2017-04-22 10:11:00

Jifunzeni huruma ya Mungu kutoka kwa Kristo na mashuhuda wake!


Mitume wa Huruma ya Mungu - Mashahidi wa Injili halisi ya Huruma. Rejea. Gal 1:1-9: “Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia; Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu. Utukufu una yeye milele na milele, Amina.  Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.

Wote wanaokusudia kuhubiri Injili, wanapaswa kwanza kuusoma na kuutafakari Waraka huu wa Mtakatifu Paulo kwa Wagalatia. Mtakatifu Paulo alielekeza Waraka wake kwa Kanisa mahalia lililokuwa uwanja wa mgongano kati ya Injili halisi na si-Injili (mpinga-Injili, anti-Gospel). Ukisoma vizuri Waraka huo, utagundua kwamba Paulo anauandika akiwa amefadhaika, akiwa katika hali ya hisia nzito, hivyo anatumia lugha nzito na misamiati mikali sana. Anasema - “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.” Hii ni lugha ambayo kimsingi haitumiki tena katika Kanisa letu. Baba Mtakatifu Yohane wa XXIII na Baba Mtakatifu Paulo VI wakati wa Mtaguso wa Pili wa Vatikano walisema mara kadhaa kwamba kwa karne nyingi ilikuwa rahisi kupita kiasi kuwafukuza watu Kanisani.

Lakini Mtakatifu Paulo anasema - unahubiri Injili? Umebarikiwa. Unahubiri si-Injili? Umelaaniwa. Kumbe, haitoshi kuwa mwanakanisa ili ubarikiwe na Mungu. Waraka kwa Wagalatia uliandikwa na Paulo kwa Wakristo, Wanakanisa Hai wa eneo la Galatia la wakati ule. Paulo anaona hatari kubwa sana inayoibuka katika Makanisa changa, ndiyo maana anawaandikia Wakristo wa Galatia kwa ukali - hakuna Injili nyingine, tofauti na ile tuliyowahubiri. Wapo tu watu fulani fulani wanaowavurugia vichwa vyenu na roho zenu. Katika jumuiya hizo za waamini wa Galatia, kumbe, sambamba na Injili sahihi mafundisho potofu yalihubiriwa vilevile. Hatari aliyoiona Paulo mwanzoni kabisa mwa historia ya Kanisa, ipo na inashamiri sana katika Kanisa letu hata nyakati zetu hizi.

Lugha yetu inatakiwa kuwa - ‘ndiyo, ndiyo; hapana, hapana’. Ndiyo maana ama unahubiri Injili na unabarikiwa kwa sababu hiyo, ama unakubali si-Injili na unalaaniwa. Hakuna njia nyingine. Mitume wa Huruma ya Mungu - Mt. Sista Faustina, Mt. Yohane Paulo II na M.H. Padre Mikaeli Sopoćko walihubiri Injili halisi ya Yesu Mfufuka halisi, Bwana wa Huruma, with uncompromising spirit and resolve!

Paulo anaandika: “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.” (Gal 1:6-7)  Kwa nini Wakristo wa kwanza walimuacha Yesu upesi hivi? Kwa sababu Injili fake, si-Injili inavutia zaidi na hivyo ni rahisi kuacha Injili ya kweli na kuambatia mafundisho ya watu matapeli. Wakristo wanachangamkia sana mafundisho hayo na wanajisikia vizuri kukiri na kuishi kwa misingi ya mafundisho hayo. Inatosha kuona vidhehebu vingi vingi vinavyoibuka kila kukicha kama uyoga na kutushawishi kwa nyimbo, makofi, dansi, vizawadi na kelele za vipaza sati. Na Yesu alishatuonya zamani - ‘watatokea watu, wakisema hivi na hivi. MSIWAFUATE.’

