2017-04-03 14:00:00

Papa Francisko shuhuda wa amani nchini Misri: Ratiba elekezi


Ratiba elekezi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inaonesha kwamba, ataondoka kutoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, Fumicino Ijumaa, tarehe 28 Aprili 2017 majira ya saa 4: 45 asubuhi kwa majira ya Saa za Ulaya na kuwasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo saa 8:00 kwa saa za Ulaya. Kutakuwepo na makaribisho ya kitaifa kwenye Ikulu ya Misri. Ratiba inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu atapata nafasi pia ya kumtembelea Rais wa Misri pamoja na Mufti mkuu wa Msikiti wa Alzhar. Viongozi hawa wawili watatoa hotuba kwa washiriki wa mkutano wa kimataifa kuhusu amani.

Majira ya saa10: 40 za jioni kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanasiasa na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao huko Misri. Rais wa Misri naye atapata nafasi ya kutoa hotuba kwa niaba ya viongozi wenzake. Baadaye jioni, Baba Mtakatifu atamtembelea Mheshimiwa Sana Papa Tawadros II na kutoa hotuba yake. Hivi ndivyo atakavyokuwa anafunga siku yake ya kwanza ya ziara ya kitume nchini Misri, ziara ya pili kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika, baada ya kutembelea Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Jumamosi tarehe 29 Aprili 2017, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa mahubiri yake. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wale wote watakaokuwa kwenye msafara wake, watapata chakula cha mchana pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Misri. Majira ya saa 9:15 kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko atakutana na kusali pamoja na wakleri, watawa na majandokasisi kutoka Misri pamoja na kuwapatia neno. Baadaye, itafuatia sherehe ya kuagana na saa 11: 00 Jioni kwa Saa za Ulaya, Baba Mtakatifu atakuwa anafunga vilago kutoka Misri, tayari kurejea mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baraza la Maaskofu Katoliki Misri linasema kwamba, Neno la Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inaonesha Mto Nile, alama ya maisha, Piramidi ambayo kimsingi ni alama ya utamaduni na maendeleo ya wananchi wa Misri. Msalaba na Mwezi ulioko kati kati ya picha ni kielelezo cha imani za wananchi wa Misri katika ujumla wao. Njia ni alama ya amani ambayo kila  binadamu anatamani kuipata; amani ndiyo inayoongoza hata kauli mbiu ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri. 

Wakati huo huo, Kamati ya maandalizi ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri inasema kwamba, kauli mbiu inayoongoza hija hiyo ni “Papa wa amani nchini Misri”. Hayo yameelezwa na Askofu Emmanuel Ayad Bushay wa Jimbo  la Kanisa na Kikoptik la Luqsor, Tebe, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya ujio huo. Hivi karibuni, Dr. Greg Burke msemaji mkuu wa Vatican alisema, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa na Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri, Baraza la Maaskofu Katoliki Misri, Mheshimiwa Sana Papa Tawadros II pamoja na Sheikh Ahmed Mohamed El Tayyib wa Msikiti Mkuu wa Al Azhar, mjini Cairo, ili kutembelea Misri kuanzia tarehe 28 - 29 Aprili 2017. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko atatembelea mji wa Cairo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.