2017-04-13 17:12:00

Muziki mtakatifu unapaswa kuwafikia hata walioko pembezoni mwa jamii


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amepokea CD mbili kutoka katika Kwaya ya Kikanisa cha Sistina kilichoko mjini Vatican, CD ambazo zinaenda kwa jina, “Cantate Domino” yaani “Mwimbieni Bwana”, ambazo zitaanza kuuzwa wakati wowote kuanzia sasa. CD hizi zimeandaliwa na Gazeti  la “Repubblica” linalochapishwa kila siku nchini Italia. CD hizi anasema Monsinyo Massimo Palombella, Mkurugenzi wa Kwaya ya Kikanisa cha Sistina anasema kuwa ni mkusanyiko wa nyimbo ambazo zimeimbwa na kwaya hii na kurekodiwa kwa mara ya kwanza kabisa katika Kikanisa cha Sistina.

Katika CD hizi pia kuna nyimbo za misa ya “Papae Marcelli na Mottetti”  wa Palestrina ambazo ziliimbwa kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1567. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kwaya ya Sistina, Gazeti la “Repubblica” pamoja na viongozi wa idara ya Muziki kutoka Italia. Monsinyo Massimo Palombella, Mkurugenzi wa Kwaya ya Kikanisa cha Sistina anasema uzinduzi wa CD hizi ni sehemu ya utekelezaji wa mantiki ya Baba Mtakatifu Francisko kuhakikisha kwamba, hata watu wanaoishi pembezoni mwa jamii na katika mambo msingi wanafikiwa na furaha ya Injili kwa njia ya muziki mtakatifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.