Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Hija ya kitume ya Papa Francisko Misri inalenga kupandikiza amani!

Papa Francisko anatembelea nchini Misri kama mjumbe wa amani na majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! - REUTERS

21/04/2017 11:53

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri kuanzia tarehe 28-29 Aprili 2017 inaongozwa na kauli mbiu “Papa wa amani nchini Misri”. Hii ni hija ya kitume inayopania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa familia ya Mungu nchini Misri, ili kujikita katika misingi ya haki, amani, maridhiano na uhuru wa kuabudu. Tofauti msingi zinazojitokeza miongoni mwa familia ya Mungu nchini Misri ni utajiri unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kujipambanua kuwa ni kiongoni anayesimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Ni kiongozi anayekazia ulinzi na usalama; haki na amani kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Haya ni mambo mazito ambayo kimsingi yanapaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Hii ni sehemu ya mahojiano yaliyotolewa kwa Shirika la Habari la Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, SIR na Balozi Abdel Rahman Moussa pamoja na Ahmad Al-Tayyib, Imam mkuu wa Msikiti mkuu wa Al-Azhar, ulioko Cairo, nchini Misri, wakati huu wa maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri. Akiwa nchini humo, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Misri, Papa Tawadros II, Patriaki wa Kanisa la Kikoptik nchini Misri pamoja na wajumbe watakaokuwa wanashiriki katika mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa.

Papa Tawadros II anamwona Baba Mtakatifu Francisko kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa amani na ukweli; Baba na mtetezi wa maskini na wanyonge sehemu mbali mbali za dunia! Ni kiongozi anayethamini utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya vyanzo vikuu vya majanga na maafa makubwa yanayowaandama watu sehemu mbali mbali za dunia kwa wakati huu. Ni kiongozi anayeendelea kujipambanua kwa kutaka kutangaza na kushuhudia Injili ya amani, upendo na mshikamano wa kidugu sehemu mbali mbali za dunia. Kutokana na mchango wa Baba Mtakatifu Francisko katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ndiyo maana familia ya Mungu nchini Misri inajiandaa kwa furaha kubwa kumpokea na kumkarimia Papa Francisko atakapowatembelea nchini Misri.

Papa Tawadros II anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi ambaye anatoa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kiekumene miongoni mwa wafuasi wa Kristo ili kujenga na kudumisha uekumene wa: sala na maisha ya kiroho; uekumene wa damu na huduma makini hasa kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili nao pia waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Kila mwaka ifikapo tarehe 10 Mei, Kanisa la Kikoptik linasali kwa ajili ya kuombea umoja, upendo na mshikamano wa kidugu kati ya Wakristo, kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya mkutano wa sala kati ya Patriaki Shenouda III alipokutana na Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1973 mjini Vatican.

Ushirikiano huu unaendelezwa kwa kiasi kikubwa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye katika ujumbe wake wa Pasaka ya mwaka 2017 kwa Papa Tawadros II anakaza kusema: giza, dhambi na udhaifu wa binadamu vinaweza kuwa ni mwanzo mzuri katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene; ili kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano kati ya Makanisa, ili kwa pamoja Wakristo waweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika huduma makini kwa binadamu sehemu mbali mbali za dunia.

Taarifa zinaonesha kwamba, katika mkutano wa majadiliano ya kidini utakaofanyika kwenye Chuo kikuu cha Al-Azhar, Cairo nchini Misri, zaidi ya wajumbe mia mbili wamealikwa ili kushiriki na kusikiliza changamoto zitakazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko mintarafu majadiliano ya kidini, uhuru wa kuabudu na haki msingi za binadamu. Viongozi wa kidini wanapaswa kushirikiana na kushikamana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anaangaliwa kama mjumbe wa amani anayekwenda kupandikiza mbegu ya amani, matumaini na mshikamano hasa baada ya mashambulizi ya kigaidi kufanyika hivi karibuni nchini Misri na kusababisha maafa makubwa kwa  Wakristo. Viongozi wa dini ya Kiislam wanakaza kusema, ugaidi hauna dini kwani ni chimbuko la hofu na utamaduni wa kifo, dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baada ya mkutano wa majadiliano ya kidini, wajumbe watatoa tamko la pamoja, ili kusimama kidete kupinga vitendo vyote vya kigaidi.  Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli amealikwa pia kushiriki katika mkutano huu wa majadiliano ya kidini yanayofumbatwa pia katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

21/04/2017 11:53