2017-04-08 09:57:00

Umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika maisha ya waamini!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, “Misericordiae vultus” anasema, Kanisa limeagizwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu ambao ni kiini cha Injili; huruma ambayo kimsingi inapaswa kupenya na kugota katika moyo na akili ya binadamu. Kanisa linapaswa kuwaendea wote pasi na ubaguzi kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ushuhuda unaofumbata huruma ya Mungu, mwanga na njia inayowaelekeza watu kwa Baba wa milele! Huruma ya Mungu ni sehemu ya mpango wa maisha unaoleta furaha na amani ya ndani! Mapadre kwa namna ya pekee ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu inayoadhimishwa kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Upatanisho!

Padre Rocco Rizzo, Mratibu mkuu wa waungamishaji kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ilikuwa ni nafasi muafaka kwa waamini wengi kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kwa njia ya Saramenti ya Upatanisho, matendo makuu ya Mungu kwa mwanadamu! Waamini na watu wenye mapenzi mema wamegundua tena ndani mwao furaha, amani na utulivu wa ndani unaofumbatwa katika toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho. Imekuwa ni nafasi ya kushirikisha na kuhamasishana kuhusu umuhimu wa jamii kujikita katika huruma, upendo na msamaha; mambo msingi yanayokuza na kudumisha mafungamano ya kijamii, chachu muhimu sana ya maendeleo endelevu ya binadamu!

Padre Rocco Rizzo anakaza kusema, waamini wengi ambao walikuwa wamesahau mahali ulipo mlango wa Kanisa, lakini zaidi mahali ambapo kilipo kiti cha huruma ya Mungu, walipata nafasi ya kuweza kukimbilia na kuambata tena ndani mwao, huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, hali inayoonesha kwamba, kweli waamini walikuwa na kiu ya kutubu na kuongoka, tayari kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Maadhimisho ya Mafumbo makuu ya Kanisa hasa wakati wa Pasaka na Noeli ni muda muafaka wa kutubu na kuongoka, ili kuadhimisha Mafumbo ya imani kwa moyo mweupe na ushiriki mkamlifu.

Wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kulikuwepo na Mapadre waungamishaji 13 wanaounda Baraza la Waungamishaji wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na wengine 30 waliongezwa ili kurahisisha maungamo kwa mahujaji na waamini waliokuwa wanataka kujipatanisha na Mungu. Inafurahisha kuona kwamba, kuna idadi kubwa ya vijana wa kizazi kipya wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Lakini bado kuna haja ya kuandamana, kuwasindikiza na kuwafunda vijana wa kizazi kipya mambo msingi ya imani, maisha na utume wa Kanisa! Changamoto kubwa kwa vijana ni kupekua dhambi, kutubu, kuungama na kutimiza malipizi.

Vijana wengi wamepoteza dhana ya dhambi kwa kuwa na dhamiri mfu! Kuna dhambi ambazo zimegeuka kuwa ni sehemu ya mazoea kiasi kwamba, hawaoni tena sababu ya kuziungama. Kumbe, vijana wanapaswa kusaidiwa kujenga dhamiri nyofu, tayari kutambua mapungufu yao na kuyaungama. Wajitahidi kuwa ni majembe ya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2017. Baba Mtakatifu anawakumbusha waungamishaji kwamba, wao pia ni wadhambi walionjeshwa huruma na upendo wa Mungu, kumbe wawe wanyenyekevu wanapoadhimisha mafumbo ya huruma ya Mungu. Waoneshe: ukarimu, utu wema, huruma na upendo kwa waamini wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Malipizi ya dhambi yasaidie kumfunda na kumjenga mwamini katika mambo matakatifu; kwa kujikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.