2017-04-14 17:06:00

Hata katika madhulumu, Wakristo wanaitwa kuwa waaminifu kwa Kristo!


Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli hivi karibuni amemwandikia Papa Tawadros II wa Kanisa la Kikoptik, ujumbe wa imani na matumaini baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea nchini Misri wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi. Hii ni changamoto kubwa inayosababishwa na watu wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani lakini pia ni uchungu mkubwa kwa watu wanaowalilia na kuwaombolezea ndugu zao waliopoteza maisha kutokana na mashambulizi haya.

Hata hivyo ni wajibu wa Wakristo wote kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake hata katika hali tete kama  hizi. Mashambulizi ya kigaidi kwa watu waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya sala ni uvunjaji mkubwa wa haki msingi za binadamu. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, Makanisa yote yanafungamanishwa na uekumene wa damu kutokana na Wakristo sehemu mbali mbali za dunia kumwaga damu yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Licha ya patashika nguo kuchanika, Wakristo hawana budi kuendelea kubaki kuwa waamini hata kiasi cha kuyamimina maisha yao kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu, daima yuko pamoja nao na kamwe hatawaacha pweke.

Yesu ni chemchemi ya wokovu wao na kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amewakomboa wanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa njia ya unyenyekevu, uvumilivu, huruma, upole, msamaha na mapendo ya dhati ameshinda mateso yote na hatimaye kufufuka kwa wafu! Waamini wanakumbushwa umuhmu wa kukumbatia na kuambata Heri za Mlimani kama muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu hasa pale wanapokumbana na hali tete katika maisha na ufuasi wao kwa Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.