2017-04-13 14:31:00

Papa Francisko: Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha kwa watu wake!


Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini Habari Njema, amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa. Kwa muhtasari huu ndio utume uliotekelezwa na Kristo Yesu katika maisha yake, dhamana inayoendelezwa na Mapadre kwa kuwashirikisha watu wa Mungu, furaha ya Injili; kuwaondolea watu dhambi zao kwa kuwapaka mafuta ya huruma, kwa kutambua kwamba, Mapadre wamepakwa mafuta ili kushiriki ukuhani wa Kristo Yesu, dhamana wanayopaswa kuitekeleza kwa ukamilifu wote katika maisha yao.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya Alhamisi kuu asubuhi, tarehe 13 Aprili 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kubariki Krisma ya Wokovu; mafuta yatakayotumia kwa ajili ya wagonjwa, wakatekemeni na Krisma itakayotumika kwa ajili ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa. Mapadre wamerudia tena ahadi za utii kwa Askofu mahalia mbele ya watu wa Mungu kama walivyofanya siku ile walipopewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekaza kusema, Padre anatangaza na kushuhudia furaha ya Injili wakati wa mahubiri yake, hasa yakiwa mafupi na yanayogusa ujumbe wa Neno la Mungu pale inapowezekana, ili kweli waamini waweze kuguswa katika akili na nyoyo zao kwa Neno na Sala zake kama alivyoguswa pia na Kristo Yesu. Padre anapaswa kuwa mmissionari na shuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, kwa kusimama karibu na wanyonge na wale wanaohitaji msaada wake, ili wote hawa waweze kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu. Mapadre, kimsingi ni mashuhuda na watangazaji wa Injili ambayo kimsingi ni chemchemi ya furaha kwa watu.

Hii hazina yenye thamani kubwa na kiini cha maisha na utume wa Kanisa unaobubujika kwa Mapadre kupakwa mafuta na kabla yao ni Kristo Yesu, Kuhani mkuu aliyepakwa mafuta na Roho Mtakatifu tangu akiwa tumboni mwa Bikira Maria, akawa ni kielelezo cha furaha iliyoujaza ukimya wa moyo wa Mtakatifu Yosefu; mafuta yaliyomfanya Yohane Mbatizaji akaruka tumboni mwa mama yake Elizabeth, Yesu anarejea tena katika maisha ya waja wake ili kuwatangazia furaha ya Injili inayogeuka na kuwa furaha na ukweli katika huruma.

Haiwezekani kutenganisha mambo makuu ya Injili: ukweli usiojadilika; huruma inayowaambata watu wote na furaha ya kweli inayojikita katika undani wa mtu pamoja na kuwakumbatia wote! Furaha ya Kristo Yesu ni kuona  maskini wakiinjilishwa na watoto wakishiriki katika dhamana na utume wa Kuinjilisha. Furaha ya Injili inamguso tofauti kwa kila mwamini kama kielelezo cha upya wa Neno la Mungu. Hii ni furaha ambayo Mapadre wanapaswa kuimwilisha katika maisha na utume wao kwa kuilinda Injili.

Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kuhakikisha kwamba, Injili wanayoitangaza na kuishuhudia inaendana na kipimo cha watu wao kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya. Wawe tayari kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyetoka kwa haraka na kwenda kumhudumia binamu yake Elizabeth; mapadre wawe tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo inayowaondolea watu woga na wasi wasi wa maisha; kwa kuonesha ujasiri unaosheheni nyoyo na maisha ya wale wote wanaobahatika kukutana na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha Mapadre wenzake kwamba, Yesu Kristo ni chemchemi ya maji ya uhai yanayoweza kuzima kiu ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya watu kama alivyofanya kwa Mwanamke Msamaria pale kisimani na hatimaye, Roho Mtakatifu akawajaza neema wananchi wa mji ule kiasi cha kuthubutu kumkaribisha Yesu kuendelea kukaa kati yao. Hivi ndivyo alivyofanya Mama Theresa wa Calcutta kwa kuzima kiu ya upendo, huruma na faraja kwa maskini sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Habari Njema ya Wokovu inabubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu uliochomwa kwa mkuki na humo kunabubujika, wema wote, unyenyekevu na ufukara unaowavuta wengi kwake. Mapadre wanapaswa kumjifunza Kristo Yesu, ili waweze kutangaza na kushuhudia kwa dhati kabisa Injili ya wokovu kwa maskini, kwa kuwaheshimu na kuwathamini, kiasi hata cha kujisadaka bila ya kujibakiza bila kujidai kwa jambo lolote lile!

Mapadre wajifunze kutangaza na kushuhudia ukweli wote hata kama utawagharimu kwani Roho Mtakatifu anawafundisha kusema yale wanayopaswa kusema kwa wakati muafaka. Ukweli huu unawakirimiwa maskini furaha, unawapatia ari mpya wadhambi na kuwapatia tena nafasi ya kuweza kupumua wale waliopagawa na pepo wachafu! Haya ndiyo mambo makuu ambayo Baba Mtakatifu anawaalika Mapadre wenzake kuyatafakari na kuyamwilisha katika maisha na utume wao, ili kweli Habari Njema ya Wokovu iweze kupata utimilifu wake ndani mwao kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyeweza kuitangaza na kuishuhudia katika ukweli wote; kwa kumwambata yule mwanamke Msamaria; hii ndiyo furaha inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu na kuenea katika nyoyo za watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.