2017-04-04 13:00:00

Papa: Udugu wa Mtakatifu Pio X: Sakramenti ya Upatanisho na Ndoa


Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limewaandikia Maaskofu wote barua kuhusu uamuzi uliofikiwa na Baba Mtakatifu Francisko mintarafu Udugu wa Mtakatifu Pio X, ambao kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mchakato wa kutaka kuurejesha tena katika umoja wa Kanisa. Baba Mtakatifu amewapatia Mapadre wa Udugu wa Mtakatifu Pio X ruhusa ya kuadhimisha Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linapaswa kuishi na kushuhudia huruma na kwamba, kila mwamini anapaswa kuwa ni chemchemi ya huruma.

Kwa kufuata mwelekeo huu wa shughuli za kichungaji unaotaka kuwahakikishia waamini dhamiri nyofu, licha ya uwepo wa vikwazo vya kisheria ambavyo vinaifanya Jumuiya ya Udugu wa Mtakatifu Pio X kuwamo kwa wakati huu, Baba Mtakatifu kwa kufuata ushauri uliotolewa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Tume ya Kipapa ya “Ecclesia Dei” yaani “Kanisa la Mungu”, ameamua kutoa ruhusa kwa Maaskofu mahalia uwezekano wa kuwaruhusu Mapadre hao kuadhimisha Sakramenti ya Ndoa kwa waamini wanaoshiriki katika utume wao kwa kuwepo wa Padre wa Jimbo ambaye ni mjumbe na mwakilishi ili kuweza kupokea nia za wanandoa watarajiwa wakati wa kuadhimisha Sakramenti ya Ndoa kwa kuzingatia taratibu, sheria na kanuni za “Vetus ordo” (Mapokeo ya zamani kabla ya Mageuzi ya Liturujia ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican) ikiwa kama Ibada hii ya Misa inaadhimishwa na Padre wa Jumuiya ya Udugu wa Mtakatifu Pio X.

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linasema, pale ambapo haiwezekani au hakuna Mapadre Jimboni wanaoweza kupokea nia ya wanandoa husika, Askofu mahalia anaweza kutoa kibali kwa Padre wa Jumuiya ya Udugu wa Mtakatifu Pio X ambaye pia atalazimika kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kumhimiza mhusika kupeleka nyaraka muhimu za Sakramenti ya Ndoa, kwenye Makao makuu ya Jimbo mapema iwezekanavyo. Kwa njia hii, Kanisa linataka kuwapunguzia msongo wa mawazo waamini wote wanaopata huduma kutoka kwa Mapadre wa Udugu wa Mtakatifu Pio X pamoja na kuhakikisha uhalali wa Sakramenti ya Ndoa. Utekelezaji wa maagizo haya unategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano kutoka kwa Maaskofu mahalia. Barua hii imeandikwa na kutiwa sahihi na Kardinali Gerhard L. Muller na Askofu mkuu Guido Pozzo viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.