Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Kristo Mfufuka ni mwanzo wa amani na furaha kwa mwanadamu!

Pasaka ni ushindi dhidi ya dhambi na ni mwanzo mpya wa amani na furaha ya binadamu. - REUTERS

17/04/2017 14:20

Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka ya Bwana ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na ni mwanzo wa mchakato mzima wa amani na furaha kwa wanadamu. Pasaka ni kilele cha maadhimisho ya safari ya siku arobaini jangwani ambayo kwa mwaka huu, Kanisa Katoliki nchini Tanzania limetafakari kuhusu furaha ya Injili na Uumbaji; madhara ya dhambi na neema ya ukombozi ambayo imeletwa kwa njia ya Kristo Yesu! Kumbe, Siku kuu ya Pasaka ni kilele cha ukombozi wa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti!

Ufufuko wa Kristo ni kielelezo makini cha ushindi dhidi ya uwongo, uonevu na ukatili. Ufufuko wa Kristo unajenga na kuimarisha daraja kati ya mbingu na dunia na kumrejeshea tena mwanadamu ile furaha ya asili kwa kumtaka kusimama kidete kulinda na kuheshimu kazi ya uumbaji, kwani kwa njia ya Ufufuko binadamu amerejeshewa tena hadhi na utu wake! Hivi ndivyo anavyoandika Askofu Augustine Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar katika ujumbe wake wa Pasaka kwa mwaka 2017. Anasema, Ufufuko wa Kristo ni nguvu ya wanyonge, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto ni kuona na kutenda katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Familia ya Mungu nchini Tanzania, haina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kujenga misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuhakikisha kwamba, viongozi na watanzania katika ujumla wao wanatumia vyema: elimu, uwezo, weledi na karama zao katika kukabiliana na: matatizo, kero na changamoto zinazowakabili watanzania kama lilivyo baa la njaa kwa wakati huu. Viongozi wawajibike na kutenda katika ukweli, haki, uadilifu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Ufufuko wa Kristo ni ujumbe wa furaha unaofukuza giza la: wizi, ubadhirifu na ufisadi wa mali ya umma; saratani ya rushwa, biashara, matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya ambalo ni janga linalowanyemelea vijana wengi nchini Tanzania. Nia njema ya Serikali ya awamu ya tano izingatiwe kwa kujikita katika utawala bora unaozingatia sheria na haki msingi za binadamu; ili juhudi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya tano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi iweze kupata chapa endelevu. Ufufuko wa Kristo Yesu, uwasukume viongozi wa ngazi mbali mbali kuwajibika kikamilifu kwa kutetea utu na heshima ya binadamu; haki msingi badala ya kutafuta umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko kama alivyofanya Pilato kwa kupindisha ukweli!

Askofu Augustine Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar anawataka watanzania kujenga na kuimarisha utamaduni wa kupokea na kukubali mabadiliko yanayofumbatwa katika kujinyima na kujikatalia, ili kushiriki katika ujenzi wa haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Watanzania wana matumaini makubwa na Serikali ya awamu ya tano! Haiwezekani serikali ikaongozwa na mtu mmoja tu! Kumbe, hapa viongozi wote wanapaswa kushirikiana na kushikamana na raia wao; kwa kutenda kadiri ya sheria, taratibu na kanuni za nchi pasi na woga usiokuwa na mvuto wala mashiko. Falsafa ya kutaka kumfurahisha mtu ni hatari kwa haki msingi za binadamu! Vyombo vya ulinzi na usalama, sheria na haki msingi za binadamu vitekeleze dhamana yao kwa haki na weledi ili kuwajengea watanzania dhana ya utawala bora unaozingatia sheria, haki na utu wa binadamu. Mikopo kwa wanafunzi wote wa Tanzania itolewe pasi na ubaguzi, kwani hili ni deni ambalo lazima lilipwe kwa wakati wake! Mkopo si msaada ni haki ya mlipa kodi na masharti yake lazima yazingatiwe!

Askofu Augustine Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar anasema, kuna haja kwa serikali kujizatiti kikamilifu katika sera, mipango na mikakati ya uchumi ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na fursa nyingi zaidi za ajira; maboresho katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi, ili kuwalatea watanzania furaha na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hii ni changamoto inayopaswa kushughulikiwa na familia ya Mungu nchini Tanzania, ili kweli amani na furaha viweze kudumu na kuwaambata watanzania wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

17/04/2017 14:20