2017-04-16 10:00:00

Dumisheni ufukara unaojikita katika mshikamano wa udugu na upendo!


Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu pamoja na “Madhabahu ya Kuvulia Nguo” yanayolikumbuka kwa namna ya pekee tukio la Mtakatifu Francisko wa Assisi kujivua mambo ya kidunia, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza katika huduma kwa Mungu na jirani yana umuhimu wa pekee sana kwa maisha na utume wa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Asisi-Nocera Umbra-Guado Tadiono. Ufunguzi wa “Madhabahu ya Kuvulia Nguo” hapo tarehe 20 Mei 2017 ni neema nyingine inayotolewa kwa mahujaji na familia ya Mungu katika ujumla wake jimboni humo!

Haya Madhabahu yalitembelewa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Oktoba 2013 miezi michache tu baada ya kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Alionesha furaha isiyokuwa na kifani alipotembelea eneo hili kwa kutambua kwamba, alikuwa amemteua Mtakatifu Francisko wa Assisi kuwa ni msimamizi katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukazia umuhimu wa amani, mazingira na ufukara. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini madhabahu haya amemwandikia ujumbe Askofu Domenico Sorrentino wa Jimbo Katoliki la Asisi-Nocera Umbra-Guado Tadiono, Italia kumshukuru kwa kumshirikisha katika uzinduzi huu.

Madhabahu haya yana umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Mtakatifu Francisko wa Assisi ambaye katika ujana wake alijimanua kutoka katika malimwengu, anasa na utajiri mkubwa aliokuwa nao baba yake Pietro di Bernandone. Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyekuwa amemwongokea Mungu si kwamba, alitaka kukosa adabu na heshima mbele ya baba yake mzazi, bali alitaka kuonesha upendo kwa Kristo Yesu kwa kuondokana na mambo yasiyo ya lazima, hali inayojionesha katika “Ukumbi wa Kuvulia Nguo”. Akiwa tupu na huru, kijana Francisko akajiaminisha mikononi mwa Askofu Guido aliyemfunika kwa joho lake la kiaskofu, linaonesha upendo wa Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika ukumbi huo pia kuna ushuhuda wa umaskini wa hali ya juu unaofumbatwa katika maisha ya watu ambao pengine wanakosa hata mahitaji msingi katika maisha, lakini upande mwingine wa shilingi kuna kundi dogo la watu wanaofaidi utajiri na rasilimali ya dunia. Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa uchumi unaoendelea kutekeleza maisha ya watu; wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania! Kijana Francisko aliacha ushuhuda wenye mvuto kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa wa Ukoma, kwa kuwaonesha huruma katika maisha yao: kiroho na kimwili.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, ufunguzi wa madhabahu haya mapya utakuwa ni ushuhuda wa kinabii kwa Kanisa, kwa kujimanua kutoka katika malimwengu, kwa kuambata ufukara, kwa kujifunza kukaa pamoja na kuwahudumia maskini kama njia ya kugusa na kuhudumia Fumbo la Mwili wa Kristo! Mkristo anapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa matendo yake kwa maskini kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji na sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa upendo na udugu sanjari na kuzingatia mambo msingi tu ya maisha.

Changamoto hii ilivaliwa njuga na Mtakatifu Francisko aliyepewa dhamana ya kulijenga Kanisa la Kristo, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Kristo Yesu ni kielelezo makini cha utupu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho, ushuhuda wa unyenyekevu na utii wa hali ya juu kabisa kiasi hata cha kufa Msalabani. Fumbo la Umwilisho anasema Baba Mtakatifu Francisko linapata utilimifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Huu ni mwaliko kwa waamini kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote sanjari na kumwilisha upendo kwa jirani. Waamini wawe na ujasiri wa kuuvua ubinafsi wao, ili kuambata uzuri tayari kushuhudia furaha ya Injili inayofumbatwa katika mshikamano wa kidugu.

Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee, toba na wongofu wa ndani; sanjari na kujenga utamaduni wa kuwathamini, kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana katika maisha yao, ili kukabiliana na changamoto mamboleo na hatimaye kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi magumu katika maisha. Mama Kanisa anapenda kuimarisha utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ndiyo maana, Kanisa linajiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Madhabahu haya iwe ni fursa ya kukutana na kuwasaidia vijana kuhusu maamuzi ya miito yao; kwa kuonesha umoja katika nia na mawazo, ili kujenga familia zitakazowajibika kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya katika hija ya maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.