2017-04-07 13:30:00

Sinodi ya Maaskofu: Ni kwa ajili ya vijana pamoja na vijana!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, Kanisa linataka kuandamana na kushibana na vijana ili kuwasikiliza, kuwafunda na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbali mbali ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayofanyika mwezi Oktoba 2018 mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” ni nafasi ya pekee kwa Maaskofu kuwasikiliza vijana kwa makini ili hatimaye, Kanisa liweze kuibua mbinu mkakati wa utume kwa vijana wa kizazi kipya.

Kardinali Lorenzo ameyasema haya Alhamisi, 6 Aprili 2017 kwa wajumbe 300 kutoka katika nchi 103 na vyama 44 vya kitume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya wanaoshiriki katika kongamano la kimataifa ili kufanya tathmini ya kina mintarafu maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani, Jimbo kuu la Cracovia, Poland tayari kuweka sera, mipango na mikakati ya maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa nchini Panama kunako mwaka 2019. Kongamano hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kushirikiana na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu.

Kardinali Baldisseri amewakumbusha vijana kwamba, wao ndio walengwa wakuu wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018. Ni Sinodi inayowalenga vijana wote wa kizazi kipya kutoka ndani na nje ya Kanisa. Jambo la msingi ni kutambua matumaini, changamoto na fursa ambazo vijana wanaweza kuzitumia katika kufanikisha ndoto zao za maisha kwa kusaidiwa na mwanga wa Injili. Vijana ni jeuri na amana ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, kumbe, wanapaswa kupewa uzito wanaostahili katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Kanisa linataka kuwa ni daraja linalowaunganisha na kuwakutanisha vijana pamoja na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Kardinali Baldisseri anakaza kusema, maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani huko Panama kwa mwaka 2019 yanamweka Yohane, yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu kuwa ni mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya katika hija ya maisha yao hapa duniani. Yohane, aliamua kumfuasa Kristo Yesu bila kuogopa akaandamana naye hadi pale Mlimani Kalvari alipomwona Yesu anainamisha kichwa na kukataa roho! Kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, changamoto na mwaliko kwa vijana kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu.

Maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani katika kipindi cha miaka mitatu yatakuwa chini ya ulinzi, tunza na tafakari ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, aliyethubutu kumtungia Mungu utenzi wa sifa kwa vile “Mwenyezi Mungu alikuwa amemtendea makuu katika maisha yake”, kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2017 inayoadhimishwa kwa ngazi ya Kijimbo, Jumapili ya Matawi, tarehe 9 Aprili 2017 kwa vijana kuwazunguka Maaskofu wao mahalia! Mjini Roma, vijana hawa watamzunguka Baba Mtakatifu Francisko kwenye mkesha wa maadhimisho haya utakao fanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Mkuu lililoko Jimbo kuu la Roma na Jumapili, vijana wataandama na matawi kumshangilia Kristo Yesu: Masiha na Mfalme anayeingia Yerusalemu kwa unyenyekevu mkubwa.

Kwa upande wake, Askofu Fabio Bene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu amepembua kwa kina na mapana mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu na hatua ambayo kwa sasa imefikiwa na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Maneno mazito yanayopaswa kuzingatiwa katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ni pamoja na: Kusikiliza kwa makini; kuwahusisha vijana ambao ni walengwa wakuu; kutambua, kufasiri matukio katika mwanga wa Injili na kuchagua vipaumbele katika maisha; kuandamana na kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya katika maisha na utume wa Kanisa.

Ni matumaini ya Sekretarieti kuu ya Sinodi kwamba, Majimbo mbali mbali yataweza kutunga sala kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa Vijana. Mwezi Septemba, 2017 kutafanyika semina ya kimataifa kuhusu ulimwengu wa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko amekwisha kusema kwamba, vijana ndio walengwa wakuu wa Sinodi ya Vijana, watakaosindikizwa na Mababa wa Sinodi. Ni maadhimisho yanayowagusa watu wote wa Mungu kutoka katika medani mbali mbali za maisha, tayari kuhitimisha mchakato huu kwa maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.