2017-04-14 16:23:00

Mchango wa Ijumaa kuu unapania kuwasha moto wa matumaini!


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, mwanzo mwa kipindi cha Kwaresima aliwaandikia Maaskofu barua ya kuwakumbusha umuhimu wa mchango unaotolewa na waamini wakati wa maadhimisho ya Ijumaa kuu ili kusaidia mchakato wa maendeleo katika Nchi Takatifu. Anasema, lengo la mchango huu ni kuendeleza matumaini kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati wanaoishi katika hali tete sana ya historia na maisha yao kama Wakristo.

Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu yawe ni chemchemi ya ushuhuda wa upendo na mshikamano kwa wananchi walioko huko Mashariki ya Kati, mahali ambapo ni chimbuko la Habari Njema ya Wokovu. Tangu mwanzo wa Kanisa, wakristo huko Mashariki ya Kati wamekuwa kweli ni mashuhuda wa Injili, changamoto na mwaliko wa kuendelea kuungana kwa kuchangia kikamilifu ustawi na maendeleo ya wananchi huko Mashariki ya Kati. Mchango ulitolewa kwa Mwaka 2016 umesaidia kwa kiasi kikubwa katika ukarabati wa maeneo matakatifu. Itakumbukwa kwamba, mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu ulianzishwa na Mwenyeheri Paulo VI ili kusaidia kulinda na kudumisha anama na urithi wa Wakristo huko Mashariki ya Kati, lakini ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza.

Kardinali Sandri anakaza kusema, maisha ya Wakristo huko Iraq, Syria na Misri ni tete sana; kwani huku ni mahali ambako uekumene wa damu unaendelea kushika kasi kutokana na mauaji ya mara kwa mara kwa Wakristo katika nchi hizi. Kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma mbali mbali kuna Wakristo ambao wanalazimika kuyakimbia makazi yao na hata wakati mwingine kuikana imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kuwasha moto wa matumaini kwa Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati.

Msaada wa kwanza unaopaswa kutolewa ni sala inayojikita katika uekumene wa sala. Pili ni uekumene wa huduma, ili kusaidia kugharimia miradi mbali mbali ya maendeleo kwa wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati pasi na upendeleo, hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu. Fedha hii inasaidia pia kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta, hifadhi na usalama wa maisha yao. Waamini wanahamasishwa kuendelea kufanya hija za maisha ya kiroho huko katika Nchi Takatifu kama kielelezo cha uekumene wa maisha ya kiroho. Ni mahali muhimu sana pa historia, imani na maisha ya Kikristo, chombo muhimu sana katika mchakato mzima wa uinjilishaji. Sehemu kubwa ya pato la wananchi wa maeneo matakatifu linatokana na mchango wa mahujaji katika Nchi Takatifu.

Maadhimisho ya Juma kuu, yawasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa amani inayobubujika kutoka katika nyoyo za watu, lakini zaidi, amani kwa familia ya Mungu inayoishi kwenye Nchi Takatifu. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko linapenda kuwashukuru wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuchangia ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.