2017-04-20 11:00:00

Matunda ya Maadhimisho ya Mwaka wa huruma, Jimbo kuu la Mwanza!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yalizinduliwa rasmi kwa Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya asili na mlango wa huruma ya Mungu, tarehe 8 Desemba 2015. Maadhimisho haya yakafungwa rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu na Papa Francisko wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu hapo tarehe 20 Novemba 2016 kwa kumwomba Kristo Yesu, Uso wa huruma ya Baba wa milele awamiminie waja wake neema na baraka kama umande wa asubuhi, ili kila mtu aweze kushirikiana na wengine katika mchakato wa maboresho ya mustakabali wa maisha ya binadamu hapa duniani. Baba Mtakatifu anatamani kwamba, harufu nzuri ya huruma ya Mungu iwafikie watu wote kama ishara ya endelevu ya uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya binadamu!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa na neema ya pekee kabisa kumtafakari Kristo Yesu uso wa huruma ya Baba wa milele; kulitafakari na kulimwilisha Fumbo la huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya binadamu kwa kutumia dawa ya huruma ya Mungu kuliko ukali; kwa kuonesha na kushuhudia kwamba, Kanisa ni Mama mpendelevu, mvumilivu na anayewaka moto wa upendo kwa watoto wake wote!

Askofu mkuu Ruwaichi anapenda kwa niaba ya waamini wote, lakini zaidi kwa niaba ya familia ya Mungu kutoka Jimbo kuu la Mwanza kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuzindua na kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa Jimbo kuu la Mwanza imekuwa ni fursa na mwaliko wa kujitazama na kujikusanya; muda wa toba na wongofu wa ndani tayari kuanza safari ya kumrudia Mwenyezi Mungu kwa kujizatiti katika mambo msingi ya maisha ya kiroho na kiimani kama viumbe wa Mungu na watu waliokombolewa na kutakaswa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti!

Mwaka wa huruma ya Mungu kwa Jimbo kuu la Mwanza imekuwa ni fursa ya toba na wongofu wa ndani; sala na tafakari ya Neno la Mungu pamoja na kumwilisha katika uhalisia wa maisha matendo ya huruma kiroho na kimwili. Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, huruma ni msingi thabiti wa uhai, maisha na utume wa Kanisa ndiyo maana Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni nafasi ya kuhamasisha waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kiroho na kimwili!

Anasema, matendo ya huruma kiroho ambayo kimsingi ni ushauri kwa wenye shaka, kuwafundisha wajinga, kuwaonya wakosefu; kuwafariji wenye huzuni; kusamehe makosa; kuvumilia wasumbufu pamoja na kuwaombea walio hai na wafu ni fursa ya kuwa karibu na wale wanaojisikia kuwa mbali na Kanisa au kusukumizwa pembezoni mwa maisha na utume wa Kanisa! Watu wengi wameonja kutoka kwa waamini wa Jimbo kuu la Mwanza ladha ya huruma ya Mungu katika maisha yao. Waamini wengi wamejitahidi kufanya toba ili kurekebisha maisha yao ya Kikristo; wamerekebisha ndoa kwa kuachana na “uchumba sugu” ili kuambata tena maisha ya Kisakramenti na neema. Wamejipanga vyema zaidi ili kuishi imani yao kwa bidii kwa kuonesha ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Ni matumaini ya Kanisa kwamba, waamini wataendelea kutunza ndani mwao neema na matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwani hili ni zoezi endelevu na ni sehemu ya vinasaba vya maisha kiroho.

Waamini wa Jimbo kuu la Mwanza wamepata nafasi ya kufanya hija ndani na nje ya Jimbo kuu la Mwanza kwa kutambua kwamba maisha yenyewe ni hija na kwamba binadamu ni msafiri hapa duniani, kuelekea kwenye maisha ya uzima wa milele, mbinguni kwa Baba mwenye huruma! Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Mwanza anakaza kusema, kutokana na mang’amuzi ya kichungaji aliyoyapata wakazi za ziara zake za kichungaji kwenye Parokia za Jimbo kuu la Mwanza, kwa kuheshimu na kuzingatia uamuzi wa Baba Mtakatifu Francisko wa kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, aliona umuhimu wa kuwapatia tena waamini wa Jimbo kuu la Mwanza nafasi ya kuendelea kufaidi matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili waamini wengi zaidi waweze kuambata na kukumbatia huruma ya Mungu katika maisha yao.

Jimbo kuu la Mwanza linafunga rasmi maadhimisho ya Mwaka wa huruma ya Mungu katika maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu, yaani tarehe 23 Aprili 2017. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi anakumbusha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika maisha yao; kwa kuiadhimisha, kuiambata, kuishuhudia na kuimwilisha, kwani huruma ya Mungu inagusa maisha yote ya mwamini kwani hii ni safari ya imani, ufuasi na ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.