2017-04-08 13:30:00

Papa Francisko anawataka vijana kuwa mashuhuda wa furaha ya Injili


Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo kwa Mwaka 2017 yanayoongozwa na kauli mbiu “Mwenye nguvu amenitendea makuu” ni nafasi maalum kwa Maaskofu mahalia kukutana na kuzungumza na vijana katika majimbo yao kama sehemu ya mchakato wa ushiriki wa vijana katika maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana sanjari na maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama. Baba Mtakatifu Francisko anasisitiza kwamba, vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuhusishwa kikamilifu katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”.

Lengo ni kuwawezesha vijana ili hatimaye waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa wale wanaowazunguka. Lakini, ili kuweza kutekeleza dhamana na changamoto hii katika maisha, vijana wanapaswa kufundwa vyema katika mwanga wa Injili ya Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Mtume Yohane, mwanafunzi aliyependwa zaidi na Yesu pamoja na Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa ndiyo mihimili mikuu iliyoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko ili kuongoza mchakato wa maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana kwa Mwaka 2017 Jimbo kuu la Roma yamepambwa kwa uwepo na ushiriki wa ujumbe wa vijana 300 kutoka katika nchi 103 na vyama 44 vya kitume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya wanaoshiriki katika kongamano la kimataifa ili kufanya tathmini ya kina mintarafu maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani, Jimbo kuu la Cracovia, Poland tayari kuweka sera, mipango na mikakati ya maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa nchini Panama kunako mwaka 2019. Kongamano hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kushirikiana na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu.

Askofu Fabio Bene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu katika mahojiano maalum na Radio Vatican anaelezea kuhusu umuhimu wa maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yatakayolisaidia Kanisa kujipyaisha, tayari kuandamana, kuwasikiliza na kuwafunda vijana  katika mwanga wa Injili. Haya yanawezekana kwa uwepo na ushiriki wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia hii, vijana ambao ni jeuri na matumaini ya Kanisa na Jamnii, wataweza kuchangia katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kristo miongoni mwa watu wa Mungu.

Vijana hawawezi kutembea peke yao, watajikwaa na kuanguka, wanapaswa kuandamana na waamini waliokomaa katika imani, matumaini na mapendo; watu wenye msimamo thabiti kimaisha na kimaadili; waamini ambao wako tayari kuwa kweli ni dira na mwongozo katika maisha ya vijana. Katika mwelekeo huu, kweli Kanisa linaweza kuendelea kujizatiti katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kati ya watu wa Mungu. Hii ni Sinodi kwa ajili ya vijana pamoja na vijana anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maandalizi na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, tayari kupokea matunda ya Sinodi na kuyamwilisha katika vipaumbele vya maisha yao. Bikira Maria, nyota ya uinjilishaji mpya awasaidie vijana kuiga mfano bora wa mtume Yohane, mwanafunzi aliyependwa sana na Yesu, akamfuasa Kristo katika maisha yake kiasi hata cha kushuhudia mateso, kifo na ufufuko wake; akawa na ujasiri wa kutangaza Fumbo la Ufufuko wa Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.