2017-04-10 14:54:00

Mshikamano na uekumene wa damu na Wakristo nchini Misri!


Dr. Olav Fyske Tveit, katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwengu, WCC., amelaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea nchini Misri na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha na wengine wengi kupata majeraha makubwa wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, tarehe 9 Aprili 2017. Baraza la Makanisa Ulimwenguni limetuma salam zake za rambi rambi kwa Papa Tawadros II wa Kanisa la Kikoptic la Misri kama kielelezo cha umoja na mshikamano katika kipindi hiki kigumu cha historia ya Kanisa lao.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawataka wananchi wa Misri kushikamana ili kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa kwa kukataa kishawishi cha kutaka kuwagawa kwa misingi ya udini usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa wananchi wa Misri. Baraza la Makanisa linamtaka Rais Abdel Fattah-Al Sisi wa Misri kuhakikisha kwamba, Serikali yake inalinda na kudumisha uhuru wa kuabudu, ulinzi na usalama kwa raia na mali zao pamoja na kuhakikisha kwamba, waamini wenye misimamo mikali ya kiimani wanaotaka kuvuruga haki msingi za binadamu, amani na mafungamano ya kijamii wanashughulikiwa kisheria.

Kwa upande wake Askofu Antonios Aziz Mina, Askofu mstaafu wa Kanisa la Kikoptiki la Guizeh, Misri anasema mashambulizi haya ya kigaidi yamewalenga Wakristo wakati huu  wa maadhimisho ya Juma kuu, lakini pia yanahatarisha amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa; mashambulizi ambayo kamwe hayamwogofya Papa Fran cisko kutembelea Misri kuanzia tarehe 28 – 29 Aprili 2017 na kwamba hija yake itasaidia kuwaimarisha Wakristo ambao kwa miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakikabiliwa na mashambuli ya mara kwa mara kutoka kwa waamini wenye misimamo mikali ya kiimani.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limelaani kwa nguvu zote mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea nchini Misri na kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu. Inasikitisha kuona kwamba, mashambulizi haya yamefanywa wakati Wakristo wanaadhimisha Jumapili ya Matawi. Familia ya Mungu nchini Misri ijikite katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; iendeleze mchakato wa uponyaji wa madonda ya misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kujenga umoja na mafungamano ya kijamii. Umefika wakati wa kusimama kidete kupinga na kulaani utengenezaji na biashara haramu ya silaha inayoendelea kupandikiza mbegu ya utamaduni wa chuki na kifo, lakini jambo la msingi linalopaswa kukumbukwa ni kwamba, Fumbo la Pasaka litaendelea kung’ara katika maisha ya watu!

Viongozi mbali mbali wa kidini kutoka Uingereza kwa pamoja wamelaani mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Wakristo huko Misri na kwamba, hakuna sababu yoyote msingi inayoweza kukubalika ili kuhalalisha mashambulizi haya ya kinyama dhidi ya watu waliokuwa wanasali kama sehemu ya utekelezaji wa haki yao kikatiba. Nalo Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani linaungana na wakristo waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika mashambulizi ya kigaidi nchini Misri, Jumapili ya Matawi, tarehe 9 Aprili 2017. Salam za rambi rambi na mshikamano zimetolewa pia na Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji kwa kuitaka Serikali ya Misri kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu, upendo na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu nchini Misri. Shirika hili linasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri ni muhimu sana katika kujenga na kudumisha uekumene wa damu miongoni mwa Wakristo pamoja na kukataa kishawishi cha utamaduni wa kifo na kutaka kulipizana kisasi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.