2017-04-21 07:00:00

Ninyi ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma ya Mungu!


Dominika ya pili ya Pasaka huitwa Dominika ya huruma ya Mungu iliyozinduliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000 wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Ufufuko wa Kristo ni utimilifu wa huruma ya Mungu kwa watu wake. Wimbo wa zaburi umetualika kumshangilia tukisema: “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele”. Kwa fumbo hili la Pasaka tunaushuhudia umilele wa upendo wa Mungu kwetu kwa kumtoa mwanae wa pekee kuwa fidia kwa dhambi zetu. Wakati wa kesha la Pasaka tuliitangaza Mbiu ya wokovu tukisema: “Lo, dhambi ya Adamu hakika ililazimika ikafutwa kwa kifo cha Kristo”.

Hakika upendo wa Mungu ni wa milele. Upendo wake hauna mwisho na haukatishwi tamaa na mioyo migumu iliyofungwa. Mungu hachoki kutupenda. Katika umilele huu ndipo tunapochota nguvu na matumaini katika nyakati za majaribu na katika udhaifu wetu kwa sababu tunapata hakika ya kwamba Mungu hatuachi kamwe. Katika muktadha huu tunaendelea kuionja furaha ya fumbo la Pasaka na kuishangilia siku hii kubwa katika historia ya mwanadamu.

Fumbo la Pasaka linatufunulia maana ya maisha yetu ya kikristo. Tunaitafakari hali ambayo tunaipokea baada ya kumiminiwa huruma ya Mungu mioyoni mwetu. Hali hiyo ni upya wa maisha. Tunazaliwa upya katika Kristo. Mtume Paulo anatuambia kwamba: “jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya”. Pasaka inauelezea ukristo wetu kama upya wa ubinadamu wetu na hivyo ni mwaliko wa kutembea katika mwaliko huo. Antifona ya mwanzo imetuelekeza katika upya huu ikitualika kwa kusema: “kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu”. Maziwa yasiyoghoshiwa ni maziwa halisi yasiyochanganywa na kitu chochote. Hiki ndicho chakula cha mtoto mchanga ambacho kwacho humpeleka katika ukamilifu na kukomaa kimwili. Hivyo kwetu sisi tunaalikwa kuipokea huruma ya Mungu mithili ya maziwa hayo kwa ajili ya ukomavu wetu kiroho. Huruma ya Mungu inatupeleka katika ukomavu wa kiutu.

Neno la Mungu katika Dominika hii ya leo linatufunulia upya huu wa maisha katika jumuiya ya kwanza ya wakristo. Tunu njema za maisha haya ambazo zinafunuliwa kwetu ni pamoja na umoja na matendo ya huruma. Jumuiya hii ya mwanzo inazipambanua tunu hizi kama nyenzo muhimu za maisha ya kipasaka, maisha ambayo yanatupeleka katika kuitambua nafsi yako binafsi katika nafsi za wengine. Ni mwaliko wa kujifunua na kutoa nje ili kumtambua, kumgusa na kumkiri Kristo mfufuka kama “Bwana na Mungu” hasa katika maisha ya wale wanaohitaji upendo na huruma yake. Huruma ya Mungu inapaswa kujifunua katika mshikamano na upendo baina ya ndugu. Sisi ambao tumefufuliwa pamoja naye tunaalikwa kudhihirisha upya wa maisha kwa mshikamano wetu na wenzetu katika matendo yetu ya upendo.

Jumuiya ya kwanza ilidumu katika umoja na upendo kwa sababu ya mambo kadhaa. Kwanza walidumu katika mafundisho ya mitume. Mafundisho hayo si mengine bali ni Injili ya Kristo ambayo Kristo aliwaagiza wafuasi wake kuieneza akisema: “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa”. Injili ni ufunuo wa utimilifu wa huruma ya Mungu katika Kristo. Ndani mwake tunachota maelekezo adhimu kupitia maafundisho, miujiza na uponyaji wake ambao unaidadavua vilivyo huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo iliyapokea mafundisho haya na kudumu kwake.

Mafundisho haya yalikuwa kwao kama maziwa yasiyoghoshiwa na hivyo ni chanzo cha ukomavu wako kiroho na kuimarika katika upya wa maisha. Sakramenti takatifu, hususani Sakramenti ya Ekaristi takatifu ambayo ni zawadi Kristo kwa wanadamu, zawadi ya udumifu nafsi yake kati yetu na uthibitisho wa upendo wake, ziliwaimarisha katika udumifu huo wa mafundisho ya mitume. Kwa njia ya sakramenti, wafuasi hawa wa kwanza walipokea neema ya Mungu ambayo ni msaada wake wa kimungu kwa ajili ya kudumu katika njia yake.

