Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko kuadhimisha kumbu kumbu ya mashuhuda wapya wa imani!

Papa Francisko tarehe 22 Aprili 2017 ataadhimisha Liturujia ya Neno la Mungu kama sehemu ya kumbu kumbu ya mashuhuda wa imani wa karne ya XX na karne ya XXI. - ANSA

12/04/2017 13:44

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, wakristo wengi wamepoteza maisha yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, pengine kuliko hata ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo. Ushuhuda wa mateso na kifo cha waamini hawa ni chemchemi kwa Makanisa kujikita zaidi na zaidi katika uekumene wa damu unaowaunganisha wakristo wote katika mateso na kifo, kama njia ya kumfuasa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso, dhuluma na nyanyaso na vifo vya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tarehe 22 Aprili 2017 saa 11: 00 kwa Saa za Ulaya ataadhimisha Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Bartolomeo lililoko kwenye Kisiwa cha Tiberina kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao makuu yake mjini Roma. Hii ni taarifa ambayo imetolewa na msemaji mkuu wa Vatican Dr. Greg Burke.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imepokea kwa mikono miwili na kwa moyo wa shukrani taarifa ya Baba Mtakatifu Francisko kuungana nao katika Liturujia ya Neno la Mungu kama sehemu ya kumbu kumbu ya mashuhuda wa imani walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake katika karne ya XX na XXI. Sala hii ni kutaka kutoa heshima kwa wakristo wanaoendelea kujisadaka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wakati wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 Ukristo, Mtakatifu Yohane Paulo II aliomba masalia ya mashuhuda wa imani kwa nyakati hizi yahifadhiwe kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Bartolomeo. Hii ni nafasi ya pekee kabisa wakati huu ambapo kuna wakristo wengi wanaoendelea kuteseka, kunyanyasika na kuuwawa kikatili kwa ajili ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A, Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

12/04/2017 13:44