaji msingi ya makundi ya watu hawa, amani kamwe haitaweza kupatikana! Binadamu lazima awe ni kiini cha maamuzi, sera na mikakati mbali mbali, ili yote haya yatekelezwe kama sehemu ya mchakato wa huduma kwa binadamu katika kukidhi mahitaji yake msingi kwa kupambana na umaskini, ujinga na maradhi.

Binadamu anapaswa kujengewa uwezo anasema Kardinali Giovanni Battista Re wa kupambana na mazingira pamoja na changamoto za maisha, ili kujiletea maendeleo ya kweli! Ili kufanikisha muktadha huu kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga uchumi jamii unaowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi; kwa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano; kwa kuimarisha utandawazi wa huruma, upendo na mshikamano unaowawezesha hata akina Lazaro maskini, walau kuambulia “sahani ya supu nzito” kutoka kwenye meza za matajiri wa dunia hii. Mwenyeheri Paulo VI alianzisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa upendo na mshikamano. Maendeleo ya watu ni mchakato unaopania kutoa kipaumbele kwa binadamu, haki na amani; upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mataifa, changamoto pevu inayopaswa kuvaliwa njuga na wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.