2017-04-16 15:50:00

Italia yampongeza Papa Francisko kwa kuwatetea wanyonge!


Rais Sergio Mattarella wa Italia katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka, amemtumia salam na matashi mema, Baba Mtakatifu Francisko, pamoja na kumpongeza kwa kuendelea kuwa kweli ni “Jembe la nguvu” katika kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee wakati wa Kipindi cha Pasaka. Rais Mattarella anaendelea kukaza akisema, mafundisho pamoja na mikakati ya shughuli za kichungaji za Baba Mtakatifu Francisko zinaendelea kuwa kweli ni chemchemi ya kutafuta suluhu makini kwa changamoto na magumu yanayoendelea kuiandama Jumuiya ya Kimataifa kwa nyakti hizi

Rais Sergio Mattarella kwa namna ya pekee anakumbushi hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkesha wa kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 60 ya Mkataba wa Roma uliotiwa mkwaju kunako mwaka 1957, kwa kuitaka Jumuiya ya Ulaya kujikita katika mchakato wa kuwajengea watu matumaini mapya yatakayoshirikisha wananchi wengi wa Jumuiya ya Ulaya. Anampongeza Baba Mtakatifu kwa hija zake za kitume alizozifanya hasa kwa kutembelea maeneo mbali mbali ya Italia: Jimbo kuu la Milano, Jimbo Katoliki la Carpi na Milandola; ambako watu wanateseka kutoka na maafa asilia. Mwishoni, ni matumaini ya Rais Sergio Mattarella kwamba, wataweza kukutana tena na Baba Mtakatifu Francisko mapema iwezekanvyo kwenye Ikulu ya Italia. Mwishoni, anapenda kumwonesha urafiki pamoja na kuthamini sana utume wake wa kichungaji kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.