2017-04-15 08:59:00

Ni Pasaka ya Bwana, Tuishangilie na kuifurahia!


Bwana amefufuka kweli kweli, Aleluya! Haya ndiyo mashangilio yetu yanayotawala furaha yetu wakati maadhimisho ya sherehe kubwa hivi. Yeye aliyeteswa, aliyesulubiwa na kuuwawa juu ya msalaba amefufuka, ametoka kaburini, mshindi na hafi tena. “Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni”. Tushangilie pamoja na mzaburi tukisema: “siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, tutashangilia na kuifurahia”. Kwa hakika ni siku ya shangwe kwani ukombozi wetu umetimia, tumekombolewa kutoka katika utumwa wa shetani, minyororo ya dhambi imekatiliwa mbali nasi tumefanywa kuwa huru. Ukuu wa sherehe hii unathibitishwa pia na urefu wa adhimisho lenyewe ambalo hudumu kwa takribani siku hamsini, ambamo kwamo sisi wanakanisa hupata fursa ya kumtukuza Mungu na kumshuhudia Kristo mfufuka.

Tukio la ufufuko ni la hakika. Tukiongozwa na masomo ya Dominika hii tunaweza kuchota mambo kadha wa kadha ambayo yanasakafia ukweli wa tukio hili. Injili ya Dominika hii inaweka mbele yetu picha ya kaburi tupu. Maria Magdalena anakuwa wa kwanza kulitambua hili walakini kwa ajili ya kulithibitisha na kulitapia tija anakwenda kuwataarifu mitume wake ambao wawili kati yao Petro na Yohana wanakimbia mbio nao pia wanashuhudia. Kushirikisha huku kwa Maria Magdalena kunaipa nguvu hoja hii ya uwazi wa kaburi kwani kutokana na tamaduni za kiyahudi ushahidi wa mwanamke haukuwa na nguvu sana na pia ushahidi ulitolewa na mtu mmoja tu pia ulitiliwa mashaka. Hivyo kitendo chake cha kuwashirikisha kinafanya watu watatu kuwa mashahidi na hivyo kutoweka mashaka ya aina yoyote.

Tunapoliona kaburi lipo wazi na pia somo la Injili likiongeza kwamba: “Petro akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala; na ile leso iliyokuwa kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwazongwa mbali mahali pa peke yake”, jambo linaloashiria kwamba yeye ambaye alizikwa humo hayupo kwa hakika tunasukumwa kuangalia sehemu nyingine za maandiko matakatifu ili kuthibitisha kama kweli amefufuka. Hapa ni lazima kujiuliza: kama kweli tulimzika humu na sasa kaburi lipo wazi watakuwa wamemweka wapi? Maria Magdalena alipoulizwa na Malaika sababu ya kilio chake aliwaambia: “kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka”(Yoh 20:13) au tukiangalia zaidi jinsi alivyomjibu Yule aliyedhania kuwa ni mtunza bustani kumbe ni Yesu mfufuka akisema: “Bwana ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa” (Yoh 20:15). Yote haya yanathibitisha kwamba hata kati wa wafuasi wake asubuhi ile ya ufufuko bado walikuwa katika hali ya sintofahamu.

Uthibitisho wa ufufuko wake unajisimika zaidi katika tendo la Kristo kuwatokea katika matukio kadhaa.  Kama tungebakiwa na ushuhuda huo wa uwazi wa kaburi basi tungepata shida kuuelewa ushuhuda wa mtume Petro na ujasiri alikuwa nao mbele ya Wayahudi kwamba amefufuka. Mtume Petro anasema waziwazi kwamba huyo mliyekusudia kumnyamazisha kwa sababu ya husuda na tama zenu za kibinadamu “Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika, si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndiyo sisi , tuliokula na kunya naye baada ya kufufka kwake kutoka kwa wafu”. Kristo aliwatokea mahali pengi baada ya ufufuko kuthibitisha kwamba hayumo tena kaburini, mwili wake haujaibiwa kwa kutokuukuta kaburini bali yupo hai.