Injili ya Mtakatifu Paulo ni Injili ya Huruma ya Yesu anayetuhesabia haki na kutuweka huru. Hii ni Injili ya neema. Si-Injili ni mafundisho yanayokuletea dhana kwamba mwanadamu mwenyewe kwa matendo yake anaweza kujihesabu kuwa mwenye haki, anaweza kuokoka kwa nguvu zake mwenyewe.  Sisi tulikombolewa kwa neema huru ya Mungu kwa sadaka ya Yesu Msalabani. Lakini si-Injili inadai kuwa sisi wenywe tunaweka mahesabu yetu na Mungu sawa kwa njia ya kutii Sheria. Injili ni ujumbe wa Huruma, si-Injili ni ujumbe wa uwezekano wa kuhesabiwa haki kwa misingi ya matendo yetu sisi wenyewe. Mgongano huo upo katika Kanisa letu na unaendelea kuwepo. Nasi tukijitazama vizuri katika ukweli, tutagundua kwamba wengi wetu tuliopo hapa, ni wafuasi wa si-Injili. Tunafanana na Mfarisayo hekaluni anayejisifu mbele ya Mungu kwa sababu anatimiza kikamilifu vigezo na masharti ya dini yake. Lakini siye yeye aliyeondoka Hekaluni akihesabiwa haki, bali ni mtoza ushuru yule.

Si-Injili tunaipenda na inatuvutia sana. Tunapenda kuwa na hakika kwamba wokovu wetu ni haki yetu. Tunapenda kitabu cha Mawaridi ya Sala amabcho hakina idhini ya Kanisa Katoliki - maana humo ndani tunakutana mkusanyo wa ajabu wa sala mbalimbali ambazo zimewekewa ahadi mbalimbali. Ukisali sala hii - tayari muda fulani umepunguziwa mateso ya Toharani. Ukisali hii - utapata hiki. Eti Mungu ni ATM. Chomeka kadi ya sala, mashine inajibu unavyotaka wewe.  Hatutaki kusimama mbele ya Mungu kama watu ambao wanamwia kitu chochote. Tunataka kusimama mbele ya Mungu katika hisia kwamba sisi wenyewe tumejistahilishia wokovu wetu kwa matendo yetu na si kwamba wokovu wetu ni mastahili ya Mungu. Ipo hatari kwamba endapo tunakiri si-Injili, basi, hatuwapeleki watu kwa Yesu na kwamba hatutakutana na Yesu katika Roho Mtakatifu.

Tuwatazame Mitume wa Huruma ya Mungu, tusome mafundisho yao katika Shajara ya Sista Faustina, katika mahubiri, nyaraka na vitabu vya Papa Yohane Paulo II, katika vitabu na mahubiri ya Pd. Mikaeli Sopoćko - Baba mwungamishaji wa Sista Faustina ambaye tunamwia kufahamu Ujumbe wa Huruma ya Mungu kwa sababu Padre huyo ndiye aliyemuamuru Sista Faustina kila kitu alichokuwa anakiona na kusikia kutoka kwa Yesu alipokuwa anamtokea. Bila Padre huyo huenda ujumbe huo usingetufikia maana Sista Faustina alikuwa hataki kuandika akijiona hastahili na hata elimu yake ni ndogo maana alikomea darasa la nne tu la shule ya msingi. Katika mwanga wa mafundisho na misimamo ya Mitume hao wa Huruma ya Bwana tujihoji kama tunakubali kuongozwa na kupelekwa kwa Yesu wa kweli wa Injili ya kweli?

Kristo huyo mwingine asiye wa kweli ni nani, basi? Katika Waraka wake Mt. Paulo anasema kwamba huyo ni Kristo asiye na Msalaba wake. Ndiyo maana anawahoji Wagalatia - “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?” (Gal 3:1) Anayeshika njia ya kuhesabiwa haki na kuokoka kwa matendo yake mwenyewe, huyo hahitaji Msalaba wa Yesu. Ndiyo maana Yesu baada ya Ufufuko wake alikuwa anawaonyesha wafuasi wake Madonda yake Matakatifu kama kitambulisho cha uhalisia wake. Ni mimi - tazameni alama za Mateso yangu, alama za Msalaba wangu! Yesu asiye na Madonda Matakatifu, Yesu asiye na Msalaba wake - si Yesu wa kweli. Ni Yesu fake! Anayeshika njia ya “self-justification” hana Roho Mtakatifu maana Roho Mtakatifu alimiminwa na Yesu kutoka Msalabani na kuvuviwa kwa Mitume wake na Yesu Mfufuka mwenye alama za Mateso yake.

