Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Kardinali Stella, toeni harufu nzuri ya utakatifu wa maisha kila siku!

Mapadre onesheni na kushuhudia utakatifu wa maisha kwa njia ya huduma makini, maisha ya sala, na maadhimisho ya mambo matakatifu.

21/04/2017 13:16

Wakleri wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajikita zaidi na zaidi katika mchakato wa kumtafuta na kumwambata Kristo Yesu katika maisha yao ya kila siku kwa njia ya: sala, tafakari ya Neno la Mungu na maadhimisho ya mafumbo matakatifu ya Kanisa. Wakristo wanapaswa kujihoji nafsini mwao kuhusu: uaminifu katika maisha na wito wao; ujasiri wa kusimama kidete kutangaza na kushuhudia kweli za Injili sanjari na kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa mataifa.

Kwa kuzingatia mambo haya makuu katika maisha ya wafuasi wa Kristo, Habari Njema ya Wokovu inaweza kusonga mbele kama alivyojitahidi kutangaza na kushuhudia Mtakatifu Benedikto Abate, Msimami wa Bara la Ulaya. Haya yamesemwa hivi karibuni na Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya wakleri, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Mtakatifu Benedikto Abate kwenye Monasteri ya Montecassiono, nchini Italia. Anasema, huu ndio muhtasari wa maisha ya Mtakatifu Benedikto ya kumtafuta Mungu wake, yaani “Quaerere Deum” kama yanavyojulikana kwa lugha ya Kilatini, Mungu ambaye ni kiini na chemchemi ya furaha na matumaini yake katika maisha.

Wakati wa shida na mahangaiko makubwa Barani Ulaya, Mtakatifu Benedikto, Abate alipenda kuwafariji watu wake kwa kuwatakia amani na utulivu wa ndani; kwa kuhakikisha kwamba, Mwenyezi Mungu anapewa kipaumbele cha kwanza katika maisha yao. Hii ni hija inayopani kumwilisha Heri za Mlimani, mafundisho makuu ya Yesu katika uhalisia wa maisha ya watu; ili kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kujadiliana mustakabali wa maisha yao. Kwa njia hii, maisha anasema Kardinali Stella yanakuwa ni mchakato wa huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuwatambua: maskini waroho, watu wenye huzuni, wapole; wenye njaa na kiu ya haki; wenye rehema na moyo safi; wapatanishi na wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki. Hili ni kundi la wale ambao si mali kitu mbele ya macho ya walimwengu anasema Kardinali Stella, lakini hawa ndio wale wanaoitwa na Yesu kuwa ni wenyeheri; kielelezo makini cha upendo na urafiki wa Mungu unaowaokoa na majanga ya maisha ya binadamu; tayari kuwashirikisha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Heri za Mlimani ni kiini na muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu yanayotoa kipaumbele cha pekee kwa mambo msingi katika maisha kwa kutambua kwamba, wanapendwa na Kristo Yesu. 

Kardinali Beniamino Stella anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, hiki ndicho kielelezo cha utakatifu wa maisha yanaopaswa kumwilishwa na kushuhudiwa katika uhalisia wa maisha ya Wakristo, lakini kwa namna ya pekee katika: maisha, wito na utume wa Wakleri. Maisha ya utakatifu yanaboreshwa kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu; huduma ya upendo bila ya kujibakiza sanjari na uwajibikaji makini katika majukumu ya maisha ndani na nje ya familia, kama kielelezo cha matumaini kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

21/04/2017 13:16