Mara zote aliwathibitishia kuwa ni yeye kwa kula na kunywa nao na hata kwa mtume Tomaso alimwambia “lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; uuelete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini bali aaminiye” (Yoh 20:27). Kristo alitaka kumthibitishia kuwa si mzimu au anaona maruweruwe bali ni Yeye yuleyule waliyekuwa naye kabla ya kifo chake wakitembea naye na kula naye, yeye yuleyule waliyemshuhudia akikamatwa na kuteswa lakini sasa amefufuka. Uthibitisho huu wa muunganiko wa Kristo mfufuka na na yeye waliyekuwa naye kabla ya kifo chake uliipatia nguvu zaidi hoja ya uwazi wa kaburi kwamba yeye aliyesulubiwa msalabani hadi kifo chake, yeye aliyezikwa na siku ya tatu wanafunzi walimkosa katika kaburi lake amefufuka kweli.

Yesu mfufuka anadhihirika kwa wale waliochaguliwa na Mungu, yaani kundi zima la wafuasi wake ambamo mimi na wewe tunajumuishwa. Hapa ndipo tunapopokea wajibu wetu kama wakristo wa kudhihirisha maisha ya ufufuko. Katika Ubatizo tunakufa na kufufuka na Kristo. Mtume Paulo anatuasa kwa kusema: “yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu”. Kristo anaendelea kujidhihirisha kati yetu kwa njia mbalimbali za neema hususani kwa njia ya Sakramenti ambazo ni ishara za wazi zinazotuletea neema ya wokovu. Ushiriki wetu katika karama hizi za kimbingu ni udhihirisho wa imani yetu thabiti, imani inayotufanya na kuwezeshwa na Mungu kushuhudia kweli amefufuka. Ufufuko wake unatuletea wokovu kwani unatuondoa katika utumwa wa shetani na kuwa wana huru wa Mungu.

Ufufuko wa Kristo ni ukamilifu wa historia ya wokovu wa mwanadamu. Wakati wa sherehe za kuzaliwa kwake Kristo tulimtambuisha tukisema mwokozi wetu amezaliwa. Maisha yake ya hadharani yaliyoambatana na mafundisho yake, miujiza yake na uponyaji yameliandaa tendo hili kubwa linaloudhihirisha upendo wa Mungu. Hili linafafanuliwa na ukamilifu wa Fumbo la Pasaka linalohitimishwa na adhimisho hili kubwa la Dominika ya Pasaka. Hii ni kwa sababu wakati wa maisha yake ya hadharani Kristo alionesha wazi kabisa dhamira yake ya kumkomboa mwanadamu na kumtayarishia njia nzuri ya kuelekea kwa Mungu. Utendaji huu wa Kristo haukupokeleka vyema na jamii ya wanadamu ambao pamoja na wengine kuwa wamejifunika na kutenda matendo yaliyoonekana ni matendo ya dini matendo yao hayakumtukuza Mungu bali walijitukuza wenyewe. Utume wa Kristo ulikuwa tishio kwa jamii hii inayokinzana na sauti ya Mungu na hivyo walimwangamiza kwa kifo cha aibu msalabani.

Tendo la ufufuko ni ushindi kwa kazi za Kristo na anguko kwa kiburi cha mwanadamu. Hii ndiyo inayotoa maana kwa ukristo wetu. Ukristo ni maisha ya ufufuko, yaani kufufuka pamoja na Kristo na kuwa shuhuda wa maisha ya kipasaka. Mzaburi ametualika katika antifona ya mwanzo akisema: “Nimefufuka na ningali pamoja nawe; umeniwekea mkono wako, maarifa hayo ni ya ajabu, aleluya”. Ufufuko unadhihirisha mwendelezo wa uwepo wa Mungu na uwezo wake. Anasema “ningali pamoja nawe” akimaanisha kwamba alikuwa naye kabla na baada ya tendo hilo la ufufuko, uwepo ambao umedhihirisha ukuu wa mkono wa Mungu. Hii inamaanisha kwamba uaminifu wetu na kubaki kwetu katika neno la Kristo kunatushikamanisha naye na hivyo tunaendelea kuwa mashuhuda wake.

Mtume Paulo anatuambia kwamba: “Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya… kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndiyo weupe wa moyo na kweli”. Tuupokee ujumbe huu kama changamoto kwetu na hivyo shangwe na furaha ya siku hii ya leo ilete tija katika maisha yetu ya kikristo ambayo yana mshuhudia Kristo mfufuka, kwani Yeye amefufuka kweli, ameshinda mauti, kaburi lake lipo wazi nasi tumeona na kusadiki.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.