2017-03-31 15:24:00

Liturujia inapaswa kumwilishwa katika maisha ya watu!


Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, imehitimisha Kongamano la Siku mbili lililofunguliwa hapo tarehe 30 – 31Machi 2017 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Hekima ya kutoka katika makazi ya watu wa kawaida: Liturujia kutoka chini”. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki amewakumbusha wajumbe wa kongamano hili kwamba, kimsingi ibada za watu wa kawaida zimezaliwa kutokana na umwilisho wa imani ya Kikristo katika tamaduni za watu wengi, hali ambayo uhitaji uhusiano wa mtu binafsi kwa kufanya rejea moja kwa moja kwa Mwenyezi Mungu.

Hizi ni ibada zenye zinazojikita katika ufahamu wa Mungu, Kristo Yesu na Bikira Maria. Ni Ibada ambazo Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema, zina sura na umbo kamili, zina uwezo wa kuongezeka na kusonga mbele. Tafiti mbali mbali zinaonesha kwamba, Ibada za watu wa kawaida zinafuata mkondo wa maisha ya binadamu: kwa kuzaliwa, kuku ana hatimaye huweza kutoweka. Ni uhusiano mwema unaojikita katika maisha ya kifamilia, kijamii na kikanisa.

Haya ni mambo ambayo kamwe hayapaswi kuwashanga waamini kutoka Makanisa ya Mashariki ambao wamezoea Ibada kuu kama ile ya kutangaza Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu, kwa kuambatana na alama makini kama vile: Moto, Neno la Mungu, Maji na Mwana Kondoo aliyechinjwa, akafa na kufufuka kwa wafu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo linasherehekewa kwa uzuri na ibada wakati wa Mkesha wa Pasaka ili kuonesha: Ukuu wa Mungu, upendo na Fumbo la Kanisa. Kardinali Leonardo Sandri amewatakia heri na baraka wajumbe wote wa Kongamano ili kweli matunda ya maadhimisho haya yaweze kujenga umoja na mshikamano, unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku wakati wa maadhimisho mbali mbali ya Liturujia ya Kanisa.

Kwa upande wake, Padre David E. Nazar, SJ., amewataka wasomi wanaofundwa kwenye Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema fursa hii kujipatia elimu, ujuzi na maarifa, ili wanaporejea tena  katika nchi zao, waweze kuwasaidia ndugu zao katika Kristo kuboresha hali ya maisha yao ya kiroho. Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na mambo mengine wataweza kuyapata kwa ziada. Waamini wa kawaida ni watu ambao wana imani thabiti sana katika maisha yao na wako tayari kuishuhudia kwa kuimwilisha katika vitendo. Wakristo wa Makanisa ya Mashariki wamepitia katika vipindi vigumu sana vya kihistoria na wamebaki imara, thabiti na mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ni watu ambao maisha yao yamesimikwa katika tunu msingi za Kiinjili; Utakatifu na Sala inayowaunganisha na Mwenyezi Mungu. Kimsingi, hawa ni mashuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao. Kumbe, kongamano la liturujia ilikuwa ni nafasi ya kusikiliza jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anazungumza na watu wake kutoka katika undani wa maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.