2017-04-14 14:51:00

Papa Francisko kutembelea Bologna na Cesena, 1 Oktoba 2017


Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Askofu mkuu Matteo Maria Zuppi wa kutembelea Jimbo kuu la Bologna, nchini Italia ili kushiriki Kongamano la Ekaristi Takatifu Kijimbo pamoja mwaliko mwingine kutoka kwa Askofu Douglas Regattieri wa Jimbo Katoliki Cesena-Sarsina kwa ajili ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 300 tangu alipozaliwa Papa Pio VI, wakati huo akijulikana kama Giannangelo Braschi. Ziara hii ya Baba Mtakatifu Francisko katika majimbo haya itakuwa Jumapili tarehe 1 Oktoba 2017.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ataondoka kwa Elikopta kutoka Uwanja wa Ndege wa Vatican majira ya saa 1: 00 na kuwasili mjini Cesena baada ya saa moja. Hapa atapata nafasi ya kuweza kuzungumza na wananchi kwenye Uwanja wa “Popolo”, baadaye atakutana na Wakleri, Vijana na Familia kwenye Kanisa kuu la Jimbo la Cesena-Sarsina.

Majira ya saa 4:00 asubuhi, Baba Mtakatifu ataondoka Cesena kuelekea Jimbo kuu la Bologna na baada ya mwendo wa dakika ishirini, atawasili mjini Bologna na kukutana na kundi la vijana wahamiaji kutoka Afrika ya Kaskazini wanaopata hifadhi Jimbo Bologna. Majira ya mchana, atashiriki na waaamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kwa sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja mkubwa na baadaye atapata chakula cha mchana na maskini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petronio. Baadaye jioni, atakutana na kuzungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu na baadaye atakutana na Wakleri.

Saa 11: 00 Jioni kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kwa namna ya pekee, Jimbo kuu la Bologna, hii ni Jumapili ya Neno la Mungu, changamoto kwa waamini kuzama zaidi katika mchakato wa kulisoma, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Siku hii, waamini wote watakabidhiwa nakala ya Injili na baadaye, Baba Mtakatifu Francisko atahitimisha hija yake na kurejea tena mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.