2017-04-16 16:06:00

Kristo Mfufuka ni Jibu la fumbo la mahangaiko ya binadamu wote!


Mama Kanisa anaimba na kutangaza kwa shangwe kuu kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa amefufuka kutoka kwa wafu na uthibitisho wake ni kaburi wazi, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia kwamba, kweli Kristo Yesu, amefufuka, ili kuwaondolea watu hofu na simanzi ya maisha. Kwa watu waliokata tamaa na kuelemewa na hofu watambue kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini mapya. Hata kama Yesu amefufuka kutoka kwa wafu bado watu wanaendelea kujiuliza maswali msingi, mbona kuna magonjwa, majanga asilia, vita, biashara haramu ya binadamu, biashara ya silaha za mahangamizi, nyanyaso na ukosefu wa haki! Yesu Mfufuka yuko wapi!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kuadhimisha Pasaka ya Bwana, Jumapili tarehe 16 Aprili 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika shida na mahangaiko ya binadamu, waamini wawe na ujasiri anasema Baba Mtakatifu Francisko wa kumwangalia Yesu aliyewambwa Msalabani, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu aliyekuwa anaogelea katika lindi la dhambi na mauti. Msalaba, yaani mateso na mahangaiko ya watu bado yanaendelea kusonga mbele, lakini imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake inaendelea kufifia, lakini Kanisa linatangaza kwa ari na moyo mkuu kwamba, Kristo Yesu amefufuka kwa wafu!

Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa. Kristo Mfufuka ni chemchemi na mwanga wa matumaini kwa watu wanaodharauliwa na kunyanyasika katika ulimwengu mamboleo! Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni chemchemi ya maisha mapya na mwelekeo mpya usiozibwa na kuta za utengano. Katika shida na mahangaiko ya watu anasema Baba Mtakatifu, Kanisa linataka kuwaambia walimwengu kwamba, Kristo Yesu amefufuka kwa wafu! Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni jibu muafaka kwa mateso na mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia! Watu wanaoteseka kutokana na vita, maafa na majanga asilia. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kurejea majumbani mwao wakiwa wanarudia kusema, Yesu Kristo amefufuka kweli kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.