2017-04-10 11:17:00

Rithisheni vijana wa kizazi kipya utamaduni wa haki na amani duniani


Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia Kardinali Blase Joseph Cupich wa Jimbo kuu la Chicago, nchini Marekani anasema, si rahisi sana kwa watu kujikita  katika njia ya amani, lakini hii ndiyo njia ambayo ni muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya watu. Jimbo kuu la Chicago ni kati ya maeneo hatari sana nchini Marekani kutokana na vitendo vya uvunjifu wa amani. Tarehe 4 Aprili 2017, Jimbo kuu la Chicago limezindua kampeni ya amani, wakati ambapo Marekani na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake inafanya kumbu kumbu ya ya miaka 49 tangu Martin Luther King alipouwawa kikatili kutokana na msimamo wake wa kupigania na kutetea haki za wanyonge ndani ya jamii. Kampeni hii itahitimishwa, wakati wa maadhimisho ya Ijumaa kuu, Kanisa linapotafakari kuhusu Fumbo la Msalaba!

Baba Mtakatifu Francisko anamwona Mchungaji Martin Luther King kuwa ni kiongozi na mtume mpenda amani  pamoja na kuwa ni mtetezi wa haki msingi za binadamu, changamoto na mwaliko kwa watu wote wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kukataa kishawishi cha kulipizana kisasi na kuendeleza “mtima nyongo” na badala yake wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu; tunu msingi zinazofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika upendo wa dhati! Huu ni utajiri na changamoto kubwa wanayopaswa kurithishwa vijana wa kizazi kipya ili kuwajengea na kudumisha utamaduni wa amani kati ya watu, ndoto ambayo kimsingi inawezekana kabisa, ikiwa kama watu wataonesha utashi wao.

Utamaduni wa haki na amani, upendo na mshikamano unaovunjilia mbali kuta za utengano na ubaguzi; unaweza kuganga na kuponya madonda ya ubaguzi wa kitaifa kiasi hata cha kugusa Jimbo kuu la Chicago, ili kweli liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuihakikishia familia ya Mungu Jimbo kuu la Chicago, uwepo wake wa kiroho kwa njia ya sala, ili uzuri wa Jimbo kuu la Chicago usipotee kwa kukosa matumaini, kwani wote wanapaswa kushirikiana na kushikamana ili waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa amani, kwa kuwaonesha na kushuhudia kwa vijana wa kizazi kipya nguvu ya upendo wa dhati unaobubujika kutoka katika undani wa watu!

Baba Mtakatifu anapenda pia kuyaelekeza mawazo na sala zake kwa wahanga wa vitendo vya uvunifu wa haki na amani Jimbo kuu la Chicago, huko  Marekani. Anatambua kwamba, kuna watu wengi ambao wamewapoteza ndugu, jamaa na marafiki kutokana na vitendo vya kihalifu. Baba Mtakatifu anasema, yuko karibu nao kwa njia ya sala, ili kweli waweze kuguswa na hatimaye, kuponywa na neema, huruma na upendo wa Mungu ndani mwao, tayari kujikita katika mchakato wa upatanisho na msamaha wa kweli.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba watu kutoka katika makabila, matakabaka ya kijamii na yenye uwezo mdogo wa kiuchumi wanabaguliwa na kunyanyaswa sana sehemu mbali mbali za dunia! Ni makundi ya watu wanaopokonywa haki zao msingi; wanaoteseka na kunyanyasika; watu ambao kimsingi wanaangaliwa na jamii kwa “jicho la kengeza”. Kuna haja ya kusimama kidete kupinga tabia ya ubaguzi na vitendo vyote vinavyowasukumiza wengine pembezoni mwa jamii kwa kutambuana kwamba, wote ni ndugu wamoja, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu anahitimisha barua yake kwa Kardinali Blase Joseph Cupich wa Jimbo kuu la Chicago, nchini Marekani kwa kusema kwamba, tabia hii ya kuwa wazi: kimoyo na kiakili inapaswa kufundishwa na kumwilishwa kuanzia kwenye familia na shuleni. Baba Mtakatifu anapenda pia kuwahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala wakati wa maandamano ya amani, wakati mjini Roma, Kanisa litakua linaadhimisha Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo ili kutafakari kwa kina na mapana Fumbo la Msalaba, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.