2017-04-06 13:36:00

Fumbo la Mateso ya binadamu!


Swali kubwa na la mshangao kwa mwanadamu ni kwa nini Mungu mwema anaruhusu mateso. Kilio hiki kiko wazi tangu zamani za kale na hata wakati wetu huu. Katika maandiko matakatifu Ayubu anafika mahali anamwambia Mungu ampe jibu – Ayu. 31:37 Kadiri ya mawazo ya zamani, mateso yalihusishwa na dhambi. Katika kitabu cha Mwanzo tunaona kuwa mateso ya wazee wa kwanza yalikuwa ni sababu ya dhambi zao na sababu ya dhambi zao basi imeleta mateso, machungu na kifo ulimwenguni. Na hata wakati mwingine dhambi na mateso yakawa kama mahesabu, umekosa kiasi hiki basi dhambi yako na adhabu yako ni hii na kwa kiasi hiki. Hata leo hii, sisi na kama si wote tumebaki hapa au tunaendeleza  mtazamo huu.

Tunapoendelea kuangalia Maandiko Matakatifu tunaona kuwa Ayubu anagundua kuwa ufahamu wa ukweli wa Mungu juu ya fumbo la mateso ni tofauti kabisa na namna hii ya uelewa. Kitabu cha Ayubu kinafuta dhana hii. Hata hivyo Ayubu hatoi jibu la mwisho juu ya fumbo hili. Ila tunaona kuwa kadiri ya Ayubu, tukikaa katika fumbo la ukweli wa Mungu, tunatambua Fumbo la mateso linalomezwa na ukuu wa Mungu mwenyewe. Mtume Paulo katika Waraka kwa Warumi 8:3 anaonesha mwisho wa mateso ya mwili pale anaposema kuwa – kwa kuwa, yale ambayo Sheria iliyodhoofishwa na mwili haikuweza kuyatenda, Mungu ameyatenda: kwa kumtuma Mwana wake kwa ajili ya dhambi apokee mwili unaotawaliwa na dhambi (sawa na miili yetu), ili aihukumu dhambi kwa mwili wake. Kwa maana hii Yesu amefuta dhambi na maumivu yote yatokanayo nayo.

Tukiendelea mbele tunaona kuwa imani ya kikristo inatupatia mwanga zaidi. Kwa imani hiyo tunaona kuwa Mungu hutumia mateso ya mwanae kutekeleza nguvu yake ya kuokoa. Twaona kuwa kwa mateso ya Mwanaye, sisi tumepata wokovu. Hiki ndicho kiini cha liturjia yetu ya leo. Lakini fumbo linabaki. Hata katika tafakari ya kawaida tunaona kuwa anayetoka jasho, anayetoa sadaka ya kweli huwafaidisha wengine pia. Mmoja huteseka, hutoka jasho ili wengine wafaidi. Sadaka ya kweli inauma na kuumiza sana. Hakuna upendo wa kweli bila kutoa, bila sadaka. Hata sheria mojawapo rahisi kabisa ya kiuchumi inasema ukitaka kupata ni lazima uwekeze.

Hata Wainjili wetu hawatupi jibu la fumbo hilo – ni kwa nini Mungu atumie njia ya mateso, ingawa wanazungumzia  nguvu ya wokovu katika swala la ukombozi. Katika injili ya Marko 15:39 tunaona kuwa wakati wa kifo chake Yesu pale msalabani, yule askari alihamaki – hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu. Na hiki ndicho kiini cha Injili ya Marko – kwamba Yesu ni nani? Katika mateso yake Kristo, yule askari alitambua uwezo wa Mungu. Mwinjili Matayo 27:52-53 anaona wokovu uliotanguliwa na kifo chake na Mwinjili Yohane 22:30 anaona kutokana na kifo cha Kristo na kutupatia sisi roho wake.

Mwinjili Luka anaelezea ulazima wa mateso na kifo cha Yesu na utimilifu wa ahadi ya mpango wa Mungu wa ukombozi – 22:37 – kwani nawambieni, niliyoandikiwa lazima yatimizwe, yaani amehesabiwa pamoja na wakosefu. Basi yanihusuyo mini yanatimia sasa. Mtume Paulo anaeleza vizuri mpango huu. Anasema huku kujitoa kwake Kristo – kenosis, yaani kujishusha, kujimwaga, kujitoa, hata kuacha utukufu wake wa kimungu na kibinadamu na kukubali kifo, tena cha msalaba. Hakuna upendo zaidi ya huu. Kwa njia ya mateso, ametuinua na Mungu akamkweza juu kabisa na huu ukuu ukatuletea sisi wokovu.

Kwa hiyo tunaona kuwa kile kilichofungamanishwa na dhambi, yaani mateso, kinapewa maana mpya. Upendo wa Mungu unageuzwa kuwa utukufu. Na ndicho kinachoonekana leo hii. Mateso yanageuzwa kuwa wokovu. Fumbo linabaki, lakini maelezo yake na ukuu wake huonekana katika nguvu ya ukombozi. Ndugu zangu jibu la swali letu liko hapa, yaani kwa nini Mungu aruhusu mateso. Hata Ayubu anasema kuwa mateso hupoteza nguvu yake yakiangaliwa katika mtazamo wa Kimungu. Na hivvo leo tunaona kuwa kwa njia yake Kristo, mateso yanapoteza nguvu kwa sababu ya upendo wa Mungu unaoshinda hali zetu dhaifu. Upendo huu wa Kristo unatuwezesha leo kusali na kuimba – kwa ishara ya msalaba, tuokoe. Msalaba, katika maana hii, unakuwa wokovu na si laana.

Wito unaowekwa mbele yetu ni kwamba nasi tujiunge katika njia yake Bwana. Wiki hii kuu inatukumbusha tena ufuasi wetu, imani yetu n.k. Tusirudi nyuma, tubaki na Bwana mpaka ukamilifu wa dhahari. Tukibaki na Bwana, tutashinda. Adhimisho la tendo hili la mateso ya Bwana litupe nafasi ya kutafakari juu ya mahangaiko yetu na ya ulimwengu. Adhimisho hili linatupatia nafasi ya kutafakari kwa kina fumbo kuu la ukombozi kama alivyolitekeleza Bwana wetu Yesu Kristo. Tafakari hii itualike kujitoa bila kujibakiza kama alivyofanya Bwana. Kardinali Newman anasema sote tunateseka kwa ajili ya wengine na tunafaidika pia kutokana na mateso ya wengine, kwani hakuna aliye peke yake, ingawa siku ya hukumu kila mtu atasimama peke yake, lakini kwa sababu ya sadaka ya kila mmoja tunaamini kuwa tutakuwa tumebeba kundi kubwa pamoja nasi.

Tumsifu Yesu Kristo,

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.