2017-04-22 09:33:00

Jumapili ya kutangaza Injili ya: Huruma, Imani, Amani na Matumaini!


Mama Kanisa leo anaadhimisha Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya huruma ya Mungu iliyotangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 30 Aprili 2000 wakati wa kumtangaza Mwenyeheri Sr. Faustina Kowalska kuwa Mtakatifu. Lengo la Jumapili ya huruma ya Mungu ni kuwasaidia waamini kukimbilia ili kujizamisha katika bahari ya huruma ya Mungu kwa kuadhimisha Sakramenti za huruma ya Mungu kwa uchaji na moyo mnyofu, ili hatimaye, huruma hii iweze kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, sehemu muhimu sana ya mchakato ya kuwa na huruma kama Baba wa mbinguni alivyo na huruma, tayari kuambata utakatifu wa maisha!

Tunaweza kusema, leo Kanisa linaadhimisha Jumapili ya huruma na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka! Liturujia ya Neno la Mungu inatuonesha imani ya Mitume wa Yesu baada ya ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Hii ni Jumuiya ya kwanza iliyotikiswa na kupigishwa magoti kutokana na Kashfa ya Msalaba. Mitume wakasambaratika na kutokomea kusikojukana kama umande wa asubuhi, kiasi hata cha kupoteza imani kwa Kristo Yesu. Liturujia ya Neno la Mungu inatusaidia kuisoma tena Injili kwa mwanga wa Kristo Mfufuka, Mwinjili Yohane akimweka mbele ya macho yetu Mtakatifu Toma, aitwaye Pacha, aliyekuwa na imani haba kama kiatu cha raba! Akataka kugusa Madonda Matakatifu ili apate kusadiki. Lakini, Yesu anasema heri wale wasioona, wakasadiki!

Heri ninyi mnaompenda na kumfurahia Yesu anasema Paulo, ingawa hamjamwona. Hii ndiyo imani ya wale wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu! Hawa ndio wale wanaounda Jumuiya mpya ya Wakristo inayosimikwa katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu! Hii ni Jumuiya Kipentekoste inayojikita kwa kusikiliza Mafundisho ya Mitume, kwa kushikamana katika umoja, upendo na udugu na kumwilisha huruma ya Mungu kwa maskini na wahitaji zaidi. Ni Jumuiya inayotambulikana kwa kuadhimisha Sakramenti za huruma ya Mungu, tayari kushuhudia furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Ufalme wa Mungu kati ya watu wake.

Amani kwenu! Ni salam inayotolewa na Yesu Mfufuka kwa Mitume wake waliovunjika na kupondeka moyo! Anawarudishia tena amani na utulivu wa ndani, ili kuthibitisha ukweli wa Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake; kiini cha imani ya Kanisa inayoadhimishwa kwa kishindo kila Jumapili, yaani Siku ya Bwana, Kanisa linapokumbuka siku ile Mwenyezi Mungu alipokamilisha kazi ya uumbaji na kupumzika! Ni Siku ambayo Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu endelevu ya Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ndiyo maana Jumapili ni Siku ya Kristo!

Ni Siku ya Kanisa, kwani waamini wanajumuika kusikiliza Neno la Mungu na kulishwa chakula cha Malaika, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Siku ya mapumziko inayorutubishwa kwa matendo ya huruma! Huu ndio utajiri unaofumbatwa katika Siku hii ambayo Kristo Yesu anawarejeshea tena waja wake imani, amani, furaha na matumaini tayari kutoka kifuambele ili kushuhudia Injili ya furaha. Si Siku ya kwanza ya Juma ambamo Wakristo wanakusanyika kusali, kusikiliza Neno la Mungu, kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu na kumegewa tena amani ya Kristo Mfufuka; chemchemi ya imani, umoja, upendo na mshikamano; kielelezo makini cha vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa.

Leo Kanisa linaadhimisha Jumapili ya huruma ya Mungu na Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ni Uso wa huruma ya Baba wa milele inayojidhihirisha katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Huruma ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu linalojidhihirisha katika kazi ya uumbaji, ukombozi na utakaso. Huruma ni bahari ya upendo na msamaha wa Mungu kwa waja wake, ndiyo maana Baba Mtakatifu anaendelea kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kupewa: ukuu, sifa na shukrani na mwanadamu kutakatifuzwa kwa kuzamishwa katika huruma na upendo wa Baba wa milele!

Yesu ameifunua huruma ya Mungu kwa njia maisha, mafundisho yake yaliyojikita katika ukweli na haki; kwa njia ya miujiza yake: kwa kuwaondolea watu dhambi na kuwarejeshea tena hadhi ya kuitwa wana wa Mungu kwa kuwaondoa kwenye dhiki na taabu zao mbali mbali. Yesu aliwasamehe hata wale watu wake wa karibu kama akina Mtakatifu Toma aitwaye Pacha kwa kumpatia nafasi ya kugusa tena Madonda yake Matakatifu na Toma akaungama imani yake kwa kusema, Bwana wangu na Mungu wangu! Uinjilishaji mpya anasema Baba Mtakatifu Francisko unajikita katika ushuhuda wa huruma ya Mungu.

Yesu Mfufuka aliwaambia Mitume wake, kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia na kuwaambia pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu kwa namna ya pekee inaadhimishwa katika Sakramenti ya Upatanisho, kwa sababu inamfanya mtu aguse kwa mkono wake ukubwa a huruma ya Mungu na hivyo kuwa kweli ni chimbuko la amani na utulivu wa ndani. Mapadre waungamishi wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni watumishi waaminifu wa msamaha wa Mungu, kwa kuonesha ile sura ya Baba mwenye huruma kwa waamini wanaokimbilia kiti cha huruma ya Mungu. Huruma na msamaha wa Mungu uendelee kuwagusa watu wengi zaidi.

Kanisa linaishi kwa kuungama, kuihibiri, kuitangaza na kuishuhudia huruma ya Mungu, ili kuwaelekeza watu njia inayowapeleka kwa Baba wa milele. Leo tunahamasishwa tena kuwa na huruma kama Baba wa mbinguni alivyo na huruma! Tuyasikie maneno ya Yesu akisema leta mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye! Tukuze na kuimarisha imani kwa Kristo Mfufuka na kuendelea kujitahidi kutangaza na kushuhudia Injili ya amani, upendo na mshikamano, tayari kuwatangazia jirani zetu Injili ya matumaini mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.