2017-04-06 13:30:00

Papa Francisko kuongoza mkesha wa Siku ya Vijana Kijimbo, 2017


Baba Mtakatifu Francisko ameanza "kuyavalia njuga" maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama kwa mkesha wa nguvu pamoja na vijana wa Jimbo kuu la Roma pamoja na majimbo jirani, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma, Jumamosi tarehe 8 Aprili 2017 kuanzia saa 11: 00 jioni kwa saa za Ulaya. Hii ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ambayo kwa mwaka huu inaadhimishwa katika ngazi ya Kijimbo. Hii ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayofanyika mwezi Oktoba 2018 mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”.

Yohane, Mwanafunzi aliyependwa sana na Yesu ndiye kiini cha tafakari ya mkesha wa Siku ya Vijana Duniani kwa ngazi ya Kijimbo, itakaongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma. Yohane ni mhusika mkuu katika maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana na kwamba, tafakari ya Utenzi wa Bikira Maria, “Magnificat” inawasindikiza vijana katika maadhimisho haya kwa kuzingatia kwamba, kuna matukio muhimu sana katika Ibada kwa Bikira Maria.

Haya ni pamoja na: Jubilei ya miaka 300 tangu Bikira Maria alipotokea huko Aparecida, Brazil na Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Watatu wa Fatima, yaani Francis, Yacina na Lucia. Wenyeheri Francis na Lucia wanatarajiwa kutangazwa kuwa ni Watakatifu, mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya katika vipaumbele vya maisha yao! Kumbe, mkesha wa Siku ya Vijana Kijimbo, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu hapa Roma, umeandaliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kushirikiana na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kujizatiti zaidi katika kufanya mambo msingi katika maisha: kwanza kwa kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji; kwa kuzingatia uhuru wa kweli sanjari na kushikimana na watu wote wenye mapenzi mema ili kujenga ulimwengu unaosimikwa katika udugu, upendo na mshikamano wa kweli. Itakumbukwa kwamba, wajumbe 270 kutoka katika nchi 103 na vyama 44 vya kitume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya wanashiriki katika kongamano la kimataifa ili kufanya tathmini ya kina mintarafu maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani, Jimbo kuu la Cracovia, tayari kuweka sera, mipango na mikakati ya maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa nchini Panama kunako mwaka 2019.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2017 inayoadhimishwa katika ngazi ya Kijimbo anasema, Mwenyezi Mungu anapomgusa kijana, anakuwa na uwezo wa kutenda mambo makuu katika maisha, kama yale ambayo Bikira Maria anazungumzia katika utenzi wake, mambo yanayogusa pia safari ya maisha ya vijana wengi katika wasi wasi na mashaka, wanaweza pia kupata utimilifu wake. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, vijana wanayo mapungufu yao, ni wadhambi, lakini Mwenyezi Mungu anapowaita anaangalia yale mambo msingi ambayo wataweza kutenda kwa siku za usoni kwa kujikita katika upendo. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, vijana wanaweza kutumia maisha yao katika kuboresha ulimwengu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kuacha alama katika historia yao wenyewe pamoja na jirani zao.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana wamba, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyeweza kuunganisha historia ya maisha yake na ya wahenga wake, hata wao wanahistoria ya Jumuiya ya watu waliowatangulia katika maisha, ni sehemu ya historia ya Kanisa inayofumbatwa katika Mapokeo yanayorithishwa kizazi baada ya kizazi kwa kurutubishwa na uzoefu wa kila mtu binafsi, kumbe hata wao ni sehemu ya historia ya Kanisa, mwaliko kwa vijana ni kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili waweze kuwa ni vyombo na wadau katika kazi ya ukombozi; kwa kuwajibika sanjari na kutambua matendo ya huruma ya Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anapenda kuwauliza ni kwa jinsi gani wanavyotunza kumbu kumbu za matukio mbali mbali ya maisha yao; madonda katika maisha; hakuna mtakatifu wala mdhambi asiyekuwa na historia ya mambo yaliyopita na yale yajayo! Yesu, kwa njia ya huruma na upendo wake, anaweza kuganga na kuponya majeraha yaliyojichimbia ndani kabisa ya mioyo ya watu na hivyo Mwenyezi Mungu kuonesha nguvu yake katika udhaifu wao. Vijana wajifunze kupokea historia ya maisha iliyopita, ili kuandika historia ya maisha yao kwa leo na kesho ijayo! Ni kazi ngumu lakini muhimu sana ili kutambua upendo wa Mungu unaounganisha matukio yote ya maisha.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga utamaduni wa kutafakari kuhusu maisha yao, tayari kujiwekea malengo kwa siku za usoni, ili kutengeneza historia ya maisha ya kweli kwa kutambua kwamba, wao wenyewe wanapaswa kuwa ni wahusika wakuu wa historia na watu wanaoamua mustakabali wa maisha yao kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kufuata mfano bora wa Mama Bikira Maria kwa kuwa wameungana na historia yao ya zamani. Jambo hili linawezekana kwa kuchunguza dhamiri kila siku ili kuangilia yale mema na mazuri waliyotenda kwa siku hiyo na mabaya yaliyowaangusha; kwa kushuruku, kutubu na kujikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Ni changamoto ya kusali kwa ajili, pamoja na juu ya maisha, ili kutambua matendo makuu ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Utenzi wa “Magnificat” unaonesha kwamba, Bikira Maria alikuwa anaufahamu mkubwa wa Maandiko Matakatifu; alifahamu sala ya watu wake urithi mkubwa kutoka kwa wazazi wake. Alikuwa ni msichana mwenye Ibada na amana kubwa ya imani iliyomwezesha kutunga utenzi wa “Magnificat” ambao umekuwa pia ni utenzi wa Kanisa. Changamoto kwa vijana ni kuifahamu Biblia, kulitafakari Neno la Mungu sanjari na kujenga utamaduni wa masomo ya kiroho yatakayopasha joto mioyo yao na kuangaza mapito wakati wa nyakati za giza. Bikira Maria anawafundisha vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Ekaristi kama alama ya shukrani kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; Sakramenti ya Upatanisho kama mwanzo na hatima ya maisha yao, kwa kupyaisha maisha yao ya kila siku yanayogeuka kuwa ni utenzi wa kudumu kwa Mwenyezi Mungu. Vijana wafanye kumbu kumbu ya uwepo wa Mungu katika maisha yao kwa kujikita katika huruma na furaha ili kufuta madoa ya ubaya katika maisha.

