Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Kristo Mfufuka ni chemchemi ya furaha na matumaini ya kweli!

Kristo Mfufuka ni chemchemi ya furaha, imani na mapendo thabiti. - AP

17/04/2017 13:47

Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufuka kwa wafu ndiye aliyeshinda dhambi na mauti na kuwakirimia binadamu matumaini, ari na nguvu ya kuweza kukabiliana na Misalaba ya maisha yao ya kila siku! Lakini, ikumbukwe kwamba, Ufufuko wa Kristo ni chemchemi ya imani, furaha, upendo wa dhati na matumaini mapya katika maisha ya binadamu kwani Kristo mfufuka ni sababu ya furaha na matumaini ambayo kamwe hayawezi kufifia.

Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza  wa Kanisa la Costantinopol katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa Mwaka 2017 ambayo imeadhimishwa na Wakristo wote kwa pamoja, kielelezo cha Uekumene wa sala na maisha ya kiroho! Anasema, taarifa za vyombo vya habari na mawasiliano ya kijamii vinaendelea kuonesha jinsi ambazo watu wanakabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha. Kuna mauaji ya kutisha yanyofanywa na vikundi vya kigaidi, vita, dhuluma na nyanyaso!

Kuna athari za mabadiliko ya tabianchi; misimamo mikali ya kidini, baa la njaa, umaskini na maradhi; mambo yanayoendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa wanaonekana kuwa kama kero kwa Jumuiya ya Kimataifa na kusahau kwamba, hawa ni watu wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kuna wasi wasi mkubwa wa ukosefu wa ulinzi na usalama; amani na maridhiano kati ya watu! Kuna vitisho vya kufumuka kwa vita kama njia ya kupimana nguvu za kijeshi! Hii ni misalaba ya maisha ya kila siku ambayo inaendelea kumwandama mwanadamu na wakati mwingine watu wanaibeba kwa kulalama sana!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, licha ya magumu, changamoto na matatizo yote haya yanayoendelea kumwandama mwanadamu, lakini Kanisa bado linathubutu kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyeshinda dhambi na mauti! Furaha ya Wakristo inafumbatwa katika ushindi wa Kristo Mfufuka ambaye ni: mwanga, ukweli, njia,uzima, amani na furaha ya watu wake. Mama Kanisa anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutambua umuhimu wa uwepo endelevu wa Kristo anayeendelea kuandamana nao katika hija ya maisha yao, ili kuwashirikisha ukuu, furaha na matumaini katika safari ya maisha, mwaliko ni kumsikiliza Kristo Yesu na kumpatia nafasi ya kuambatana na waja wake.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaendelea kufafanua kwamba, Wakristo huko Mashariki ya Kati wanakabiliana na hali ngumu ya maisha. Ni watu wanaoteseka, kunyanyasika na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hali hii pia inajionesha Barani Ulaya, Afrika, Asia na Amerika. Kristo Yesu alikwisha wahakikishia wafuasi wake uwepo wake endelevu hadi utimilifu wa nyakati, atakapokuja kuwahukumu wazina na wafu! Hii ndiyo chemchemi ya matumaini ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

17/04/2017 13:47