Kumbukeni Kuhani alichokifanya mwanzoni mwa Misa Takatifu ya Usiku wa Pasaka: alitumia msumari kuchora ishara ya Msalaba kwenye mwili wa mshumaa wa Paska pamoja na herufi ya Alpha na Omega na tarakimu za mwaka huu. Kumbukeni maneno ya Nabii Isaya aliyeandika maneno ya Mungu Mwenyezi: “Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu.” (Is 49:14-16a) Kitendo cha kuchora alama kwa kutumia msumari kwenye mshumaa wa Pasaka ni ukumbusho wa maneno haya. Mungu Mwenyezi amemchora kila mmoja wetu kwenye viganja vya mikono yake, tena si kwa nyoya ya njiwa iwe kazi rahisi na isiyoleta maumivu bali kwa misumari, tena ni misumari ile iliyompigilia Yesu Msalabani.

Ndiyo maana Yesu Mfufuka, Yesu wa Huruma, anajitambulisha kwa wafuasi wake kwa kuwaonyesha mikono na miguu yake - makovu ya misumari mwilini mwake ni ID card yake, ni kitambulisho halali cha Taifa la Watakaofufuliwa! Inatushangaza kwamba wafuasi walipata shida sana kumtambua Yesu baada ya Ufufuko wake. Mariamu alimtambua kwa sauti yake tu alipomwambia - Mariamu! Wengine katika kuumega mkate tu. Wengine kwa kutazama madonda yake matakatifu. Kumbe, uso wa Yesu Mfufuka na mwili wake wa utukufu vimebadilika. Na tusishangae kwamba hakuna aliyeweza kumtambua Yesu kwa urahisi kwa sababu hakuna mtu aliyewahi kukutana na mtu aliyefufuka! Tutajua tu haya mambo yakoje tutakapofufuliwa na sisi. Kwa sasa ni fumbo kubwa. Kukutana na mtu anayetoka ng’ambo ile ya Uzima wa milele na Yerusalemu mpya ya mbinguni kunaleta ugumu. 

Lakini Yesu Mfufuka ni Yesu Mteswa pia. Yesu ni yule yule, jana leo na hata milele! Makovu ya misumari mwilini mwake ni utambulisho wa uhalisia wake! Kumbe, kitambulisho cha Taifa la Watakaofufuliwa ni makovu ya misumari miilini mwetu! Misumari inayotokana na maisha ya Mkristo ya kujitoa sadaka daima na kuishi kwa ajili ya wengine na kubeba msalaba kwa uaminifu na kwa moyo radhi. Kumbukeni Injili ya Mt. Mathayo, sura ya 25 - kwa ajili ya sifa zpi tutahukumiwa siku ya Ufufuko wetu? Si kwa matendo ya huruma na upendo na maisha ya kuishi kwa ajili ya wengine? Na kama katika maisha yako yote kazi moja tu unayofanya ni maisha ya ubinafsi, uchoyo, ya kutafuta raha na maslahi yako tu, maisha ya kuepuka shida, matatizo, magonjwa na msalaba - unaopewa na Mungu ili ujitengenezee kitambulisho chako cha Mfufuliwa? Utajitambulisha kwa kitu gani basi siku ya Ufufuko wako?

