Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Bunge Afrika ya Kusini kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Zuma

Rushwa, ufisadi, ukosefu wa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya na utawala mbaya ni kati ya mambo ambayo yamewachefua sana wananchi wa Afrika ya Kusini kiasi cha kuonesha kutokuwa na imani tena na Rais Zuma. - AFP

20/04/2017 07:38

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linasikitika kusema kwamba, hali ya kisiasa nchini humo inaendelea kuwa tete kila kukicha tangu Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini alipomwachisha kazi Bwana Pravin Gordhan, aliyekuwa Waziri wa Fedha nchini Afrika ya Kusini. Wananchi wengi walimkubali kutokana na: uadilifu, weledi na msimamo wake wa kutetea mafao ya wengi sanjari na kusimama kidete dhidi ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma, shutuma ambazo zinamwandama Rais Jacob Zuma kwa kipindi kirefu sasa!

Kashfa ya rushwa ilipelekea Rais Zuma kuwafukuza kazi baadhi ya Mawaziri walioonekana kuwa kinyume chake! Hali ya kisiasa imeingia hatua nyingine tena kwa Bunge la Afrika ya Kusini kutaka kupiga kura ya kuonesha kutokuwa na imani tena na Rais Jacob Zuma. Kura hii kwa mara ya kwanza ilikuwa inatarajiwa kupigwa hapo tarehe 12 Aprili 2017 lakini ikahailishwa baada ya Vyama vya upinzani kuitaka Mahakama kuu ya Katiba kuamuru kwamba, kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma ipigwe kwa siri.

Chama Cha ANC kinapinga shinikizo la kutaka Rais Zuma ang’atuke kutoka madarakani kwa ajili ya mafao ya umma! Kutokana na sakata hili kuhatarisha amani, umoja na mafungamano ya kijamii nchini Afrika ya Kusini, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linawataka wabunge kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu kwa kuongozwa na dhamiri nyofu wanapopiga kura ya kuonesha kuwa na imani au kumkataa Rais Zuma kuendelea kushika madaraka nchini humo! Huu ni wajibu nyeti na tete katika maisha na historia ya wananchi wa Afrika ya Kusini.

Baraza la Maaskofu linawataka wabunge kuonesha ukomavu wa kisiasa, uongozi bora na utawala wa sheria badala ya kugubikwa na ushabiki wa kisiasa ambao umepelekea kuchechemea kwa utawala bora na matokeo yake ni kuibuka kwa kashfa za rushwa na ufisadi ambao kwa sasa umekuwa ni kero kubwa kwa Afrika ya Kusini. Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linakitaka Chama tawala cha A.N.C. kusikiliza kilio cha mamilioni ya wananchi wa Afrika ya Kusini ambao wamekuwa wakiandamana kila kukicha wakitaka haki itendeke dhidi ya wala rushwa na mafisadi nchini humo.

Wachungizi wa mambo wanasema, moto unafukuta ndani ya Chama tawala kusaka mtu atakaye kuwa mrithi wa Rais Jacob Zuma anayetarajiwa kumaliza muda wake rasmi kikatiba hapo mwaka 2019, ikiwa kama mambo yatakwenda kama yalivyopangwa Kikatiba! DR. Nkosazana Dlamini-Zuma, anayemaliza muda wake kama Kamishina wa Umoja wa Afrika ni kati ya “vigogo” wa A.N.C. wanaotarajiwa kumrithi Rais Jacob Zuma wakati utakapowadia! Lakini vyama vya upinzani navyo vinaendelea kuwasha moto wa vuguvugu la mageuzi ya kisiasa nchini Afrika ya Kusini! Kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma inaweza kutoa mwelekeo wa kisiasa nchini Afrika ya Kusini kwa siku za usoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

20/04/2017 07:38