Katika utajiri huo wa umoja na mapendo ya kikristo ambao unaimarisha na Injili takatifu na masakramenti, Mtume Petro anawahimiza wakristo wa kwanza katika ustahimilivu katika majaribu. Hii ilikuwa ni tahadhari kwao kwa muendelezo wa vitisho na uadui wa shetani. Vita ya kiroho inaendelea kuwepo katika maisha ya mkristo. Lakini kutokana na hadhi tuliyoipokea, kutokana na silaha ambazo tumevikwa hatupaswi kukata tamaa bali kupambana na kusonga mbele kufikia ukamilifu. Mtume Petro anawafariji kwa kuwakumbusha thamani ya hadhi yao waliyoipokea akiwakumbusha kwamba kwa ufufuko wa Kristo “wamepata urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka na unaotunzwa mbinguni”. Pia akaongezea akiwaambia kwamba “mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho”.

Upya wa maisha ambao ni maisha ya kiinjili unabaki kuwa hai hata leo hii. Kitabu cha Injili kinabaki kuwa kitabu kilicho wazi na kinaendelea kuandikwa kupitia maisha yetu ya kila siku katika umoja wa kikristo na matendo yetu ya huruma. Katika hitimisho la Injili tumethibitishiwa hilo kwamba yapo mambo mengi ambayo Kristo ameyatenda lakini hayapo kimaandishi katika kitabu cha Injili. Hili ni dokezo la kufungua kitabu kingine cha maisha ya kikristo ambacho kinapaswa kuiendeleza habari hii njema. Huruma ya Mungu ambayo inapaswa kutupeleka katika ukamilifu wa wana huru wa Mungu inatualika kuendelea kuiandika Injili takatifu hata leo. Misaada miwili tuliyoidokeza hapo juu, yaani usikivu katika Neno la Mungu na kushiriki Sakramenti bado inabakia kuwa ni kichocheo na nguvu ya kuendelea kuiandika Injili hiyo.

Mazingira ya jamii ya mwanadamu leo hii yanaweza kutuweka katika hali ya mashaka na hofu na hivyo kukosa ujasiri wa kuiandika Injili hiyo ya Mungu. Tutaendelea kubaki katika hali hiyo bila kutenda jambo mithili ya mitume ambao walikuwa wamejifungia “kwa hofu ya Wayahudi”. Katika hali hii hatuwezi kamwe kuwa Injili kwa wengine na kuwatangazia huruma ya Mungu. Katika upendo wake mkubwa Kristo ameingia katika milango ya nyumba zetu ambayo ilikuwa imefubaishwa na dhambi na nguvu za kuzimu na kuzifungua pingu za mioyo yetu iliyofungwa na kututoa nje tukiwa huru. Hii inamaanisha kwamba tunapaswa kutoka nje na kuishuhudia nguvu ya upendo ya uponyaji ambayo imeziteka nafsi zetu.

Tunashuhudia mbele yetu ubinadamu uliojeruhiwa na wenye hofu kuu, ubinadamu wenye makovu ya majeraha mbalimbali na unaokosa uhakika na mwanga wa maisha; katika hali hii tunamsikia Kristo akituambia: “kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi”. Anatupatia utume wa kwenda kuwa vyombo vya kuieneza huruma yake kwa kuistawisha amani ya kweli inayopatika katika Kristo mfufuka. Tunapoyaponya majeraha yao na kuwarudishia tena amani ya Kristo tunamkiri Kristo na kuifanya Injili yake iendelee kuandika hata leo; tunawafanya hawa ndugu zetu kuweza kuguswa kwa mikono yako huruma ya Mungu na kumkiri Kristo kama “Bwana na Mungu” mithili ya Mtume Toma. Fumbo la Pasaka limetufunulia ukuu na umilele wa huruma yake. Tuichuchumile nafasi hii ya neema na kudumu katika upya wa maisha ya kikristo. Utakatifu wetu ung’arishwa kwa matendo yetu ya umoja na upendo wa kikristo kwani katika hayo Mungu anatukuzwa na mwanadamu anatakatifuzwa.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.