Tafakari kwa kina.  Wafuasi walimtambua Yesu kwa Madonda yake Matakatifu. Baba wa mbinguni atatambua watoto wake watakaofufuliwa siku ya mwisho kwa madonda yao matakatifu katika nafsi zao kwa imani, kwa uvumilifu, kwa moyo radhi, wakibeba misalaba yao mpaka mwisho kwa uaminifu na kutenda mema na huruma kwa majirani zao. Na kama wewe utakuwa tu na kitambulisho cha safari zako za kwenda kwa wachawi na waganga wa kienyeji katika jitihada zako za kuepuka shida na msalaba katika maisha yako, basi, nakupa pole. Utakalosikia siku ya mwisho  sipati picha.

Ndiyo maana, wapendwa Mahujaji, siku ya Ijumaa Kuu tunabusu Msalaba wa Bwana. Tunathubutu kuubusu kwa sababu moja tu - Yesu huyo Mteswa ni Mfufuka, maana amefufuka siku ya tatu. Na kwa sababu hiyo tendo hili la upendo kwa Yesu Mteswa na Msulibiwa tunaweza kulisoma pia kama tendo la kuuelewa na kuukubali msalaba katika maisha yetu sisi wenyewe. Kumbe, siku ya Ijumaa Kuu unapoubusu Msalaba wa Yesu unaubusu vilevile msalaba wako! Swali linakuja hapa - je, unajua ni nini ambacho ni msalaba katika maisha yako? Unafahamu msalaba wako? Unaukubali? Utaubusu? Utautumia kwa wokovu wa watu wengine kama Yesu alivyofanya? Unajua kwa nini unaweza kuubusu msalaba wako? Kwa sababu Yesu Msulibiwa ni Mfufuka. Amefufuka. Kwa hiyo msalaba wangu hautaniua. Bali kwa msalaba wangu ninaingia katika Uzima mpya wa Taifa la Wafufuka.

Tafakari jambo jingine pia. Bwana wetu alipokuwa Msalabani katika Mateso kwa ajili yetu, Yesu alipewa mdomoni siki kwenye sifongo iliyochomekwa juu ya hisopo. Mnakumbuka kwamba Wayahudi walipaka damu milango yao usiku wa Pasaka yao ya kuondoka Misri kwa kutumia hisopo ili Malaika wa kifo awapite asiwadhuru? Mlango wa mwanadamu ni mdomo wake, ni kinywa chake. Kwa mdomo wangu nawasiliana na watu na ulimwengu, kwa mdomo wangu najitambulisha. Mdomo wangu ni lango la maneno yangu, lango la ulimwengu wangu wa fikra, wa mtazamo, wa hoja na mawazo yangu.

Mdomo wangu unaweza kuwa Lango la Huruma au lango la ukatili na ujeuri: Katika mdomo wa Yesu pale Msalabani, katika Lango lake hilo la Huruma, hakuna neno baya lolote lilitoka akiwa katika mateso makali sana. Neno muhimu kuliko maneno yote ya Yesu msalabani lilikuwa ni neno BABA - ABBA! Mt. Luka anasimulia Mateso hayo ya Bwana kana kwamba siku ya Ijumaa Kuu ilikuwa ni tukio la kumshawishi Yesu asimwone Mungu tena kama Baba yake anayempenda. Lakini Yesu msalabani anamwita Mungu akisema - ABBA - Daddy!  Tunapata fundisho gani hapa?  Ewe Mkristo mwenzangu, usione haya kuubeba msalaba wako. Bali umshukuru Baba wa Huruma kwa kukufananisha na Mwanaye Yesu. Uukubali na kuubusu. Ni msalaba wako. Ni mali yako. Ni ufunguo wa Lango la Huruma la Nyumba ya Baba Mbinguni. Kwa mfano wa Yesu Msalabani, uendelee kumwita Mungu kama Baba yako mpendwa, Baba wa Huruma ukiwa kwenye vipindi vya mateso sana. Umkimbilie Baba tu. Huu ndio msalaba ambao wokovu wako na wa dunia umetundikwa juu yake, Njooni, njooni, njooni, tuuabudu!

