2017-04-15 08:32:00

Papa Francisko: Njia ya Msalaba katika uhalisia wa maisha ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa kuu usiku, tarehe 14 Aprili 2017 ameongoza Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo. Itakumbukwa kwamba, tafakari ya mwaka huu imeandaliwa na Professa Anne-Marie Pelletier, mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu ambaye ametafakari zaidi kuhusu mchango wa wanawake wa Injili sanjari na mateso ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu katika Ibada hii amesaidiwa kuubeba Msalaba na Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma pamoja na wawakilishi mbali mbali.

Bara la Afrika lilipewa Msalaba kituo cha Saba, Yesu anapokutana na wanawake wa Yerusalemu wanaomlilia. Hapa Msalaba ulibebwa na Sr Maria Teresa Mbeva na Sr. Maria Agatha Ogbugo kutoka katika Shirika la Wabenediktini. Walisaidiwa pia na Mama Sylviane Emmanuella Nikiema kutoka Burkina Faso pamoja na Bwana Thèodro Muanza Muanza kutoka DRC. Kituo cha Nane kadiri ya mpangilio wa Mwaka 2017, Yesu anavuliwa nguo! Waliobeba Msalaba katika kituo hiki ni familia ya Bwana Hany Mourad Yassa Mosaad na Dina Atef Khalifa Sawers pamoja na watoto wao Angelina, Maria na Helena. Hii ni familia kutoka Misri. Kimsingi, Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo imewagusa na kuwaambata watu wote katika shida na mahangaiko yao mbali mbali!

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuhitimisha Njia ya Msalaba, alitoa tafakari fupi iliyogusa undani wa Fumbo la Msalaba; ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu aliyeuzwa kwa vipande thelathini vya fedha; akahukumiwa na kuteswa kama jambazi wa kutupwa;  akacharazwa mijeledi, akavikwa taji la miiba kichwani, akadhihakiwa na kutemewa mate hatimaye, akawambwa Msalabani. Ni Kristo mtu wa mateso, aliyetobolewa ubavuni mwake kwa mkuki, aliyekufa na kuzikwa, yeye ambaye ni Mungu asili ya uhai.

Mateso ya Kristo Msalabani anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kielelezo cha kashfa ya mateso yanayoendelea kushuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia, maafa asilia, vita, wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kufa maji na kuzikwa kwenye Bahari ya Mediterrania; mambo ambayo kwa sasa yanaonekana kuwa si habari tena inayosikitisha wala kuwachoma watu mioyo yao! Ni aibu ya damu ya watu wasiokuwa na hatia inayoendelea kumwagika kila kukicha kutokana na vita, dhuluma na nyanyaso za kila aina, lakini zaidi kutokana na ukabila, hali yao ya kijamii na mbaya zaidi imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anaendelea kulalama kwamba, hii ni aibu ya usaliti unaoendelea kufanywa na wafuasi wa Kristo kama ilivyokuwa kwa Yuda Iskariote na Mtakatifu Petro. Waamini wanaendelea kumsaliti na “kumpiga mnada” kutokana na dhambi na kwa kutotimiza vyema dhamana na nyajibu zao katika maisha; ukimya wao kutokana na ukosefu wa haki msingi; kwa kuwa na “mkono wa birika” kiasi cha kushindwa kuonesha ukarimu; kwa kupaza sauti kali kwa ajili ya kulinda na kudumisha masilahi binafsi badala ya kuangalia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Ni aibu ya uwongo na masengenyo kwa jirani; miguu iliyo miepesi kukimbilia katika nafasi za dhambi lakini viwete kwa kutenda mema! Hii ni aibu ya wakleri na watawa ambao wamekuwa ni sababu ya kashfa kwa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kiasi hata cha kusahau: ari na mwamko pamoja na ule upendo wao wa kwanza kwa Kristo Yesu na hivyo kushindwa kugusa undani wa mioyo na maisha yao ya wakfu. Licha ya aibu yote hii, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema, bado mioyo ya waamini ina kiu ya imani na matumaini na kwamba, atawatendea waja wake kadiri ya huruma na upendo wake na wala si kama wanavyostahili kutendewa kutokana ubaya na ugumu wa mioyo yao!

Waamini bado wana matumaini thabiti waliyorithishwa na wazazi wao; matumaini ambayo yanageuzwa na Msalaba wa Kristo, kuwa na uwezo wa kuota tena; kusamehe na kupenda kwa dhati! Anamwomba Kristo Yesu aweze kugeuza giza la mioyo yao kuwa mwanga angavu wa Ufufuko wake! Kuendelea kuwa na matumaini yanayobubujika kutoka katika uaminifu wa Kristo Yesu, huku wakizungukwa na Msalaba kama chachu, ladha na mwanga unaotoa dira kwa ubinadamu uliojeruhiwa. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, litaendelea kuwa ni sauti ya mtu aliaye katika nyika na jangwa tupu la maisha ya binadamu, ili kuweza kumwandalia njia yule atakayekuja kuwahukumu wazima na wafu na kwamba, mwisho wa siku; matumaini yatashinda tu!

Baba Mtakatifu anamwomba Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, mbele ya Msalaba wake Mtakatifu, anapenda kwa niaba ya familia ya Mungu kupiga magoti ya aibu, akiwa na matumaini, ili aweze kuwasafisha kwa maji na damu azizi iliyobubujika kutoka ubavuni mwake, ili aweze kuwasamehe; aweze kuvunjilia mbali mnyororo wa ubinafsi, upofu wa kutenda mapenzi ya Mungu pamoja na kupenda mno kumezwa na malimwengu. Anamwomba Kristo awasaidie waja wake kuona fahari ya Msalaba, ili kuuabudu na kuutukuza, kwani ni kwa njia ya Msalaba, Yesu ameonesha ubaya wa dhambi na ukuu wa huruma na upendo wake; ameonesha ubaya wa shutuma za binadamu kwa nguvu ya huruma yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.