Bikira Maria katika utenzi wa “Magnificat” anasaidiwa kwa namna ya pekee na imani, mtazamo na maneno ya binamu yake Elizabeth kutambua ukuu wa matendo na utume wa Mungu ambao amemkabidhi Bikira Maria. Vijana wanapokutana na wazee, wawe ni chemchemi ya utajiri kwa kujifunza hekima na dira kutoka kwa wazee pamoja na kupokea ushuhuda wa watu waliowatangulia, ili kujenga kesho imara na thabiti zaidi. Vijana wakumbuke kwamba, wao wana nguvu, lakini wazee kumbu kumbu na hekima kama alivyoshuhudia Elizabeth.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuthamini Mapokeo na kuwa ni waaminifu kwa matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kutekeleza katika maisha yao ya sasa, changamoto ni kutambua asili yao ili kuweza kurejea tena katika mambo msingi, daima wakiwa na uaminifu unaojikita katika ugunduzi ili kuunda nyakati mpya ili kuendelea kuupyaisha ulimwengu. Vijana wawe na ujasiri wa kuthamini yaliyopita, yaliyopo na yale yajayo, kwa kuambata urithi wa tunu msingi za maisha ya ndoa, wito wa upadre na maisha ya kitawa; tunu ambazo kamwe haziwezi kupitwa na wakati bali yataendelea kuwa ni chemchemi ya furaha, ikiwa kama vijana watapata uzoefu na mang’amuzi ya upendo unaaomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao kwa kutambua na kuitikia wito kutoka kwa Mungu, jambo linalowawezesha kuwa na furaha ya kweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.