Katika maisha yako ya kawaida usione haya Msalaba wa Yesu na msalaba wako kwa kuuvaa kwa fahari shingoni mwako. Askofu anabeba msalaba kifuani, sisi Mapadre tuna beji ya msalaba wetu, Masista wanavaa misalaba yao waziwazi, wewe je? Usivae msalaba nje - kwenye mkufu au katika rozari - siku zile tu unapokuwa na shida ya kumwona Askofu au padre ofisini, eti, akuone wewe ni mcha Mungu na hivyo akusaidie. Usiwe mnafiki na Yuda Iskariote.  Vaa Msalaba kila siku, usiku na mchana, si kwa kujionyesha, bali kwa kuthibitisha kwamba huukimbii msalaba uliopewa na Mungu. Uutambue na uubusu na uuthamini. Ni wa kwako. Msalaba wako utakutengenezea ID card yako ya Taifa la Watakaofufuliwa - madonda matakatifu nafsini mwako. Ukiupuza na kuukataa, Mungu hatakutambua siku ya kufa kwako.  Ni kwa alama za Mateso ya Msalaba tu Yesu alijitambulisha kwa wanafunzi wake, nao walimtambua. Ni kwa alama za Mateso ya Msalaba wako, Mungu Baba atakutambua siku ya kufa kwako.

Ujifunze kufanya Ishara ya Msalaba kwa ibada, heshima kubwa kabisa, unyenyekevu na uchaji. Ishara hii ni takatifu, ishara hii ni kitambulisho cha Mfalme na Kuhani wa Agano Jipya. Kuanzia sasa usiukufuru. Usithubutu kuutumia Msalaba kama heleni sikioni mwako au kwenye bangiri. Marufuku! Chukizo kubwa mbele ya Bwana! Weka Msalaba wa Bwana katika kila chumba ukutani na sebuleni katika altare ya familia. Tazama Picha ya Yesu wa Huruma aliyotupatia Yesu mwenyewe kupitia kwa Sista Faustina kama chombo maalum cha kutushirikisha Huruma yake. Katika picha hiyo   Madonda Matakatifu ya Yesu ni ujumbe nambari wani. Viganja vyake na miguu. Na Donda la Moyo wake linaloshine kwa mionzi  / miali ya Damu na Maji.  Rozari ya Huruma tuliyosali katika Novena iliyotangulia Sherehe hii huzungumza juu ya Mateso na Kafara ya Yesu Msalabani. Baba wa milele, ninakutolea Mwili na Damu, Roho na Umungu wa Mwanao Mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristo, kwa kulipia dhambi zetu na dhambi za dunia nzima. Kwa ajili ya Mateso Makali ya Yesu, utuhurumie sisi na dunia nzima.

Yesu wa Huruma ni Yesu Mteswa, Yesu-Kafara, Yesu Mfufuka. Mtume wa Huruma ya Mungu hana budi kuwa mtu anayekubali Mateso, Mtu-Kafara aliye tayari kutoa sadaka ya maisha yake kwa Mungu, kwa Kanisa na kwa wokovu wa watu; Mtu aliyefufuka pamoja na Yesu kutoka maisha ya dhambi na utumwa wa shetani kwa maisha mapya. Tazameni na someni maisha ya Sr. Faustina, Papa Yohane Paulo II na Pd. Mikaeli Sopoćko - ni maisha ya mateso, magonjwa, misalaba ya kila aina, kukataliwa na watu, dhihaka, upweke, uchungu na mashambulizi ya Yule Mwovu. Ukielewa fumbo la maisha ya Mtume halisi wa Huruma, basi, ushuhuda wa Ukristo wako na ujumbe wa Huruma ya Mungu utakuwa na uzito na hautapuuzwa na watu.

Mitume wa Huruma ya Mungu - Mt. Sr. Faustina, Mt. Yohane Paulo II na Mwenye Heri Padre Mikaeli Sopocko, mtuombee!!

Na Padre Wojciech Adam Koscielniak.

Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.