Fumbo la Pasaka la Msalaba na Ufufuko wa Kristo ni kiini cha Habari Njema ambayo Mitume na Kanisa baada yao, wanapaswa kuitangaza na kuishuhudia duniani. Mpango wa wokovu wa Mungu umetimilika mara moja tu kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu! Ijumaa kuu, ni Siku ambayo Kanisa linaadhimisha na kukumbuka mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, katika kilima cha Kalvari nje kidogo ya mji wa Yesuslemu, kiini cha imani, matuma. Ni siku ambayo kwa mateso makali na ya kutisha Yesu anakufa msalabani, ikiwa ndiyo siku ya kumi na nne ya mwezi wa Nisani. Safari hii ya mateso ilianza hivi, pale bustanini Gesthmane, bila kusema neno Yesu alijitoa kwa watesi wake, na ndipo wakamfunga mikono yake na kiuno pia, njia ya mateso ikaanza na mara wakafika nyumbani kwa kayafa, ambako Yesu alitakiwa kupelekwa mbele ya baraza.
Wakati huu ilikuwa yapata asubuhi, lakini giza lingali bado, tena hata masaa kazaa, na ilikuwa miiko kumhukumu mtu kungali giza bado, kulingana na desturi za kiyahudi. Pale ndipo wote walipokutanika mbele ya Kayafa na mara Yesu akaletwa mbele yao. Na hapo wale mashahidi wakatoa ushuhuda wa uwongo kuhusu Yesu, ili tu auwawe. Ila sasa wote mbele ya Kayafa wakasema asulubiwe. Na sasa Yesu akapelekwa mbele ya Pilato, na ilikuwa yapata saa sita kamili. Hapa watu hawakuingia ndani ya Pretorio ili wasije wakanajisika kwa kuingia katika jengo la watu wa mataifa. kwani wakati huo pia, Pasaka ya kiyahudi ilikuwa ikikaribia. Ila katika haya yote hawakusita kumsulibisha mtu asiyekuwa na hatia yeyote. Na ndipo Pilato akampeleka Yesu kwa Herode, na ndipo Herode akafadhaika sana, kwani alijua makuu aliyotenda Yesu. Na kwa mfadhaiko huo Herode alimrudisha tena Yesu kwa Pilato.
Hapo ndipo Pilato akamtwaa Yesu mbele ya watu, na kwa maneno haya akamtambulisha Yesu; tazameni mtu (ecce homo). Maana halisi ya neno hili Tazameni mtu, ni rejeo la maneno yaliyonenwa na Nabii Isaya akisema ”wengi waliomwona walishtuka, kwa vile sura yake ilikuwa imeharibiwa, hakuwa tena na umbo la kibinadamau. Is 52:14. Tazameni Mtu, mtu wa masikitiko makubwa, anavyoangaika Msalabani, akiwa uchi, akitemewa mate, wakimkejeli na kumdhihaki, amedhoofika na hata mifupa yake inahesabika. Basi, Tazameni Mtu, “ Ecce homo”, Nabii Isaya anaendelea kutuambia “hakuwa na umbo, wala sura ya kutupendeza, wala hakuwa na uzuri wowote wa kuvutia, alidharauliwa na kukataliwa na watu, alikuwa mtu wa huzuni na uchungu, alikuwa kama mtu kinyaa kwa watu, alidharauliwa na akaonenakana si kitu. Is 53:2-3. Angalia mateso haya tafakari tuwe na uchungu wa dhambi moyoni, tuomboleze na kulia kwa toba na wongofu wa ndani na huruma na msamaha wa Mungu utuinue tena!
Ecce homo: Tazameni mtu, Huu ni upendo wa Yesu, upendo usiopimika , kwani leo ametufia msalabani , amesulibiwa kwa dhambi zetu , hichi ndicho kifo kilichonenwa na manabii , pale nabii Isaya aliposema, Alidhulimiwa, akahukumiwa na kupelekwa kuuawa, na hakuna mtu aliyejali yaliyompata, alifukuzwa kutoka nchi ya walio hai kwa ajili ya makosa ya watu wangu. Is 53:8. Utabiri mwingine wa kinabii kuhusu Yesu kusulibiwa Msalabani ni pale mfalme Daudi, mfalme wa Waisraeli, yapata miaka 1000 kabla ya Kristo, alipotabiri undani na ukatili wa kifo cha msalaba , ambacho yeye mwenyewe kamwe hawezi kukikabili. Utabiri huu tunaupata kwenye zaburi ya 22:14 – 18, inayosema.. nimekwisha kama maji yaliyo mwagika , mifupa yangu yote imetenguka , Moyo wangu ni kama nta unayeyuka ndani mwangu , koo langu limekauka kama kigae , ulimi wangu wanata kinywani mwangu, umeniacha kwenye mavumbi ya kifo. Genge la waovu limenizunguka , wamenitoboa mikono na miguu, nimebaki mifupa tupu adui zangu wananiangalia na kunisumanaga, wanagawana nguo zangu na kulipigia kura vazi langu. Zab 22;14-18.
Maziko ya Yesu nayo pia yalikuwa yamekwisha tabiriwa kuwa yatakuwa ni maziko ya namana gani, pale nabii isaya anapotuambia.. walinizika pamoja na wahalifu , katika kifo aliwekwa pamoja na matajiri, ingawa hakutenda ukatili wowote, wala hakusema neno lolote la udanganyifu. Is 53:9. Utimilifu wa maneno haya ni kwamba Yesu amekufa kama mtu dhaifu katika macho ya Dunia na katikati yake wahalifu wawili walisulibiwa naye. Mt 27:38. Na baada kifo chake mtu tajiri Yosefu wa Arimathaya aliomba mwili wake ili kwenda kuuzika.
Maandiko haya ya manabii yametimia leo ili tupate kuamini kuwa Yesu ni Bwana na kwa dhambi zetu amekufa mauti tena mauti ya msalaba ili apate kutukuomboa na kutuelekeza wote kwa Baba. Mwimbaji mmoja aliimba ila kwa kiingereza ( where you there when they crucified my lord...yaani: Je,’ ulukuwepo walipomsulibisha Bwana wangu .. akaendelea sometimes it does indeed cause me to tremble....yaani hunifanya hata mara kutetemeka ninaposikia maneno haya Msalabani Yametimia, ndipo akainamisha kichwa akatoa roho. Yametimia maana yake, yamekamilika, kukamilishwa katika kizingiti cha juu na cha mwisho kabisa ikichorwa milele katika mawazo na mioyo ya mwanadamu.
Na Padre Agapiti Amani ALCP/OSS.
All the contents on this site are copyrighted ©. |