2017-04-06 07:25:00

Kanisa linataka kuwasikiliza vijana! Haya vijana kazi kwenu!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo linapenda kuwasindikiza vijana katika maisha na utume wao, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili katika medani mbali mbali za maisha. Kanisa litaendelea kujenga  na kuimarisha utamaduni wa kuwasikiliza na kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya ili kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao. Baba Mtakatifu kwa kutambua umuhimu wa utume wa vijana kama jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, ameamua kuitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa kunako mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE, hivi karibuni limeadhimisha Kongamano la Vijana Barani Ulaya lililoongozwa na kauli mbiu “Kuwasindikiza Vijana ili kujibu kwa uhuru kamili wito wa Kristo”. Jimbo kuu la Barcellona ndilo lililokuwa mwenyeji wa Kongamano hili kwa mwaka 2017. Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ni kuwarudisha tena Mababa wa Sinodi shuleni, ili kuwasikiliza, kutembea pamoja na kufanya mang’amuzi ya kina na vijana wa kizazi kipya.

Mababa wa Sinodi wanataka kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya. Ni wakati wa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini; kujadiliana; kupembua ili hatimaye, kufikia maamuzi ya kina yatakayoliwezesha Kanisa kuibua  sera na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya. Mwinjili Luka anapozungumzia jinsi Yesu alivyowatokea wafuasi wa Emau anasema, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao! Kardinali Baldisseri anasema kuandamana na vijana katika hija ya maisha ni mchakato ambao utalisaidia Kanisa kuwafunda vijana ili hatimaye, katika uhuru kamili waweze kuitikia wito wa Kristo Yesu.

Mama Kanisa anawaalika vijana kutoka katika mzunguko wa kujitafuta wenyewe ili kujiridhisha, mtazamo unaotawala katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kanisa linataka kuwaswalisha vijana, Je, ninyi vijana mko upande wa nani? Swali hili msingi linapaswa kufanyiwa kazi na vijana katika ujumla wao, huku wakisaidiwa na Mama Kanisa ili kufanya mang’amuzi ya kina. Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu inaendelea kuandaa Hati ya kutendea Kazi, “Instrumentum Laboris” ambayo inatarajiwa kukamilika kati kati ya mwaka 2017, ili iweze kutumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kwa tafakari zaidi ili hatimaye, Kanisa kuweza kupata mwelekeo mpana zaidi wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Mwezi Oktoba, 2018.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anakaza kusema, Bara la Ulaya kwa sasa linakabiliwa na changamoto tete za maisha, kwa mfano kwa sasa idadi ya watoto wanaozaliwa ni ndogo sana, kiasi kwamba, idadi kubwa ya watu ni wazee, hali ambayo ni changamoto kubwa hata katika maisha ya Kipadre. Kwa sasa kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora Barani Ulaya. Hii ni changamoto katika ukarimu kama moja ya tunu msingi za maisha ya Kiinjili!

Ukarimu kwa ajili ya kupokea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia nzima ya binadamu. Bara la Ulaya linapaswa pia kujielekeza zaidi katika mchakato wa kuwajumuisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha yake, kwa kufanya kumbu kumbu ya mambo mazuri yaliyowahi kutokea Barani Ulaya. Kwa bahati mbaya, vijana wa kizazi kipya Barani Ulaya inaonekana kuwa wamechoka na kuanza kuingia “pensheni hata kabla ya wakati”; ni watu wenye vurugu na watu wasiopenda mshikamano wa kijamii, mambo ambayo yanatishia amani na mafungamano ya kijamii.

Vijana kwa kukata tamaa ya maisha, baadhi yao wamejikuta wakijiunga na makundi ya kigaidi, uhalifu wa magenge na misimamo mikali ya kidini na kiimani, hatari kubwa kwa ulinzi na usalama. Vijana kwa kukosa mwelekeo na maana ya maisha, wanajikuta hata wao hawawezi kuwajali na kuwathamini wengine. Mama Kanisa anawataka vijana wa kizazi kipya kumwilisha mang’amuzi ya Sinodi kwa kuandamana na Kanisa katika ujumla wake. Vijana wajenge ujasiri wa kusikiliza kwa makini; kupembua kwa makini misimamo ya maisha na kuthubutu kuimwilisha mawazo yao chanya katika uhalisia wa maisha. Kumbe, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ni changamoto kwa Kanisa zima!

Kardinali Lorenzo Baldisseri anasema, vipaumbele vya Kanisa kwa utume wa vijana kwa wakati huu: Mosi, ni kuhakikisha kwamba, kweli Sinodi inaadhimishwa kama Sinodi kwa kuwapatia nafasi Mababa wa Sinodi kushirikisha mawazo, changamoto na suluhu katika maisha na utume wa vijana. Pili, Kanisa halina budi kuwasikiliza kwa makini vijana wa kizazi kipya na kujibu matamanio yao katika mwanga wa Injili. Tatu, ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linaibua mbinu mkakati kwa ajili ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya vijana; kwa kuwaonesha mambo wanayopaswa kufuata na kuzingatia na yale ambayo wanapaswa kuyaacha ili kutembea kweli katika mwanga wa Injili ya Kristo Mfufuka. Nne, ni kuwatia vijana shime kuota ndoto, kushiriki katika unabii na kuthubutu kutenda katika mwanga wa Roho Mtakatifu.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anakaza kusema, hadi sasa hakuna jambo ambalo tayari limekwisha amriwa, bali wanasubiri mawazo kutoka kwenye Mabaraza ya Maaskofu ili kutengeneza Hati ya Kutendea Kazi pamoja na majibu yanayoendelea kutolewa kwa njia ya mitandao ya kijamii. Vijana kwa namna ya pekee, wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa kutuma mawazo yao kwenye mtandao ufuatao: (www.sinodogiovani2018.va).

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.